July 8, 2024

Jinsi ya kuwashinda matapeli wanaotaka kunufaika na Corona

Usiwe mwepesi kufungua viunganishi, vimbatanisho na nyaraka ulizotumiwa kwenye barua pepe au mitandao ya kijamii kama una mashaka nazo.

  • Kuwa makini kwa kila ujumbe unaopata mtandaoni unaokuelekeza kutoa taarifa zako binafsi.
  • Usiwe mwepesi kufungua viunganishi, vimbatanisho na nyaraka ulizotumiwa kwenye barua pepe au mitandao ya kijamii kama una mashaka nazo.

Dar es Salaam. Wakati janga la ugonjwa la virusi la Corona likizalisha tatizo lingine kubwa la habari za uzushi, wapo baadhi watu wanatumia janga hilo kuwatapeli watu mtandaoni na kuwaachia maumivu zaidi. 

Watu hao hutumia njia ya kutuma ujumbe kwa barua pepe, meseji za kawaida (SMS) na WhatsApp kuwataka watu kuchangia fedha kwa ajili ya mapambano dhidi ya COVID-19.

Wengine huenda mbali zaidi na kudukua taarifa za ugonjwa huo ili kuzitumia kwa manufaa yao binafsi. 

Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema njia rahisi ya kuepuka utapeli huo ni kuwa makini kwa kila ujumbe unaoupata hasa kama umeambatana na viunganishi, maelekezo au nyaraka zinakutaka kufanya jambo fulani. 

Maelekezo hayo wakati mwingine humtaka mtu kutuma taarifa muhimu za kifedha au neno la siri la barua pepe au akaunti ya benki ili kuzitumia visivyo. 

Katika mazingira hayo unatakiwa kufanya nini?

WHO, shirika lililo mstari wa mbele kupambana na COVID-19 duniani, limetaja mambo yatakayokusaidia kuzishinda mbinu za matapeli wa mtandaoni hata kama wana nguvu kiasi gani.

Chunguza kwa makini barua pepe

Mara nyingi wadukuzi hutumia barua pepe kutuma ujumbe. Angalia anuani ya barua pepe waliyotumia kama inatoka katika mamlaka husika na kama unaweza wapigie wahusika wakuthibitishie kama wametuma taarifa yoyote kwako inayokutana uchukue hatua fulani.

WHO imesema hii itakuweka salama zaidi kwa sababu utaepuka kufungua ujumbe wa barua pepe husika na kuingia katika matatizo zaidi.

Siyo kila barua pepe unayopokea ina habari njema. Zingine zinatumiwa na matapeli. Picha|Mtandao. 

Kuwa makini na viunganishi

Wakati mwingine  watu hao hutuma viunganishi (links) za mtandaoni ambazo zinakupeleka sehemu nyingine. 

Kabla ya kufungua kiunganishi au kiambatanisho ulichotumia jihakikishie kama ni salama kwako kabla ya kuingia katika mtego.

Mathalan, viunganishi vyote vya WHO huanza hivi ‘https://www.who.int’ au wizara ya afya ya Tanzania https://www.moh.go.tz/ si vinginevyo. Nenda kaangalie mtindo wa viunganishi wa vya taasisi iliyotumika kutuma ujumbe ili kuwa na uhakika.


Soma zaidi: 


Usitoe taarifa zako binafsi

Shirika hilo linasema kuwa jiulize kwanini mtu anataka taarifa zako binafsi kwa njia isiyo sahihi? Hakuna sababu ya mtu kutaka neno siri na jina lako ili kupata taarifa ya umma. 

Usikubali kuyumbishwa na mtu yoyote mtandaoni anayetumia Corona kutaka kuingilia usiri wako na kuutumia vibaya kuleta madhara. 

Usiwe mwepesi wa kuchukua hatua

Waharifu wa mtandaoni hutumia dharura  na majanga makubwa kama COVID-19 kuwafanya watu wachukue hatua ya kufanya kitu fulani kwa haraka bila kufikiria. 

Wakati wote tulia na pata muda mzuri wa kufikiri kuhusu ujumbe uliotumia au kuombwa fedha mtandaoni ili kufahamu kama umetoka mahali sahihi na una maana katika mapambano ya ugonjwa huo na si vinginevyo. 

Tulia kwanza kabla hujachukua hatua ya kujibu ujumbe uliotumiwa. Hakiki kama aliyekutumia ana nia njema. Picha|Mtandao.

Usitaharuki kama umetoa taarifa zako muhimu

Huenda unasoma habari hii ukiwa tayari umetuma taarifa zako binafsi kwa watu ambao unaamini siyo wema na ulifanya makosa. Hutakiwi kuhuzunika wala kutaharuki maana bado una nafasi kubwa ya kuwashinda.

Kama ulituma neno la siri la barua pepe, mitandao ya kijamii au akaunti ya benki, badilisha mara moja kila mahali ili wasifikie taarifa zako. 

Unakumbushwa ukiona uhalifu wa namna hiyo, toa taarifa katika mamlaka husika ikiwemo polisi na mamlaka za afya ili hatua zichukuliwe na watu wengine wapate msaada. 

Kwa kufanya hivyo, tutakuwa tunaimarisha mapambano dhidi ya COVID-19 kwa kulinda afya zetu na maisha yetu. 

Usisahau Corona bado ipo. Chukua tahadhari kwa kunawa mikono mara kwa mara, usiguse pua, mdomo au macho, vaa barakoa na epuka mikusanyiko isiyo kuwa ya lazima.