October 7, 2024

Kamati yabaini matatizo maabara ya kupima corona Tanzania

Kamati hiyo imebaini kuwa moja ya mashine za kupimia virusi hivyo ilikuwa na hitilafu kwa takriban miezi miwili.

  •  Imebaini mashine mojawapo ya kupima corona ilikuwa na matatizo kwa takriban mieizi miwili.
  • Serikali yaanza kupima corona katika maabara mpya.

Dar es Salaam. Serikali imesema kamati iliyoundwa kuchunguza maabara ya taifa ya jamii kuhusu mwenendo wa upimaji virusi vya corona imethibitisha mashaka aliyokuwa nayo Rais John Magufuli baada ya kubaini kuwa moja ya mashine za kupimia virusi hivyo ilikuwa na hitilafu kwa takriban miezi miwili.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto amewaambia wanahabari jijini Dar es Salaam kuwa kamati hiyo imebaini mapungufu katika kadhaa katika shughuli hiyo ya upimaji wa ugonjwa wa virusi vya Corona (COVID-19).

Mapema mwezi huu waziri huyo aliunda kamati ya wataalamu 10 kuchunguza kwa kina mwenendo wa utendaji wa maabara ya Taifa ya jamii katika upimaji wa COVID-19 baada ya Rais Magufuli kuonyesha mashaka kutokana na vipimo hivyo kubaini baadhi ya vitu visivyo binadamu kama mbuzi na papai kuwa na corona.

“Mojawapo ya mashine za kupima sampuli za COVID-19 ilikuwa na hitilafu kwa takriban miezi miwili bila ya uongozi wa maabara kuchukua hatua za kuifanyia matengenezo,” amesema Ummy Jumamosi (Mei 23, 2020).

Ummy amesema kamati hiyo imebaini kuwepo kwa mapungufu katika mfumo wa kimuundo, kiutendaji na uendeshaji wa kitaaluma katika upimaji wa vipimo, uhakiki wa ubora wa majibu.


Soma zaidi: 


Kamati hiyo, iliyokuwa ikiongozwa na Profesa Eligius Lyamuya wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Muhimbili (Muhas), imebaini pia udhaifu katika uhifadhi wa vipimo vya COVID-19.

“Aidha, imebainika uwepo kwa upungufu wa wataalamu wenye sifa mafunzo ya biotechnology (Bioteknolojia) and ‘molecular biology’ katika sekta ya afya ikiwemo katika maabara kuu ya taifa ya afya iliyopo NIMR,” amesema waziri huyo.

Katika kuboresha shughuli za upimaji, Ummy amesema hivi sasa upimaji wa sampuli zote za COVID-19 unahamishiwa katika maabara mpya ya Taifa ya jamii iliyopo Mabibo jijini Dar es Salaam na kutoka katika maabara ya zamani iliyopo ofisi za Taasisi ya Taifa ya utafiti wa magonjwa ya binadamu (NIMR).

Ummy amesema wameshaandaa wataalam wenye sifa na vigezo kwa ajili ya maabara hiyo mpya na kwamba wameanza kurekebisha mfumo wa utawala, utendaji na kitaaluma ndani ya maabara ya Taifa. 

Kituo cha Kudhibiti Magonjwa cha Afrika (AfrikaCDC) kimebainisha kuwa hadi Mei 23 Tanzania ilikuwa imerekodi wagonjwa 509 wa corona. Kati ya hao, 167 wameshapona ugonjwa huo huku 21 wakipoteza maisha.

Tanzania haijatangaza wagonjwa wapya tangu Aprili 29 mwaka huu.