November 24, 2024

Kicheko kwa wafanyabiashara wanaopata TIN kwa mara ya kwanza

Serikali inapendekeza kutoa unafuu wa kutolipa kodi kwa kipindi cha miezi sita kuanzia wakati mfanyabiashara au mwekezaji anapopewa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN).

  • Serikali inapendekeza kutoa unafuu wa kutolipa kodi kwa kipindi cha miezi sita kuanzia wakati mfanyabiashara au mwekezaji anapopewa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN).
  • Itaondoa usumbufu au dhana ya woga wakati wa kuanzisha biashara.

Dar es Salaam. Kama unakusudia kuanzisha biashara katika siku za hivi karibuni na umekuwa ukihofia kuanza kukatwa kodi wakati biashara yako ikiwa changa, sasa una kila sababu ya kutabasamu, baada ya Serikali kutoa ahueni ya kodi. 

Serikali imetangaza kusudio la kutoa nafuu ya kutolipa kodi kwa kipindi cha miezi sita kuanzia wakati mfanyabiashara au mwekezaji anapopewa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN). 

Akizungumza jana bungeni wakati akiwasilisha bajeti ya Serikali Kuu kwa mwaka 2019/2020,  Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amesema hatua hii inatofautiana na hali ilivyo sasa ambapo mfanyabiashara anapopewa TIN anaanza kufanyiwa tathmini (tax assessment) ya mapato yake ya biashara na kutakiwa kulipa kodi. 

“Hatua hii itawezesha wafanyabiashara na wawekezaji wapya kupata muda wa kujiandaa na mahitaji yanayotakiwa katika shughuli wanazofanya na kuondoa usumbufu au dhana ya woga wakati wa kuanzisha biashara,” amesema Waziri Mpango. 

Amesema katika kipindi hicho mfanyabiashara anakuwa anashughulikia  mahitaji ya Leseni ya biashara na vibali vingine muhimu vya biashara, jambo litakamsaidia kujipanga kabla hajaanza kulipa kodi.