Jipange kabla ya kuanzisha biashara
Kabla hujaanza kufanya biashara wafahamu wateja, washindani wako na jinsi ya kupata mtaji kuendeleza biashara yako.
- Wafahamu wateja, washindani wako na jinsi ya kupata mtaji kuendeleza biashara yako.
- Jipange usiwe na haraka ya kufanya biashara ambayo hujaifanyia utafiti, hutafika mbali.
Wewe ni kijana ambaye umemaliza chuo na upo nyumbani? Unatamani kuanzisha biashara ndogo kukuingizia kipato wakati ukisubiri kuajiriwa au kuwa na biashara kubwa? Lakini hujui uanzie wapi?
Yapo mambo muhimu unayotakiwa kufikiri kabla ya kuanzisha biashara yoyote ili kujenga msingi wa mawazo na kukua kwa biashara yako hapo baadaye.
Fahamu jinsi ya kupata mtaji
Fikiria ni wapi unapata mtaji wa kuanzisha biashara yako. Kama una ndugu au marafiki wanaokuamini ni vema wafuate wakupe pesa utakazowekeza katika biashara.
Baada ya kupata mtaji, ni vema kupangilia matumizi ya pesa wakati ukifanya biashara ili kuhakikisha unapata faida na kuweka akiba itakayotumika kuikuza biashara yako na kuepuka kukopa pesa mara kwa mara.
Wafahamu wateja wako
Kabla hujaaanza biashara inabidi ung’amue na kujua bidhaa yako utamuzia nani na soko lako litakuwa wapi. Jiulize wateja wako ni watu wa hadhi gani? Wanaendana na bidhaa yako? Ni wa umri upi?
Baada ya hapo tafuta njia za kuwafikia kwa kusoma tabia zao wanapendelea nini. Mitandao ya kijamii inaweza kuwa njia rahisi kuwapata na kuitangaza bidhaa yako.
Usisahau kuwa balozi wa kwanza wa biashara yako ni wewe. Ipe sifa inayostahili bidhaa yako huku ukikumbuka kuwa utapata wateja wengi kama utaweza kukidhi mahitaji ya walaji.
Soma zaidi:
- Acha kuwaza kufanya biashara, fanya biashara
- Mambo ya kuzingatia unapoanzisha ‘brand’ yako ya biashara
Unapaswa kujua washindani wako ni kina nani
Katika biashara yoyote unayoanzisha fahamu kuwa wapo watu waliofanya kabla yako na wanaofanya vizuri zaidi, lakini isikutishe kwasababu kila mtu kwenye biashara ana mbinu zake za kufanikiwa.
Sasa wasome wapinzani wako wanachokifanya na wapi wanakosea ili usirudie makosa yaleyale na unatakiwa ujifunze zaidi kwa kiasi gani wanafanya kazi zao.
Mfanyabiasha na mwanzilishi wa kampuni ya Alibaba Jack Ma aliwahi kusema “Jifunze kwa mpinzani wako lakini usimuige anachofanya, ukiiga tu umekufa.”
Hivyo usisite kuuliza kwa watu wanaofanya biashara kama unayoifikiria wakwambie changamoto zao, au unaweza kuwachunguza taratibu kwa kutembelea biashara zao.
Biashara ni mipango kabla hujaanza kufanya kaa chini tafakari ni jinsi gani utaiendesha. Picha| NaijaGoDigital
Panga mipango yako vizuri
Baada ya kufanya utafiti wa awali sasa uko tayari kuanza biashara yako. Weka mipango yako vizuri ili kuhakikisha biashara inakuwa endelevu.
Hii itakusaidia kufuatilia mwenendo wa biashara yako kwa ukaribu na kuhakikisha unapata faida uliyokusaidia. Mipango inayozungumzwa hapa ni pamoja na kuhakikisha bidhaa inapatikana wakati wote, huduma kwa wateja inakuwa nzuri na mazingira ya kufanyia biashara yanaboreshwa.
Usiwe na haraka hakikisha kila kitu kinaenda kutokana na mipango uliyojiwekea.