October 7, 2024

Kampeni ya mtandaoni inavyochagiza upandaji miti duniani

Kasi ya kupanda miti imekuwa ndogo kutokana na changamoto ya janga la Corona ambayo imesimamisha shughuli nyingi za kijamii duniani.

  • Ni muendelezo wa kampeni ya mdau wa mtandao wa YouTube Jimmy Donaldson wa kupanda miti milioni 20 duniani mwaka huu. 
  • Alianza mwaka jana lakini Corona imevuruga kampeni hiyo iliyoanzia mtandaoni.
  • Mpaka sasa wamefanikiwa kupanda miti milioni 5.8.

Dar es Salaam. Mitandao ya kijamii ni miongoni mwa nyenzo muhimu kufanikisha ajenda za kijamii ikiwemo maendeleo. Wapo ambao wanatumia kwa kuwasiliano lakini wengine wanatumia kama fursa ya kuboresha maisha ya watu. 

Jimmy Donaldson maarufu kama Mr Beast ambaye mwishoni mwa mwaka 2019 aliweka azimio la kupanda miti milioni 20 katika mabara sita duniani ikiwemo Afrika ifikapo mwaka huu wa 2020. 

Donaldson ambaye ni raia wa Marekani alifanikiwa kuchagisha 46.46 bilioni ambazo zitatumika kupanda miti hiyo duniani kote ikiwa ni mchango wake wa kupambana na mabadiliko ya tabia nchi yanayotokana na ukataji wa miti. 

Hata hivyo, Mr Beast na wadau wengine wa mazingira watakuwa na kibarua kigumu cha kukamilisha azma yao kwa sababu mpaka sasa wamefanikiwa kupanda miti milioni 5.8 mpaka sasa sawa na asilimia 29.1 ya miti yote inayopaswa kupanda katika kampeni hiyo. 

Kasi ya kupanda miti imekuwa ndogo kutokana na changamoto ya janga la Corona ambayo imesimamisha shughuli nyingi za kijamii duniani.

Kwa Kenya, miti 450,000 imepandwa kwenye msitu wa Kijabe ambao unategemewa na vyanzo vya maji nchini humo kwa asilimia 75. Picha| Bham Now.

Maeneo yaliyofaidika na kampeni hiyo

Nchi za Kenya, Madagascar na Msumbiji ni miongoni mwa nchi ambazo zimefaidika na kampeni ya upandaji miti ambapo itasaidia kuhifadhi mazingira katika bara la Afrika na duniani. 

Kwa Kenya, miti 450,000 imepandwa kwenye msitu wa Kijabe ambao unategemewa na vyanzo vya maji nchini humo kwa asilimia 75.

Miti mingine 500,000 imepandwa Madagascar kwenye milima ya Kianjavato na fukwe za bahari za nchi hiyo.

Zaidi, miti 450,000 imepandwa Msumbiji huku mingi ikiwa ni mikoko ili kuokoa jamii za pwani za nchi hiyo.

Kwa mujibu wa tovuti ya Shirika la Arborday linaloshirikiana na Teamtrees kwenye mradi huo, shughuli hizo za upandaji wa miti zitakua endelevu na zimewapatia baadhi wakazi wa nchi husika ajira za muda mfupi na za muda mrefu.


Zinazohusiana


Katika bara la Asia, wadau hao wamepanda miti milioni 1.3 Ulaya (250,000) na Amerika imepandwa miti milioni 2.5.

Azimio la timu hiyo inayolenga kupunguza athari za mazingira na kulinda viumbe hai vilivyopo hatarini kutoweka ni kumaliza upandaji wa miti hiyo mwishoni mwa mwaka huu.

Kampeni hiyo iliyoanza mwishoni mwa mwaka jana, ni kati ya kampeni zilizoshirikisha watu wengi akiwemo Mkurugenzi wa kampuni ya Shopify ya Canada ambaye amechangia pesa ya kupanda miti milioni moja huku Mkurugenzi wa kampuni ya teknolojia ya SpaceX Elon Musk akichangia upandaji wa miti milioni 1.

Licha ya kuwa kipindi cha makusanyo kimepita, Mr Beast na timu yake bado wanapokea michango huku hadi sasa wakiwa na Sh51.8 bilioni zinazotarajiwa kupanda miti zaidi ya milioni 22.2.