November 24, 2024

Kliniki kuwanufaisha wafanyabiashara maonyesho ya Saba Saba 2019

TanTrade imeeleza kuwa wakati wa maonyesho hayo wafanyabiashara wenye mambo yanayowasumbua kuhusu vibali, masoko, mitaji na usajili wa biashara watapatiwa suluhu.

  • TanTrade imeeleza kuwa wakati wa maonyesho hayo wafanyabiashara wenye mambo yanayowasumbua kuhusu vibali, masoko, mitaji na usajili wa biashara watapatiwa suluhu.
  • Wataalamu kutoka serikalini na sekta binafsi watakuwepo kutoa huduma hizo kwa wafanyabiashara.

Dar es Salaam. Wafanyabiashara wenye changamoto mbalimbali za kibiashara huenda wakapata ahueni kwa baadhi mambo yanayowasumbua baada ya Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) kutangaza kuanzishwa kwa huduma ya kliniki ya biashara wakati wa maonyesho ya biashara ya kimataifa ya Dar es Salaam maarufu kama Saba Saba.

Taarifa ya Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) ya Juni 11, 2019 inaeleza kuwa kliniki hiyo, itakayotolewa katika Uwanja wa Maenesho wa Mwalimu Nyerere (Saba Saba) Barabara ya Kilwa, itaanza kuwahudumia wafanyabiashara kuanzia Juni 29 hadi Julai 12 mwaka huu.

“Lengo la Kliniki hii ni kutatua changamoto mbalimbali zinazowakumba wafanyabiashara kama vile taratibu za usajili wa biashara, leseni, viwango, vibali mbalimbali, taratibu za ulipaji kodi, usajili wa namba ya kulipa kodi, upatikanaji wa mitaji na masoko ndani na nje ya nchi,” imeeleza TanTrade katika taarifa hiyo kuelekea maonyesho ya 43 ya Sabasaba.

Kliniki hiyo, kwa mujibu wa TanTrade itakuwa na wataalamu mbalimbali kutoka taasisi za umma na sekta binafsi zinashughulika na uwezeshaji wa biashara nchini.


Soma zaidi: Rais Magufuli awafuta kazi Tizeba, Mwijage joto la korosho likipanda


Kwa muda mrefu wafanyabiashara nchini wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali za masoko na uendeshaji wa biashara nyingi zikichagizwa na urasimu katika baadhi ya taasisi za Serikali nchini yakiwemo madai ya rushwa, ucheleweshwaji wa vibali na makadirio makubwa ya kodi ambayo hayaendani na biashara husika.

Mwishoni mwa wiki iliyopita Rais John Magufuli alikutana na wafanyabiashara Ikulu jijini Dar es Salaam kujadili namna ya kutatua changamoto hizo ili kuchagiza ukuaji wa uchumi nchini.

Siku moja ya mkutano huo alimfuta kazi Waziri wa Viwanda na Biashara Joseph Kakunda na kumteua Innocent Bashungwa kusukuma jahazi la wizara hiyo ambayo tayari imeshaongozwa na mawaziri watatu tangu Rais Magufuli aingie madarakani Novemba 2015.

Mbali na kufanya mabadiliko madogo katika baraza la mawaziri, Dk Magufuli alimng’oa Charles Kichere katika nafasi ya Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya MapatoTanzania (TRA) na kumteua Edwin Mhede ikiwa ni moja ya jitihada za kuongeza mapato na kukabiliana na malalamiko kutoka kwa wateja.