July 8, 2024

Kiswahili kinavyotumika kukuza utalii Marekani

Ni katika mnara wa mawe wa Georgia Guidestones ambao umeandikwa kwa lugha nane maarufu duniani ikiwemo lugha ya Kiswahili.

  • Kimetumika katika kutoa maelezo yaliyoandikwa katika mnara wa mawe wa Georgia Guide stiones.
  • Kiswahili ni kati ya lugha nane zilizotumika katika kutoa maelezo yanayotoa muongozo wa jinsi maisha yanayotakiwa. 
  • Mnara huo ni nguzo muhimu ya utalii Marekani.

Dar es Salaam. Endapo umewahi kufika Marekani, hasa katika jimbo la Georgia, na haufahamu lolote kuhusu mnara wa Georgia Guide Stones, basi unahitaji kufahamu zaidi maana una taarifa muhimu kuhusu lugha ya Kiswahili.

Mnara huo ambao umejengwa kwa mawe umeenda juu kwa mita kadhaa, umekuwa kiungo muhimu cha shughuli za utalii wa historia katika jimbo hilo. 

Kwa waliowahi kutembelea, ni lazima watakua wamekutana na maandishi yaliyoandikwa kwa lugha nane tofauti na kubandikwa kwenye mnara huo. 

Moja ya lugha hiyo ni Kiswahili ambacho chimbuko lake ni ukanda wa Afrika Mashariki hasa Tanzania. 

Maandishi hayo ambayo yako katika mfumo wa amri 10, yanatoa maelekezo na maonyo ya watu kutunza amani, kuheshimiana hata baada ya vita baridi kati ya Marekani na Urusi. 

Lugha nyingine ambazo zimepata fursa ya kufikisha ujumbe huo ni Kiingereza, Kichina, Kiarabu, Kiebrania, Kihindi, Kirusi na Kihispania.

Matumizi ya Kiswahili katika mnara huo japokuwa kinachangamoto ya tafsiri, yanadhihirisha wazi kuwa lugha hiyo imeendelea kuwa nguzo muhimu ya mawasiliano duniani. 

Kiswahili ambacho ni lugha ya Taifa ya Tanzania, kimekua ni kiungo muhimu cha shughuli za biashara, utalii na mawasiliano ya watu mbalimbali ambao wamekuwa wakitaka kujifunza utamaduni wa nchi hiyo. 

Kwa sasa Kiswahili ni miongoni mwa lugha nne zinazotumiwa katika shughuli  Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC). Lugha zingine ni Kifaransa, Kiengereza na Kireno. 


Soma zaidi


Historia ya mnara wa Georgia Guidestones

Vyanzo mbalimbali likiwemo shirika la habari la CNN, vinaeleza kuwa mnara huo umejengwa kwa mawe makubwa ya vipande aina ya granaiti (granite) yaliyo na urefu wa futi 20 kuelekea juu miaka 40 iliyopita.

Mnara huo uliojengwa kwa udhamini wa mtu aliyejulikana kwa jina “R.C. Christian” baada ya kukataa kutaja jina lake halisi. 

Mnara huo una vipande vikubwa vitano huku vinne vikiwa na uzito wa tani 20 vikiwa vimesimamishwa na kingine kikiwa juu chenye uzito wa kilogramu 11,300. 

                       

Upekee wa mnara wa Georgia ni ustadi uliotumika kujenga ambao unatoa fursa ya kujionea maajabu ya kiastronomia (astronomy).

Maajabu hayo ni pamoja na kuiona nyota ya kaskazini ijulikanayo kama Polaris, mwale wa jua ifikapo mchana na eneo la kati la mnara huo linaonyesha mabadiliko ya jua kadri misimu ya mwaka inavyobadilika.

CNN inaeleza kuwa, astronomia iliyowekwa ingeweza kusaidia vizazi kutambua mwelekeo (compass), muda na tarehe.

Programu za habari za sauti (podcast) ikiwemo podcast ya “Supernaturals” inaelezea kuwa, mawe hayo yalijengwa ikiwa ni mnara wa kukumbusha vizazi ambavyo vingenusurika na vita ili kuendelea kuweka uwiano katika dunia.