July 8, 2024

Kusaga awataka watanzania kumsheherekea Ruge

Amesema hakuna mtu anayeweza kuelezea kwa ukamilifu wasifu wake kutokana na mchango mkubwa alioutoa katika kampuni ya CMG na Taifa kwa ujumla.

  • Amesema hakuna mtu anayeweza kuelezea kwa ukamilifu wasifu wake kutokana na mchango mkubwa alioutoa katika kampuni ya CMG na Taifa kwa ujumla. 
  • Kupitia muziki Ruge aliwaunganisha vijana na viongozi wa Serikali katika shughuli za kijamii.
  • Aliufanya muziki wa kizazi kipya kupata heshima yake katika vyombo vya habari.

Dar es Salaam. Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Clouds Media Group (CMG) Joseph Kusaga amewataka watanzania kusheherekea maisha ya marehemu Ruge Mutahaba kwasababu hakuna mtu anayeweza kuelezea kwa ukamilifu wasifu wake. 

Kusaga maarufu kama Joe amesema alikutana na Ruge miaka 25 iliyopita ambapo tangu hapo alikuwa ni zaidi ya rafiki na ndugu kutokana na mchango mkubwa alioutoa katika kampuni ya CMG na Taifa kwa ujumla. 

Akizungumza kwa majonzi na huzuni leo (Machi 2, 2019) katika hafla ya kutoa heshima za mwisho kwa marehemu katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam, Kusaga amesema watanzania wanapaswa kumsherehekea Ruge kwa sababu alimwambia akifa wasilie.

“Aliyelala hapo ni rafiki yangu kipenzi aliyevuka hata viwango vya kuwa ndugu na rafiki niliyekutana naye miaka mingi iliyopita zaidi ya miaka 20, tulikutana miaka 25 iliyopita tukifanana mawazo, tukayapigania, tukikwama na kufaulu pamoja rafiki nisiye na maelezo ya kutosha ya kumwelezea, “amesema Kusaga 

Amewaambia waombolezaji waliokuwepo katika viwanja hivyo kuwa hakuna mtu anayeweza kuelezea kwa ukamilifu wasifu wa Ruge na kilichobaki ni kusheherekea maisha yake yaliyoacha alama katika mioyo ya watu.


Soma zaidi: 


Amesema marehemu alikuwa mstari wa mbele kuhakikisha tasnia ya habari nchini inapata msukumo wa aina yake kwa kuifungamanisha na muziki wa kizazi kipya ambao umekuwa chanzo cha mapato kwa vijana wengi nchini.   

“Ruge tunayasheherekea maisha yake hapa ametumia miongo miwili iliyopita kuhakikisha tasnia inaendelea katika mwelekeo unaoendana na nyakati akiongoza uzalishaji wa vipindi vya radio, TV na burudani, kuanzisha na kuongoza matukio makubwa ya kiburudani kuyataja machache tu ukiingalia Fiesta ambayo ipo miaka 17.”

“Fiesta imekuwa tamasha kubwa zaidi la muziki Afrika Mashariki na Kati likitoa nafasi  ya kukuza na kuonyesha vipaji na ajira kwa vijana. Unataja vipi Fiesta bila kumtaja Ruge. Ruge ndiye aliyekuwa kinara kabisa wa Fiesta, Halili yupo pale,” amesema Kusuga.

Amesema Ruge alichangia sana Clouds kusimama na yeye kuingi katika tasnia ya habari licha ya mahangaiko mengi waliyopitia wakati wakitafuta namna ya kugusa maisha ya watu hasa vijana kwa kuwafungulia dunia ili wapate kile wanachokitaka. 

Baadhi ya waombolezaji wakiwa ndani ya ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam wakati wakiaga mwili wa marehemu Ruge Mutahaba leo. Picha|Mtandao.

Katika kuonyesha msisitizo, Kusaga aliwataja Rais John Magufuli na Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete kama mashuhuda wa mchango wa Ruge katika jamii na jinsi alivyojitoa kuwaunganisha wasanii na kuhimiza uzalendo na mshikamano kupitia muziki. 

Enzi za uhai wake, Ruge alifanikiwa kuwaleta pamoja takribani wasanii 50 ambao waliimba wimbo wa ‘Tuulinde Muungano Wetu’ na kuwezesha kusikika kwa nyimbo mbalimbali ukiwemo wa ‘Ishi Na Mimi’. 

“Tutakosea Mheshimiwa (Rais Magufuli) tusipoutaja wimbo wa Ishi na Mimi ambao tunafahamu wewe unaupenda zaidi na ule wa ‘Ohoo Tanzania’ ambao Agosti 8 mwaka 2017 kule Chogeni Tanga ulinyanyuka kwenye kiti na kucheza na vijana wako ni kazi ya Ruge Mtahaba aliyelala kwenye jeneza hapo,” amesema Kusaga

Amesema Ruge aliweza kufanya muziki uliokuwa unaitwa wa kiuni uweze kutumika katika shughuli mbalimbali za kijamii ukiwemo mradi wa ‘Malaria Haikubaliki’ ambapo kutipia mradi  huo nchi nyingi za Afrika zilimchukua akawasaidie kwenye miradi ya aina hiyo ikiwemo Ivory Coast, na hata kutoa elimu kwenye sensa.