Kifo cha Magufuli chaahirisha sherehe za Muungano wa Tanzania
Makamu wa Rais Dk Philip Mpango amesema Serikali iliamua kutokufanya sherehe za Muungano wa Tanzania mwaka huu kutokana na tukio la hivi karibuni la kifo cha Hayati Rais John Magufuli.
- Serikali imesema haijafanya sherehe za Muungano mwaka huu kutokana na kifo cha Hayati John Magufuli.
- Muungano wa mwaka huu unaadhimishwa kwa kongamano maalum jijini Dodoma.
- Fedha za sherehe hizo kugawanywa Tanzania Bara na Zanzibar.
Dar es Salaam. Makamu wa Rais Dk Philip Mpango amesema Serikali iliamua kutokufanya sherehe za Muungano wa Tanzania mwaka huu kutokana na tukio la hivi karibuni la kifo cha Hayati Rais John Magufuli.
Hayati Dk Magufuli alifariki dunia Machi 17 mwaka huu kwa maradhi ya moyo ambapo nafasi yake imechukuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Badala yake sherehe hizo za kuadhimisha miaka 57 ya muungano zinaadhimishwa kwa kongamano maalum linalowakutanisha wasomi na Watanzania katika ukumbi wa Chimwaga jijini Dodoma.
Dk Mpango aliyekuwa akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo leo Aprili 26, 2021 amesema imekuwa ni utamaduni wetu kuadhimisha sherehe za muungano kitaifa kwa gwaride maalum na burudani katika kiwanja mahususi lakini mwaka huu ni tofauti.
“Lakini kwa mwaka huu kutokana na tukio la hivi karibuni ambapo nchi yetu iliondokewa na mmoja wa mashujaa wetu Hayati John Magufuli aliyekua kiongozi mkuu wa Taifa letu, tuliamua badala ya sherehe tuadhimishe kwa kongamano hili,” amesema Dk Mpango.
Soma zaidi:
-
Miaka 55 ya Muungano wa Tanzania inaadhimishwa kwa aina yake
-
Rais Magufuli afuta sherehe za Uhuru kwa mara ya pili
Amesema fedha zilizotengwa kwa sherehe hizo zitagawanywa pande zote mbili za muungano yaani Tanzania Bara na Zanzibar na kila mmoja ataamua matumizi yake.
Aidha, Makamu wa Rais amewataka Watanzania kuendelea kuuenzi muungano kwa kudumisha umoja wa kitaifa, ulinzi na usalama.
Amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia imelifanya suala la muungano kama moja ya vipaumbele vyake na itaulinda na kuuendeleza kwa vizazi vijavyo.
“Watakaojaribu kuchezea muungano, hapo mimi sitakuwa mpole,” amesema Dk Mpango katika hutuba yake.
Muungano wa Tanzania ni matokeo ya kuungana kwa nchi mbili za Tanganyika na Zanzibar Aprili 26, 1964. Waliosisi ni Rais wa kwanza wa Tanzania Hayati Julius Nyerere na Sheikh Abeid Karume, aliyekuwa Rais wa kwanza wa Zanzibar.