July 5, 2024

Kozi zitakazopewa kipaumbele mikopo elimu ya juu mwaka 2020-21

Kozi zitakazopewa kipaumbele zaidi ni pamoja na ualimu wa sayansi, programu za uhandisi na sayansi ya afya.

  • Kozi zitakazopewa kipaumbele zaidi ni pamoja na ualimu wa sayansi, programu za uhandisi na sayansi ya afya.
  • Watakaosomea sayansi za msingi na sayansi ya ardhi nao hawataachwa nyuma.
  • Shahada zingine zote ambazo hazikutajwa kwenye kundi la kwanza, la pili au la tatu zitajumuishwa katika kundi la tatu.

Dar es Salaam. Wakati Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) ikitarajia kufungua dirisha la maombi ya mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu wiki ijayo, imetangaza makundi matatu ya kozi zitakazopewa kipaumbele katika utoaji wa mikopo hiyo  ikiwemo programu za uhandisi na ualimu wa sayansi.

HESLB katika taarifa yake iliyotolewa Julai 17, 2020 imeeleza kuwa mfumo wa uombaji wa mkopo kwa njia ya mtandao utakuwa wazi kwa siku 40 kuanzia Jumanne, Julai 21, 2020 hadi Jumatatu, Agosti 31, 2020.

“Tunawashauri wanafunzi wahitaji kutumia muda wa sasa hadi mfumo utakapofunguliwa (Julai 16, 2020 hadi Julai 21, 2020) kusoma ‘Mwongozo wa Utoaji Mikopo kwa Mwaka 2020/2021’ unaopatikana kuanzia sasa katika tovuti ya HESLB katika lugha za Kiswahili na Kiingereza,” imeeleza taarifa hiyo.

Mwongozo huo unatoa maelekezo ya kina kuhusu sifa, utaratibu na vigezo vitakavyotumika katika uchambuzi wa upangaji mikopo kwa mwaka wa masomo 2020/21.

Waombaji wote waliodahiliwa kusoma shahada mbalimbali kwa mwaka wa masomo 2020/2021 wanapaswa wawe wamehitimu kidato cha sita au stashahada au sifa nyingine linganishi katika kipindi cha miaka mitano yaani kati ya 2016 na 2020.


Zinazohusiana: 


Kozi zitakazopewa kipaumbele

Katika mwongozo huo, kundi la kwanza la wanafunzi ambao watapewa kipaumbele linajumuisha kozi za ualimu sayansi (Fizikia, Kemia na Baiolojia), ualimu wa hisabati na masomo ya biashara na shahada ya uzamili katika uhandisi wa ndege na matengenezo. 

Pia kozi za sayansi za afya ikiwemo udaktari, upasuaji meno, madawa ya mifugo, ufamasia, uuguzi na ukunga; programu za uhandisi; jiolojia ya petroli na kemia ya petroli; kilimo, misitu, sayansi ya wanyama na usimamizi wa uzalishaji yatapewa kipaumbele. 

Kundi la pili la wanafunzi ambao watanufaika na mikopo hiyo ni  wale ambao kozi zao zitajikita katika programu za msingi za sayansi ambazo zinajumuisha shahada ya sayansi kwa ujumla katika wanyama, mimea, kemia, fizikia, baiolojia, baiolojia ya viumbe vidogo, baiolojia ya mifugo na baioteknolojia, uvuvi na mifugo. 

“Programu ya Sayansi ya Ardhi (Ubunifu Majengo, Ubunifu Mandhari nje ya Majengo, Usanifu ndani ya Majengo, Uchumi Ujenzi, Mipango Miji na Vijiji, Usimamizi na Uthaminishi Ardhi, Jiospasho, Teknolojia katika Usanifu),” inasomeka sehemu ya mwongozo huo ikielezea kozi la kundi la pili. 

Katika kundi la tatu na la mwisho ni la wanafunzi wanaokusudia kusoma kozi za biashara na uongozi, sayansi za jamii, sanaa, sheria, lugha, fasihi na masomo ya uandishi wa habari na mawasiliano. 

“Programu nyingine zote ambazo hazijaorodheshwa katika kundi lolote kati ya hayo matatu, zitaangukia katika kundi la tatu,” unaeleza mwongozo huo.