November 24, 2024

Jinsi ya kukabiliana na changamoto unapoanza mwaka 2021

Usihangaike na vitu ambavyo viko nje ya uwezo wako. Dunia bado inakuhitaji. Changamoto ni sehemu ya maisha, zinakufanya uwe imara zaidi.

  • Ni pamoja na kuyafahamu madhaifu yako na kuyarekebisha inapobidi
  • Kama umewahi kukata tamaa, huenda ulijikosesha fursa ya kupata au kuwa mtu mkubwa. Bado nafasi ipo.
  • Usikubali maoni ya watu juu ya uwezo wako yakufanye ujione dhaifu.

Dar es Salaam. Katika maisha haya ambayo kesho yako hauifahamu, changamoto na dharura huenda zimewahi kumpata kila mtu. 

Wapo walioamka asubuhi na kupewa taarifa za kuondokewa na mtu ambaye ni tegemezi kwao, wapo ambao biashara zilikufa, wapo walioibiwa simu na wapo ambao vibarua viliota nyasi. 

Haya ni baadhi ya matukio ambayo hutokea bila mtu kutarajia au kupanga. Ni dharura. Katika mazingira kama hayo, wengine hupata msongo wa mawazo na kuchukua hatua hasi dhidi ya maisha yao ikiwemo kujiua. 

Hata hivyo, usihangaike na vitu ambavyo viko nje ya uwezo wako. Dunia bado inakuhitaji. Changamoto ni sehemu ya maisha, zinakufanya uwe imara zaidi. 

Pale changamoto inapokukuta, ufanye nini?

Usiwe mwepesi wa kukata tamaa

Wewe siyo wa kwanza kukutwa na dharura hiyo inayokukumba. Wapo wengine wengi tu. Badala ya kukata tamaa, pata maoni ya watu wako wa karibu juu ya changamoto yako huenda yakakusaidia

Shoma Gibbe ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kiadventista cha Friedensau cha Ujerumani anayesomea shahada ya uzamiri ameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa wakati anaanza kusoma masomo yake nchini humo, alikua haelewi kitu darasani kutokana na changamoto ya lugha.

Alifikia hali ya kukata tamaa ili akatishe masomo yake lakini alipata suluhu katikati ya changamoto yake.

“Mwanafunzi kutoka Ghana alinisihi nisikate tamaa kwani hata yeye kipindi anaanza alipata changamoto kama yangu. Nilichokifanya nilikuwa naingia darasani narekodi voice sauti za profesa nikirudi chumbani naanza kusikiliza upya alikuwa anasema nini,” amesema Gibbe ambaye sasa yupo mbioni kumaliza masomo yake yaliyomchukua miaka miwili.

Wakati mwingine uamuzi unaofanya katika maisha yako, unaweza kukuweka mbali na wategemezi wako, jambo ambalo linaibua changamoto nyingi. 

Emmanuel Mkuya amesema, aliwahi kusitisha masomo yake ili kutafuta pesa kujikomboa kiuchumi. Baada ya wazazi wake kugundua, waliacha kumhudumia kwa kuwa walikasirishwa na maamuzi yake.

“Kodi ilikua imeisha, ilinibidi nianze kulala ofisini, nikajichanga nikafungua biashara ya chips nayo ikafa baada ya ugonjwa wa corona kutangazwa, sikukata tamaa, niliendelea kupambana,” amesema Mkuya ambaye ni msanifu wa picha (Graphic Designer).

Pambana kutafuta furaha itakayokufanya utabasamu wakati wote hata kama unakabiliwa na changamoto mbalimbali. Picha| freepik.com

Amini juu ya uwezo wako

Pale unaposhindwa kupita katika mashindano au usahili fulani, haimaanishi kuwa hauna uwezo. Ubora na madhaifu yako unayajua wewe mwenyewe.

Mathalan, kwa Zipporah Zealot ambaye ni mwanamuziki aliwahi kukatalliwa licha ya kuamini juu ya kipaji chake cha uimbaji.

Zealot anasema “nilihisi kabisa kwa uwezo wangu nitakua kati ya washindi lakini haikua kama nilivyo tegemea. Changamoto zilikua nyingi, na mashindano yaliisha sikubahatika kuwa mshindi, hii ilinifanya nijisikie vibaya sana na nilikata tamaa kabisaa, nilijihisii siwezi.”

Kwa mujibu wa binti huyo, ilimchukua muda kujua kuwa yale yalikuwa ni mashindano tu na yeye ni bora kuliko mashindano.

Kwa sasa Zealot anayetamba na wimbo wa “Kona” anaendelea na safari yake ya muziki huku akiamini na kutumia vyema uwezo uliopo ndani yake. 

Na wewe amini uwezo ulionao katika kuboresha maisha yako. Usikubali changamoto zikurudishe nyuma.

Pata muda wa kufikiri na kufanya maamuzi muhimu

Kuna maamuzi sahihi na maamuzi muhimu katika kila changamoto. Mfano kama ukiibiwa simu, huenda maamuzi sahihi ni kuifuatilia simu hiyo ili kuona uwezekano wa kuipata. 

Hata wakati unafanya hivyo, kumbuka huenda watu wanakutafuta na hawakupati.

Maamuzi muhimu katika hali kama hiyo ni kupata simu itakayokuwezesha kuwa na mawasiliano, wakati unafuatilia simu yako ama unajikokota kununua simu nyingine.

Unaweza kujua yapi ni maamuzi muhimu na sahihi kwa kupima uzito wa maamuzi yoyote utakayoamua kuchukua.

Mwaka huu fanya maamuzi muhimu kwa kila changamoto utakayopata wakati ukitafuta kesho yako nzuri.


Soma zaidi


Jifunze kukubali mapungufu na kuyafanyia kazi 

Zipo changamoto zingine zinazosababishwa na makosa yetu wenyewe mfano uzembe, kutokujifunza na kushindwa kusikiliza maonyo tunayopewa na watu wa karibu.

Hivyo ni muhimu kufahamu madhaifu yetu na kujifunza namna ya kujiboresha. Mfano, mtu ambaye hatimizi majukumu yake kazini na kuishia kufukuzwa kazi, huenda aliwahi onywa juu ya utendaji kazi wake na marakifi lakini hakusikiliza. 

Tunapaswa kujiboresha kila siku na kutafuta suluhu kwa kila changamoto inayoibuka mbele yetu na siyo kulalamika na kukata tamaa. 

Mwaka 2021 ni wako, pambana kutafuta furaha itakayokufanya utabasamu wakati wote hata kama unakabiliwa na changamoto mbalimbali.