November 24, 2024

Kitabu cha kuwaelimisha watoto kuhusu Corona chaingia mtaani

Kitabu hicho kipya kitasaidia watoto kuelewa na kufahamu kwa kina ugonjwa wa virusi vya Corona (COVID-19) kitakachowasaidia kujikinga na janga hilo la dunia.

  • Kimezinduliwa na zaidi ya mashirika 50 ya kibinadamu yakiwemo yale ya Umoja wa Mataifa  (UN).
  • Kitabu hicho kimepewa jina la “Shujaa wangu ni Wewe, Jinsi gani watoto wanaweza kupambana na COVID-19”
  • Kinaeleza ni kwa vipi watoto wanaweza kujilinda wenyewe, familia zao na marafiki dhidi ya virusi vya Corona.

Dar es Salaam. Zaidi ya mashirika 50 ya kibinadamu yakiwemo yale ya Umoja wa Mataifa  (UN) yameandaa kitabu kipya cha kusaidia watoto kuelewa na kufahamu kwa kina ugonjwa wa virusi vya Corona (COVID-19) kitakachowasaidia kujikinga na janga hilo la dunia. 

Mashirika ya UN yaliyoandaa kitabu hicho ni pamoja na lile la afya (WHO), la kuhudumia watoto (UNICEF), la kuhudumia wakimbizi (UNHCR) na lile la elimu, sayansi na utamaduni (UNESCO) na wadau wengine wakiwemo Save the Children na shirikisho la vyama vya msalaba mwekundu na hilal nyekundu.

Kitabu hicho chenye kikaragosi cha kufikirika, kimepewa jina la “Shujaa wangu ni Wewe, Jinsi gani watoto wanaweza kupambana na COVID-19” kinaeleza ni kwa vipi watoto wanaweza kujilinda wenyewe, familia zao na marafiki dhidi ya virusi vya Corona.

Kitabu hicho pia kinawasaidia namna wanavyoweza kukabili hisia pindi wanapokumbana na hali halisi inayobadilika haraka na mara kwa mara.

Kwa mujibu wa UN walengwa ni watoto wenye umri wa kuanzia miaka sita hadi 11 na ni mradi wa kamati ya mashirika mbalimbali kuhusu afya ya akili na usaidizi wa kisaikolojia katika mazingira ya dharura.


Zinazohusiana:


Mwanzoni mwa maandalizi ya kitabu hicho, zaidi ya watu 17,000 wakiwemo watoto, wazazi, walezi na walimu kutoka kona mbalimbali duniani walielezea jinsi gani wanakabiliana na janga la COVID-19.

UN imeeleza kuwa miichango  yao ilikuwa muhimu kwa mwandishi wa kitabu na mchoraji Helen Patuck na timu nzima katika kuhakikisha simulizi na ujumbe vinaendana na watoto wa hali tofauti na maeneo mbalimbali duniani.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Henrietta Fore, amesema kuwa duniani kote, maisha ya watoto yamebadilika, wengi wao wako katika nchi zenye karantini na hivyo, “kitabu hiki kitasaidia watoto kuelewa na kukabiliana na hali ya sasa na kujifunza ni kwa vipi wanaweza kuchukua hatua ndogo tu na kuwa mashujaa katika simulizi zao.”

Ili kuhakikisha kitabu hicho kinawafikia watoto wengi kadri iwezekanavyo, kitatafsiriwa kwa lugha nyingi, ambapo mpaka sasa kitabu hicho kimetafsiriwa kwa lugha sita huku nyingine 30 zikiwa kwenye maandalizi. 

Kitabu kinaweza kusomwa kwa maandishi kwenye mtandao na pia kusikilizwa kwa sauti kwenye intaneti.