November 24, 2024

Kairuki atoa maagizo mazito uwekezaji Tanzania

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika uwekezaji, Angellah Kairuki amekitaka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kuwafikia kikamilifu wawekezaji wazawa hususani waliopo mikoani ili kuwatambua na kuwaelimisha kuhusu fursa zinazotolewa na taasisi

Meneja wa Kiwanda cha kutengeneza Kahawa cha Wilaya ya Mbinga (MCCCO) Mhandisi Rabbian Uromi akitoa maelezo kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Angellah Kairuki kuhusu mitambo ya kutengeneza mifuko (magunia) ya kuhifadhia kahawa katika kiwanda hicho kilichopo mkoani Ruvuma wakati wa ziara yake Septemba 23, 2019. Picha| Ofisi ya Waziri Mkuu.


  • Amekitaka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kuwafikia kikamilifu wawekezaji wazawa ili kuwatambua na kuwaelimisha kuhusu fursa zinazotolewa na taasisi hiyo.
  • TIC yamjibu yasema imefungua ofisi saba za kanda kuwafikia wawekezaji wazawa. 

Dar es Salaam. Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika uwekezaji, Angellah Kairuki amekitaka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kuwafikia kikamilifu wawekezaji wazawa hususani waliopo mikoani ili kuwatambua na kuwaelimisha kuhusu fursa zinazotolewa na taasisi hiyo.

Amesema hatua hiyo itawapa fursa ya  kugakua mazingira ya wafanyabiashara na wawekezaji, jambo litakalowasaidia katika mipango ya uwekezaji nchini. 

“Ninawaagiza TIC mfike katika viwanda hivi ndani ya siku saba kuanzia sasa ili kuwatembelea na kuwaeeleza huduma zinazotolewa na taasisi yenu ikiwemo fursa zilizopo na endapo wataona inafaa wajisajili kwa kuwa ni suala la  hiari,” amesema Waziri Kairuki.

Waziri huyo alikuwa akizungumza jana (Septemba 24, 2019) alipotembelea na kukagua kiwanda cha kutengeneza kahawa cha Wilaya ya Mbinga cha MCCCO pamoja na kiwanda cha DAE kwa lengo la kukagua mazingira na utendaji wa viwanda hivyo mkoani Ruvuma.

Waziri Kairuki alitoa maelekezo hayo baada ya kubaini kuwa kituo hicho  hakijawafikia wawekezaji wazawa kikamilifu hususani waliopo mikoani ili kuwatambua na kuwaelimisha kuhusu fursa zinazotolewa na taasisi hiyo.

“Naelewa kuwa ipo miradi mingi iliyofikiwa na TIC zaidi ya asilimia 72 hivyo niwatake mfike haraka mkoani Ruvuma hususan katika viwanda hivi vya kahawa, ili kuvitambua na kueleza fursa na umuhimu wa kujisajili na Taasisi hii ili kuendelea kuchangia na kuwa na tija zaidi katika uchumi wa nchi,”amesisitiza.


Zinazohusiana: 


Ripoti ya Urahisi wa kufanya Biashara (Doing Business 2019) imeeleza kuwa Tanzania imeshika nafasi ya 144 kati ya nchi 190 katika urahisi wa kufanya biashara duniani ikiwa imeshuka nafasi 7 kutoka 137 mwaka 2018.  Na ndiyo mwaka ambao imefanya vibaya zaidi ukulinganisha na miaka mitano iliyopita.

Kulingana na vigezo vya ripoti hiyo, Tanzania imeangushwa na mchakato mrefu wa upatikanaji wa vibali vya ujenzi, leseni, usajili wa biashara na changamoto za ulipaji kodi.

Mkurugenzi wa Sera Mipango na Utafiti wa TIC, Mafutah Bunini amesema katika kuboresha utendaji wao wamefungua ofisi za kanda saba ili kuwafikia kwa urahisi wawekezaji wa ndani na kwamba wanatoa uzito sawa kwa wawekezaji wa ndani na nje.