July 3, 2024

Kushuka kwa bei ya mahindi kulivyowapunguzia maumivu walaji mwaka 2020

Bei ya jumla ya gunia la kilo 100 la mahindi kwa mwaka ulioishia Desemba 2020 ilishuka hadi Sh56,892 kutoka Sh87,59 iliyorekodiwa Desemba 2019.

  • Bei ya jumla ya gunia la kilo 100 la mahindi kwa mwaka ulioishia Desemba 2020 ilishuka hadi Sh56,892 kutoka Sh87,59 iliyorekodiwa Desemba 2019.
  • Walionufaika na kushuka kwa bei hiyo ni wanunuzi hasa walaji huku wakulima wakibaki na maumivu. 
  • Bei za mazao mengine ya chakula nazo zilishuka isipokuwa viazi mviringo na uwele. 

Dar es Salaam. Huenda miongoni mwa watumiaji wa bidhaa walionufaika zaidi mwaka 2020 ni pamoja na wa mahindi baada ya ripoti mpya ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuonyesha kuwa bei ya jumla ya zao hilo ilipungua kwa asilimia 35.1 katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita. 

Ripoti ya Mapitio ya Uchumi kwa mwezi Januari 2021 (Maonthly Economic Review) iliyotolewa na BoT mapema wiki hii inaeleza kuwa bei ya jumla ya gunia la kilo 100 la mahindi kwa mwaka ulioishia Desemba 2020 ilikuwa Sh56,892 ikiwa imeshuka kutoka Sh87,592 iliyorekodiwa Desemba 2019.

Bei hiyo ya Desemba mwaka jana ipo chini kwa asilimia 31.5 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja. 

Kushuka kwa bei hiyo ya mahindi kuliwanufaisha zaidi wanunuzi hasa walaji kwa kuwa hawakulazimika kutoboa zaidi mifuko yao kupata chakula hicho muhimu na utengenezaji wa bidhaa viwandani. 

Lakini wakulima ambao wamewekeza kulima zao hilo ilikuwa ni maumivu  kwa sababu iliwapunguzia faida ambayo wangepata endapo wangeuza kwa bei ya juu au sawa na ile waliouza Desemba 2019. 

Mahindi ni miongoni mwa mazao makuu ya chakula yanayojumuisha mchele, maharage, viazi mviringo, mahindi, mtama, uwele, ulezi na ngano ambayo hutumiwa zaidi na Watanzania.

Hata hivyo, bei za mahindi ndani ya mwaka mmoja uliopita zimekuwa zikipanda na kushuka kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya uzalishaji, hali ya hewa na gharama za usafirishaji. 

Mathalan, mwezi Oktoba 2020, bei ya jumla ya mahindi ilikuwa Sh57,188 na mwezi uliofuata ikapanda hadi Sh58,012 kabla haijashuka mwezi Desemba hadi Sh56,892.


Zinahusiana: 


Pia katika kipindi hicho bei za mazao yote ya chakula zilishuka isipokuwa viazi mviringo na uwele. 

Bei ya jumla ya viazi mviringo hadi Desemba 2020 ilikuwa Sh74,199 ikipanda kutoka Sh69,485 iliyorekodiwa Desemba 2019. 

Uwele ulipanda hadi Sh135,679 kutoka Sh130,428 iliyorekodiwa kipindi kama hicho mwaka 2019. 

“Ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2019, bei za jumla za mazao ya chakula zilishuka isipokua viazi mviringo na uwele ambao ulishuka Desemba 2020 kwa sababu ya kuwepo kwa chakula cha kutosha kwenye masoko,” inaeleza sehemu ya ripoti hiyo ambayo pia inapatikana katika tovuti ya BoT.