November 24, 2024

Kuishi karibu na minara ya simu kunasababisha kansa?

Mpaka sasa hakuna ushahidi wa moja kwa moja ambao umetolewa kuhuhu minara hiyo kusababisha udhaifu huo mwilini.

  • Mpaka sasa hakuna ushahidi wa moja kwa moja ambao umetolewa kuhuhu minara hiyo kusababisha madhara ya kiafya.
  • Wataalam wanasema mionzi  inayotoka kwenye minara ya simu haina nguvu ya kupenya kwenye mwili ukilinganisha na mionzi ya jua na ‘X-ray’.

Ni dhahiri kuwa sekta ya mawasiliano inazidi kukua kila siku kunatokana na ongezeko la watu wanaotumia simu za mkononi katika shughuli mbalimbali za maendeleo. 

Utendaji wa simu hizo hutegemea upatikanaji wa mawimbi ya sauti yanayoongozwa na minara inayojengwa katika maeneo mbalimbali ili kuwa rahisishia watu mawasiliano.

Kwa mujibu wa utafiti wa minara ya simu wa kampuni ya Tower Exchange uliotolewa mwaka 2016, inakadiriwa kuwa Tanzania ina minara ya simu zaidi  8,800, huku kampuni za Helios Towers na  kampuni ya Mawasiliano ya Simu Tanzania (TTCL) zikitawala soko hilo nchini.

Lakini baadhi ya watu wamekuwa wakijenga hoja kuwa kuishi, kutembea au kusoma karibu na minara ya simu kunawaweka watu katika hatari ya kupata kansa au matatizo mengine ya afya. Dhana hiyo ina ukweli wowote?

Mpaka sasa hakuna ushahidi wa moja kwa moja kuhusu hoja hiyo. Katika nadharia za afya kuna sababu chache ambazo zinakubaliana kuwa minara ya simu kusababisha kansa. 

Chama cha Kansa cha Marekani (ACS) kimeeleza sababu mbalimbali za kwanini minara ya simu sio tishio kwa afya ya binadamu.

Nguvu ya mawimbi ya radio yanayotumiwa na minara ya simu ni ndogo ukilinganisha na mionzi mingine kama ya jua (ultraviolet light), Eksirei (x-rays) na nyuklia (gamma rays) ambayo inaongeza hatari ya kupata kansa kwa binadamu.

Mionzi ya mawimbi ya radio inayotolewa na minara ya simu haina nguvu ya kutosha kuvunja kemikali zilizoungana za vinasaba (DNA) vilivyopo mwilini.

Bado haijathibitishwa mpaka sasa kuwa minara ya simu inaweza kusababisha kansa licha ya tafiti kuendelea kufanyika kutafuta ukweli. Picha| New Age

Suala lingine ni urefu wa mawimbi (wavelength). Mawimbi ya radio yana urefu ambao unaweza kujikusanya kwa inchi moja au mbili na siyo zaidi ya hapo. Hii ina maana kuwa mionzi ya mawimbi ya radio haiwezi kujikusanya kwa ukamilifu kuhatarisha seli za mwili.

Hata kama mawimbi ya radio kwa sehemu yangekuwa yanaathiri seli za mwili yasingefanikiwa kwasababu kiwango cha mawimbi hayo kinachopatikana ardhini wanakoishi watu ni kidogo sana kuliko kile kinachopendekezwa na watalaamu wa mawasiliano.


Zinazohusiana:


Kiasi cha miozi inayopatikana kwa kuishi karibu na minara ni kidogo kuliko kile kinachopatikana kwenye simu za mkononi, jambo ambalo linaweza kumuweka mtu katika hatari ya kupata madhara katika ubongo wake ikiwa atatumia simu kwa muda mrefu.

Licha ya kuwa minara ya simu haiwezi kusababisha kansa, huenda ikawa na madhara mengine ya kiafya ambayo ni lazima yathibitishwe na daktari. 

Daktari Joachim Mabula kutoka mtandao wa Tiba Fasta, anasema kuna madhara ya kuishi karibu minara ya simu ila sio ya moja kwa moja kwa sababu huchukua muda kuonekana.

Anasema miali ya usumaku inayotolewa na mawimbi ya radio na mionzi ya jua inaweza kusababisha msongo wa mawazo na kuwaletea shida wanawake wajawazito. 

“Hapo zamani watafiti wamewahi kugundua kuwa miali ya usumaku inayotolewa na minara ya simu na nyaya za umeme mkubwa husababisha msongo (stress) kwenye mwili unaoharibu chembe za urithi (jeni) tatizo linaloweza kusababisha kuharibika kwa mimba kwa wanawake wajawazito,” amesema Dk Mabula. 

Hata hivyo, kansa ni matokeo ya muunganiko wa sababu mbalimbali ambazo zinatakiwa kuthibitishwa na madaktari wa magonjwa ya binadamu.