Kitendawili cha maabara shule za sekondari Mbeya
Takwimu zinaonyesha kuwa Halmshauri ya Wilaya ya Mbarali haina uhaba wa maabara lakini baadhi ya shule zake zafeli vibaya masomo ya Sayansi.
- Halmashauri ya Jiji la Mbeya ina upungufu wa vyumba 23 vya mabaara, ukiwa ni mkubwa ukilinganisha na halmashauri nyingine.
- Wadau wataka uwekezaji wa miundombinu muhimu uendane na uwepo wa walimu.
Dar es Salaam. Licha ya kuwa kitovu cha mkoa, Halmashauri ya Jiji la Mbeya inakabiliwa na upungufu mkubwa wa maabara katika shule za sekondari ukilinganisha na halmashuri nyingine katika mkoa wa Mbeya.
Uchambuzi wa takwimu za msingi za elimu (Best) mwaka 2016 unabainisha kuwa halmashauri hiyo ilikuwa inahitaji maabara 23 kutimiza mahitaji huku maabara za fizikia zikihitajika zaidi. Halmashauri ya jiji hilo la Mbeya ina upungufu wa maabara ya masomo ya Fizikia 11, Bailojia saba na Kemia maabara tano.
Hata wakati Jiji la Mbeya likiwa na uhaba huo, halmashauri ya Mbarali iliyopo zaidi ya kilomita 120 kutoka makao makuu ya mkoa, haina uhaba wowote wa maabara katika shule zake za sekondari za umma kwa mujibu wa takwimu hizo. Mbarali ina mahitaji ya vyumba vya maabara 48 na vyote vilikuwepo mwaka huo.
Tofauti na Halmashauri ya jiji la Mbeya, Kyela wao wana upungufu wa wastani. Halmahsuari hiyo ina upungufu wa maabara tatu za somo la Bailojia, Fizikia (mbili) wakati somo la Kemia likiwa na upungufu wa chumba kimoja.
Wanafunzi wa sekondari ya Wiza wakiwa katika maabara. Picha| Mtandao.
Kuna uhusiano wa uwepo wa maabara na kufaulu Sayansi?
Pamoja na uhaba wa maabara, uchunguzi mdogo wa Nukta umebaini bado shule nyingi zilizopo katika halmashauri ya jiji zinafanya vizuri kidogo katika masomo ya Sayansi ukilinganisha na zile za halmashauri za Mbarali. Mathalani katika katika mtihani wa kidato cha nne mwaka 2017 Shule ya Sekondari ya Uyole wanafunzi 56 kati ya 76 walifanya vizuri katika somo la Kemia, 145 kati 242 walifanya vizuri katika somo la Bailojia. Somo la Fizikia wanafunzi waliofanya mtihani walikuwa 76 walifanya vizuri wakiwa 46 tu.
Hali ni tofauti Mbarali ambako baadhi ya shule zake za sekondari zilizofanyiwa tathmini zinaonyesha hali ni tete. Mfano, Shule ya Sekondari ya Igava ilikuwa shule ya 51 katika ya shule 55 za mkoa wa Mbeya kwa shule zilizo na wanafunzi chini ya 30 katika matokeo ya kidato cha nne mwaka 2017 licha ya kuwa miongoni mwa zile zinazobainishwa kuwa zina vyumba vyote vya maabara.
Katika matokeo hayo, wanafunzi 26 kati ya 27 waliofanya mtihani wa somo la Fizikia walivuna walifeli huku mwanafunzi mmoja akipata alama D. Ni wanafunzi wanne tu kati ya 27 walipata alama D na waliosailia wote walifeli soma la Kemia. Angalu katika somo la Bailojia kuna ahueni baada wanafunzi tisa kupata alama D na watatu alama C kati ya 25 waliofanya mtihani wa somo hilo.
Ufaulu wa Sayansi ni zaidi ya maabara
Mkazi wa Dar es Salaam aliyesoma katika Shule ya Sekondari ya Samora Machel iliyopo mkoani Mbeya, Roida Mwakamele anasema shule kuwa na vitendea kazi pekee yake kama maabara haitoshi bila kuwa na mtu atakayeongeza ufanisi kwa kutumia vifaa au miundombinu hiyo.
