November 24, 2024

Kasi ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania yashuka-Ripoti

Imepungua hadi asilimia 6.6 katika robo ya kwanza ya mwaka 2019 kutoka asilimia 7.5 kipindi kama hicho mwaka 2018 kutokana na kupungua kwa shughuli za afya, ujenzi, elimu, habari na mawasiliano.

  • Imepungua hadi asilimia 6.6 katika robo ya kwanza ya mwaka 2019  kutoka  asilimia 7.5 kipindi kama hicho mwaka 2018.
  • Imesababishwa na kupungua kwa shughuli za afya, ujenzi, elimu, habari na mawasiliano. 
  • Sekta za madini, fedha na bima ukuaji wake umeongezeka. 

Dar es Salaam. Kasi ya ukuaji wa  pato halisi la Taifa (GDP) imeshuka hadi asilimia 6.6 katika robo ya kwanza ya mwaka 2019  kutoka  asilimia 7.5 kipindi kama hicho mwaka 2018 kulikochangiwa na kupungua kwa shughuli za ujenzi, elimu, afya, habari na mawasiliano. 

Ripoti ya robo ya kwanza ya mwaka 2019 ya ukuaji wa pato la ndani (Quarterly Gross Domestic Product (QGDP)) iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inaeleza kuwa shughuli za afya ndiyo zilianguka kwa kasi zaidi hadi asilimia hasi 2.1 (-2.1%) kutoka asilimia 17.4 katika kipindi kama hicho mwaka jana. 

Kushuka kwa ukuaji wa sekta ya afya kumesababishwa na kupungua kwa wagonjwa wanaotibiwa katika hospitali zinazomilikiwa na watu binafsi. 

“Kiwango hicho cha ukuaji kilisababishwa na kushuka kwa idadi ya wagonjwa wanaotibiwa katika vituo vya afya vya binafsi kutoka wagonjwa 2,617,837 (milioni 2.6) mwaka 2018 hadi 2,390,253 (milioni 2.4) mwaka 2019,” inaeleza sehemu ya ripoti hiyo. 

Serikali imeendelea kujenga vituo vya afya umma katika maeneo mbalimbali nchini ili kuhakikisha kila kijiji kinakua na zahanati yake kama inavyoelekeza sera ya afya. 

Huenda juhudi hizo zimechangia wananchi wengi kwenda katika vituo vya afya vya umma ili kupunguza gharama za matibabu. 

Sekta nyingine zilizochangia kuporomoka kwa kasi ya ukuaji wa uchumi ni pamoja ujenzi; sanaa, burudani na muziki; elimu; habari na mawasiliano. 

Wakati kasi ya ukuaji wa uchumi ikishuka, sekta ya ujenzi, madini usafirishaji na uhifadhi wa bidhaa ndiyo zimetoa mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi mwaka 2019. 

Kwa sasa Serikali inaendelea na ujenzi wa reli ya kisasa (Standard Gauge Railway line (SGR)) kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro itakayogharimu Sh2.7 trilioni ikiwa ni sehemu ya mradi wa kilomita 1,219 hadi Mwanza.

Sambamba SGR tayari imezindua reli ya Kaskazini mwa Tanzania na ikiunganisha mikoa ya Kilimanjaro, Tanga na Jiji la Dar es Salaam ambalo lina bandari inayopokea mizigo mbalimbali kutoka nje ya nchi. 


Soma zaidi:


Pia uboreshaji wa usafiri kwa upanuzi wa bandari na ujenzi wa madaraja mbalimbali ikiwemo la juu katika makutano ya Barabara ya Morogoro na Sam Nujoma/Mandela katika eneo la Ubungo jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, baadhi ya sekta za  na sekta za madini; fedha na bima; biashara ya nyumba; taaluma, sayansi na ufundi; na utawala zimefanya vizuri baada kuonyesha ukuaji mzuri ikilinganishwa na mwaka jana. 

Ukuaji wa shughuli za nyumbani zinazojumuisha ajira za wafanyakazi wa ndani umebaki katika kiwango kile kile cha asilimia 3.1 kilichorekodiwa katika robo ya kwanza ya mwaka 2018.