October 6, 2024

Kamati ya vigogo 14 kushauri biashara kukabiliana na Corona Tanzania

Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) imeunda kamati maalum ya vigogo 14 itakayokuwa inatoa ushauri kuhusu hatua muhimu za kuchukua kuendeleza biashara dhidi ya athari za ugonjwa virusi vya Corona

  • Kamati hiyo ina wajumbe 14 kutoka taasisi za sekta binafsi.
  • Itakuwa inatoa ushauri wa kitaalam kuhusu biashara na uwekezaji wakati na baada ya mlipuko wa Corona. 

Dar es Salaam. Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) imeunda kamati maalum ya vigogo 14 itakayokuwa inatoa ushauri kuhusu hatua muhimu za kuchukua kuendeleza biashara dhidi ya athari za ugonjwa virusi vya Corona unaoendelea kusambaa maeneo mbalimbali duniani. 

Janga hilo la dunia limevuruga shughuli za kibiashara na uzalishaji, jambo linalotishia anguko la kiuchumi na kuzorota kwa utoaji wa huduma muhimu za kijamii. 

TPSF katika taarifa yake imeeleza kuwa kamati hiyo inajumuisha wataalam kutoka taasisi na kampuni za sekta binafsi ili kutoa msaada wa kitaalam utakaosaidia kunusuru biashara wakati huu wa mlipuko wa COVID-19.

“Watashauri kuhusu fursa na vihatarishi vya biashara vinavyotokana na athari za COVID-19 katika ngazi zote za sekta binafsi,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo ikielezea maeneo ambayo kamati hiyo itahusika nayo. 

Pia kamati hiyo itatoa ushauri wa miradi na programu za kimkakati zinazoweza kuanzishwa na Serikali na wadau wa maendeleo baada ya janga hilo kuisha na hali kurudi katika hali ya kawaida. 

Kazi nyingine itakuwa ni kutoa mapendekezo ya kisera kwa Serikali juu ya kukabiliana na athari za COVID-19. 


Zinazohusiana: 


Wajumbe wa kamati hiyo ni pamoja na Mshauri binafsi Dk Hosena Runogelo, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tafiti za Kiuchumi na Kijamii (ESRF) Tausi Kida, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Bankable Tanzania, Lawrance Mafuru, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya bia Tanzania (TBL) Philip Redman na Mshauri Binafsi, Dk Charles Kimei.

Wengine ni Susan Mashibe (Mkurugenzi Mtendaji VIA Aviation), Dk Joyce Mapunjo (Mshauri binafsi), Michal Bacham (Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Sigara Tanzania), Geoffrey Kirenga (Mkurugenzi Mtendaji-SAGCOT) na  Jennifer Bash (Mkurugenzi Mtendaji wa Alaska Tanzania).

Wengine ni John Ulanga (Mkurugenzi Mkazi-TMEA), Edwin Bruno (Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Smart Codes Tanzania), Seif Said Seif (Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Superdol Tanzania) na Aloys Bashebe (Mkurugenzi Mwenza wa kampuni ya Aloys&Associates). 

Machi mwaka huu, TPSF ilifanya utafiti wa kuhusu athari za COVID-19 katika shughuli za biashara, uchumi na sekta ya fedha ili kuwezesha wadau wa sekta binafsi kufanya maamuzi sahihi katika uwekezaji. 

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Smart Codes Tanzania, Edwin Bruno amesema ni heshima kubwa kuchaguliwa kuwepo katika kamati hiyo na yuko tayari kutoa na kubadilishana mawazo ya jinsi ya kupambana na COVID-19 nchini. 

Amesema ili kamati hiyo ifanikiwe kutimiza kazi zake inahitaji ushirikiana na msaada kutoka wadau wote wa sekta binafsi.