October 6, 2024

Kilio kwa wawekezaji wa Acacia soko la hisa Dar

Wawekezaji wa kampuni hiyo ya madini leo wamepoteza Sh50 kwa kila hisa kutoka bei ya jana.

  • Wawekezaji wa kampuni hiyo ya madini leo wamepoteza Sh50 kwa kila hisa kutoka bei ya jana.
  • Wenzao wa kampuni hodhi ya Jubilee (JHL) ni miongoni mwa waliopoteza leo.
  • Wawekezaji wa benki ya KCB na kampuni ya habari ya NMG wao watalala na tabasamu.

Dar es Salaam. Wawekezaji wa kampuni ya Acacia (ACA) katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) leo watalala na maumivu baada ya thamani ya hisa za kampuni hiyo kushuka kwa asilimia 1.10 na kuwafanya wapoteze Sh50 kwa kila hisa moja kutoka kiwango cha jana Mei 21, 2019.

Ripoti ya soko ya siku ya DSE ya Mei 22 inaonyesha kuwa hadi soko linafungwa thamani ya hisa moja ya Acacia ilikuwa ni Sh4,480 kutoka Sh4,530 iliyorekodiwa jana.

Wakati wawekezaji wa Acacia wakiugulia maumivu leo, wenzao wa benki ya KCB watalala na kicheko baada ya thamani ya hisa za benki hiyo kupanda kutoka Sh825 kwa hisa moja iliyorekodiwa jana wakati soko linafungwa hadi Sh870 leo hii jioni. 

Kampuni nyingine ambayo thamani ya hisa zake imeongezeka ni kampuni ya Habari ya NMG (National Media Group) ambayo imepanda kwa asilimia 2.08.  


Zinazohusiana: 


Hata hivyo, kampuni hodhi ya Jubilee (JHL) imeungana na Acacia katika maumivu leo baada ya thamani ya hisa zake kushuka kwa asilimia 0.54 huku kampuni ya uwekezaji ya NICO ikiongoza kwa  kuuza kiwango kikubwa cha hisa sokoni leo.

Acacia ndiyo kampuni iliyofanya vibaya zaidi leo sokoni huku nyingi zikibaki katika viwango vilivyokuwepo jana zikiwemo Vodacom, na benki ya CRDB, DCB na NMB.