October 6, 2024

Kigogo TPA aliyesimamishwa kazi na Rais Samia mikononi mwa Takukuru

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Deusdedit Kakoko aliyesimamishwa kazi wiki iliyopita ili kupisha uchunguzi wa ubadhirifu dhidi ya taasisi hiyo, sasa anashikiliwa na kuhojiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takuku

  • Takukuru yasema hajatoroka bali wanamshikilia kwa mahojiano na uchunguzi. 
  • Alisimamishwa kazi na Rais Samia Suluhu Hassan Machi 28 baada ya kubainika uwepo wa ubadhirifu wa Sh3.6 bilioni bandarini.

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Deusdedit Kakoko aliyesimamishwa kazi wiki iliyopita ili kupisha uchunguzi wa ubadhirifu dhidi ya taasisi hiyo, sasa anashikiliwa na kuhojiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru). 

Takukuru imesema bosi huyo wa TPA hajatoroka kama inavyodaiwa na baadhi ya watu mtandaoni  bali inamshikilia kwa uchunguzi. 

Rais Samia Suluhu Hassan alimsimamisha kazi Kakoko Machi 28 mwaka huu baada ya kubainika uwepo wa ubadhirifu wa Sh3.6 bilioni bandarini. 

“Wakati Waziri Mkuu amefanya ukaguzi waliosimamishwa ni hawa wa chini huku naomba mara moja nitoe agizo la kumsimamisha mkurugenzi mkuu wa bandari. Halafu uchunguzi uendelee,” aliagiza Rais Samia wakati akipokea ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa mwaka 2019/20 Ikulu jijini Dodoma. 


Soma zaidi:


Hata hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Brigedia Generali John Mbungo amejitokeza na kusema hajatoroka bali wanamshikilia bosi huyo wa TPA kwa ajili ya uchunguzi. 

“Kumshikilia mtu ni suala la kawaida kama kuna tatizo limetokea na kama mlivyomsikia Mheshimiwa Rais amemsimamisha kazi kwa sababu ya matatizo na sisi ni kweli tunamshikilia ili tuweze kufanya uchunguzi vizuri”- Brigedia Jenerali Mbungo wakati akihojiwa na kituo cha televisheni cha ITV leo Machi 30,2021. 

Hata hivyo, Mkurugenzi mkuu huyo wa Takukuru amesema kwa sasa hawezi kusema kuhusu sababu za kumshikilia bosi huyo lakini ni utaratibu wa uchunguzi. 

Kakoko, ambaye alithibitishwa kuwa bosi wa TPA mwaka 2018 baada ya kuwa kaimu wa taasisi hiyo, anakuwa kiongozi wa awali kabisa kusimamishwa kazi na Rais Samia ambaye alitwaa madaraka Machi 19 mwaka huu baada ya kufariki kwa aliyekuwa Rais wa Tanzania Dk John Magufuli.