”Labda kati ya shule hizo mojawapo ina walimu wawili au watatu ambao utakuta wanajukumu la kufundisha kuanzia kidato cha kwanza mpaka cha nne. Unafikiri huyo mwalimu ataweza kuwafundisha wanafunzi hao kwa umakini?Haiwezekani,” anasema Mwakamele ambaye ni mwanafunzi anayemalizia masomo ya Shahada ya kwanza ya sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Mwakamele anasema kuwa ili kuongeza ufaulu wa masomo ya sayansi kuna haja ya Serikali kuangalia upya uhitaji wa walimu wa masomo hayo na kuwaajiri wengi zaidi badala ya ahadi tu kwa kuangalia uwiano wa mahitaji katika mosomo yote ya hesabu, fizikia, kemia na bailojia.
Shule gani inafanya vizuri katika masomo ya sayansi mkoani Mbeya? Usikose kupitia Elimu Yangu.
Mbinu zinazoweza kuisaidia Temeke kutokomeza sifuri elimu ya sekondari
Walimu wanajua zaidi kinachofelisha wanafunzi wengi masomo ya sayansi. Mwalimu wa Shule ya Sekondari ya Nyamisati, Deogratius Luoga anasema mbali na uhaba wa walimu kuna wakati wanafunzi nao hukosa bidii ya kutosha katika masomo yao jambo linalofanya wafanye vibaya katika masomo ya sayansi ambayo huihitaji umakini mkubwa.
”Hapa tusiangalie mwalimu pekee yake. Tuwatazame na wanafunzi nao wanaweka bidii gani katika kujifunza kwa kuwa shule inaweza ikawa na kila kitu kuanzia walimu mpaka vitendea kazi lakini wanafunzi wasiwe na juhudi ya kutosha. Tuhimize wanafunzi kujisomea kwa makini,” anasema Mwalimu Luoga.
Hali ilikuwa mbaya kuliko sasa
Afisa elimu wa mkoa wa Mbeya, Paulina Mbigeza ameiambia Nukta kuwa kabla ya uwepo wa maabara za masomo ya Sayansi hali ilikuwa mbaya zaidi ukilinganisha na sasa.
“Serikali imefanya jitihada kubwa katika kuboresha masomo ya Sayansi hasa katika mkoa wa Mbeya ndio maana hata ukiangalia ufaulu wa mkoa wa Mbeya umeongezeka.
“Kwa matokeo ya kiujumla mkoa wa Mbeya umefanya vizuri sana umekuwa na wastani wa asilimia 81.7 pia imeshika nafasi ya sita kati ya 25 mikoa ya Tanzania bara lakini kuna changamoto ya shule moja moja katika mkoa wetu na hii ni kwa karibia mikoa yote shule zote haziwezi kufanana,’’ anasema Mbigeza.
Ili kutatua changamoto hizo, anasema wameweka mkakati maalumu kwa ajili ya kuziinua shule hizo katika kuhakikisha zinafanya vizuri katika masomo ya Sayansi na wanafunzi wanaelimika vizuri zaidi na kuufanya mkoa kuondokana na hali ya ufaulu duni iliyopo kwa sasa.
Anasema wanakaribisha wadau wa elimu waende kubadilishana mawazo na uzoefu ili kufanya mkoa wa Mbeya kuwa na matokeo mazuri zaidi.
Takwimu za Serikali katika bajeti ya Ofisi ya Rais- Tamisemi mwaka 2018/19 zinaonyesha kuwa hadi sasa kuna walimu wa shule za sekondari 88,865 huku walimu wa masomo ya sanaa wakiwa 69,395 idadi ambayo ni mara tatu zaidi ya wale wa sayansi.
Mahitaji ya walimu wa sanaa kwa mujibu wa Tamisemi ni walimu 48,245 hivyo kuwa na ziada ya walimu 20,712. Hata hivyo, walimu wa masomo ya sayansi wanaohitajika ni 35,136 wakati waliopo ni 19,459 tu ikiwa ni nusu tu ya mahitaji.