July 8, 2024

Jinsi ya kukabiliana na tatizo la kipandauso

Ni pamoja na kuepuka vichochezi ikiwemo mwanga mkali, sauti kubwa na msongo wa mawazo.

  • Kukaa mbali na mazingira yanayoweza kukupatia msongo wa mawazo.
  • Epuka unywaji wa pombe uliopitiliza.
  • Kaa mbali na mwanga mkali hasa wa jua na epuka sehemu zenye kelele.

Dar es Salaam. Wakati baadhi wakiuchukulia ugonjwa wa kipandauso kama maumivu ya kichwa, mamia ya wahanga wa ugonjwa huo wameendelea kuhangaika na hali hiyo kwa muda mrefu bila matibabu ya uhakika.

Katika andiko lililopita, Mtaalamu wa afya kutoka jijini Dar es Salaam Dk Brendavida Kaseko ameweka wazi kuwa ugonjwa wa kipandauso hauna matibabu ya kudumu bali wataalamu wa afya wanapojua kuwa mtu anasumbuliwa na ugonjwa huo wanamshauri kukaa mbali na visababishi ikiwemo msongo wa mawazo.

Hata hivyo, zipo dawa ambazo zinauzwa katika maduka ya dawa zisizohitaji melekezo ya daktari (over the counter drugs) ambazo mtu anaweza kutumia kutuliza maumivu.

“Ibuprofen, Acetaminophen, Triptans ni kati ya dawa ambazo huwa tunawapatia wagonjwa wa kipandauso,” ameeleza Dk Kaseko.

Mbali na matibabu ya dawa, vipo vitu vingine ambavyo mtu mwenye kipandauso anaweza kuviepuka ili kutokupata shambulio hilo:

1: Kukaa mbali na mazingira yanayoweza kukupatia msongo wa mawazo

Kwa baadhi ya wagonjwa wa kipandauso, shambulio husababishwa na msongo wa mawazo ambao unaweza kuchochewa na mazingira yanayowazunguka watu ikiwemo kazi, familia na majukumu ya kila siku.

Dk Kaseko amesema endapo mtu mwenye kipandauso anapohisi kuwa kazi, familia na mazingira aliyopo yanampatia msongo wa mawazo, anashauriwa kuepukana na mazingira hayo kwa kuchukua likizo ya kazi, au kwenda mbali na nyumbani na kufanya mambo anayoyapenda ikiwemo utalii, kusoma vitabu mbalimbali vya mambo anayoyapenda na kufanyia kazi kipaji chake. 

Kwa baadhi ya wagonjwa wa kipandauso, shambulio husababishwa na msongo wa mawazo, hofu na kukosa muda wa kupumzika. Picha| Business Insider.

2: Kuepuka unywaji wa pombe uliopitiliza

Matumizi ya pombe kwa wagonjwa wa kipandauso huwa na madhara yanayotofautiana kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine. 

Tovuti ya afya ya WebMD inaeleza kuwa matumizi ya pombe yanaweza kusababisha aina mbili ya kipanda uso. Cha kwanza ni cha hapo kwa hapo ambacho hutokea baada ya muda fulani.

“Unaweza usipate shambulio hadi utakapoamka. Aina hii ya kuumwa kichwa inaweza kumpata mtu yeyote japo kwa wagonjwa wa kipandauso, wapo katika hatari zaidi hata wakitumia kiasi kidogo cha pombe,” imeeleza tovuti hiyo.

Tovuti hiyo inashauri unapokunywa pombe, pata chakula pia. Usitumie pombe kama una msongo wa mawazo.

3: Epuka sehemu zenye mwanga mkali na kukaa juani

Mazingira yanayoweza kumkutanisha mtu na mwanga ni pamoja na kutembelea sehemu za starehe kama baa na disko pia uendeshaji wa gari nyakati za usiku pale pikipiki inapokua mbele yako na kukumulikwa kwa mwanga mkali.

Katika hali hizo, baadhi ya wagonjwa wa kipandauso hujikuta wakipata shambulio na kupata maumivuya kichwa yanayoweza kudumu kwa muda mrefu.

Tovuti ya Theraspecs inayojihusisha na masuala ya miwani imeandika, asilimia 89 ya watu zaidi ya 4000 waliofanyiwa utafiti wa kipandauso wamesema mwanga mkali kuwa moja ya visababishi vya shambulio la kipandauso.

Kwa mujibu wa Theraspecs, pale mwanga mkali unapompata mtu mwenye ugonjwa huo, mishipa ya macho inayounganika na kichwa hushtuka na hivyo kusababisha kichwa kupata maumivu ya muda mfupi au muda mrefu.

Pia, vichochezi vingine ni pamoja na kushindwa kula kwa wakati, kukaa kwenye sehemu za kelele kwa muda mrefu na kutokupata muda wa kupumzika.

Baadhi ya wagonjwa kipandauso hushindwa kutimiza majukumu yao kwani hali hiyo huchukua muda mrefu kabla ya kurudi kwenye hali ya kawaida. Picha| Deposit Photos.  

Unawezaje kuepuka shambulio la kipandauso?

Endapo mtu anajijua kuwa ana ugonjwa wa kipandauso, anatakiwa kuanza kuweka taarifa ya nini husababisha mashambulio yake ili aepukane na mazingira hayo na kufika hospitali ili kupata ushauri wa daktari.

Una historia gani na kipandauso, unaweza kutufikishia maoni yako kupita barua pepe ya newsroom@nukta.co.tz ili na wengine waelimike.