October 6, 2024

Kutana na kijana aliyepania kuwainua Watanzania kwa ufugaji wa funza

Wakati wengine wakiona funza kama uchafu, Katala ambaye ni Mtanzania anayesoma katika Chuo cha Afrika cha Uongozi (ALU) kilichopo nchini Rwanda, kwake hiyo ni fursa ya kuboresha maisha yake na jamii.

  • Uzalishaji huo unalenga kuleta mapinduzi katika sekta ya kilimo na ufugaji.
  • Funza hao ambao wanatokana na nzi aina ya “Black soldier” wamesheheni kiwango cha protini na kuwafanya kufaa kwa chakula mifugo.
  • Ufugaji wa funza unapunguza athari uharibifu wa mazingira na gharama za ufugaji.

Dar es Salaam. Sekta ya kilimo na ufugaji huenda ikachukua mkondo mpya, baada ya wabunifu kubuni teknolojia rahisi ya utengenezaji wa vyakula vya wanyama ili kutengeneza fursa za ajira na kipato kwa watu wanaojihusisha na sekta hizo. 

Miongoni mwa wabunifu hao ni kijana Moses Katala ambaye anajishughulisha na ufugaji wa viwavi (funza) ili kuwarahisishia wafugaji kupata chakula cha uhakika kwa ajili ya mifugo wanayofuga nyumbani.

Wakati wengine wakiona funza kama uchafu, Katala ambaye ni Mtanzania anayesoma katika Chuo cha Afrika cha Uongozi (ALU) kilichopo nchini Rwanda, kwake hiyo ni fursa ya kuboresha maisha yake na jamii.

Viwavi ni chanzo kizuri cha protini ambayo inafaa kwa chakula cha mifugo ikiwemo samaki, kuku na nguruwe ikilinganishwa na chakula kinachouzwa sokoni ambacho kinatengenezwa kutumia maharage ya soya.

Katala mwenye umri wa miaka 23 na wenzake watatu kutoka nchi za Rwanda na Uganda kupitia kampuni ya Magofarm Limited wameamua kuvalia njuga ufugaji wa viwavi ambao wanauzwa kwa bei nafuu  ili kuwapunguzia gharama za ufugaji. 

Kwa sasa, vijana hao wanaendesha mradi huo nchini Rwanda na wanaangazia masoko ya bidhaa hiyo katika nchi za Afrika Mashariki ikiwemo Tanzania. 

Kwanini viwavi na siyo kingine?

“Kutokana na takwimu zilizotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa (UN), miaka 40 ijayo Afrika pekee itakuwa na watu zaidi ya bilioni 2 na wote hao watahitaji chakula. Kulisha watu hao, uzalishaji wa chakula lazima uongezeke.

Hivyo ni kusema, uzalishaji huo naongelea uzalishaji wa nyama ikiwemo ya kuku na nguruwe na ukiangalia kwenye ufugaji, vyakula zaidi ya asilimia 70 ya gharama ya ufugaji wa kuku na samaki inatokana na chakula,” amesema Katala.

Hiyo ni fursa hasa kwa vijana kukabiliana na ukosefu wa ajira kwa  kutengeneza chakula cha wanyama kitakachongeza idadi ya mifugo hasa kuku ambao wanahitajika zaidi sokoni. 

Huenda unafikiri ni kazi rahisi lakini Katala amesema uzalishaji wa funza hao kitaalamu unachukua hadi wiki saba kufikia chakula kamili cha mifugo Picha| ALFC.

Funza wanazalishwaje?

Kazi ya uzalishaji funza huanza kwa kuwafuga nzi aina ya “Black soldier” ambapo Katala na wenzie huwaruhusu wadudu hao kutaga mayai na kisha kuyatotolesha mayai hayo ambayo huanza hatua ya ukuaji kama funza ndani ya siku tano.

Funza hao ambao hulishwa uchafu wa majumbani kama maganda ya matunda na mabaki ya chakula, hukua na kufikia sentimita tatu ndani ya wiki mbili ambapo wanakuwa tayari kuvunwa.

Huenda unafikiri ni kazi rahisi lakini Katala amesema uzalishaji wa funza hao kitaalamu unachukua hadi wiki saba kufikia chakula kamili cha mifugo.

Safari ya matengenezo ya mlo huo hufikia kwenye kilele kwa kuwakausha kitaalamu ili kutokuondoa utajiri wa protini na tindikali ya amino iliyopo kwenye funza hao na kisha kuwasaga tayari kwa matumizi.

Kwa mujibu wa Katala, teknolojia wanayoitumia ni mashine ambazo walizinunua nje ya nchi na zinatumika kwenye kuhakikisha mazingira ya wadudu hao kutaga mayai yanafanikishwa.

Asilimia 42 ya wadudu hao ni protini na asilimia 35 ni tindikali ya amino huku masalia yakiwa ni vitamini na madini mengine muhimu kwa ukuaji na afya ya mifugo.

“Tunatambua juu ya mtazamo wa wengi kuona kinyaa kwenye kuwatumia funza hawa kama chakula na ndiyo maana tunawaweka katika hali ambayo kila mtu anaweza kuwa na amani kulisha kuku na mifugo yake,” amesema Katala akitabasamu kutokana na alichosema.


Zinazohusiana


Kwanini mfugaji anahitaji funza

Kwa sasa, wafugaji wengi wa kuku, nguruwe na samaki wanatumia vyakula ambavyo vinatumia soya kama chanzo cha protini.

Tofauti na mlo huo unaotumika sasa, chakula kitokanacho na funza ni rahisi kupatikana huku kikiacha soya kuwa chakula cha kutumiwa na binadamu.

Meshack Ludaila (78) ambaye ni mkulima na mfugaji wa kuku mkoani Mwanza amesema ulaji wa funza kwa kuku haujaanza hivi karibuni kwani katika ufugaji wake, kuku hufurika shambani wakati akilima wakipigania funza wanaokuwa shambani.

“Wapo funza fulani shambani ambao kwenye kulima, ukifukua udongo utawaona. Wana weupe fulani hivi, kuku wakimuona tu, wanampigania na inaonekana ni chakula kikubwa kwao,” amesema Ludaila.

Hata mdau wa ufugaji na kilimo anayehamasisha shughuli hizo kwenye mtandao wa Instagram kupitia @jifunze_kilimo_na_ufugaji, Obison Obadia amesema mbali na ujazo wa protini kwenye funza, wadudu hao wanaweza kumpatia mfugaji mapinduzi kwenye shughuli zake.

Obadia aliyesema chakula mbali na funza kinapatikana kwa Sh15,000 kwa ujazo wa kilogramu tano ameunga mkono hatua ya Katala na kusema itaondoa gharama zisizo za msingi kwa mkulima.

Mbali na ujazo wa protini kwenye funza, wadudu hao wanaweza kumpatia mfugaji mapinduzi kwenye shughuli zake. Picha| Bioenergyconsult.

Matarajio aliyonayo kwa Tanzania

Katala amesema ana mpango kutumia taka zinazozalishwa majumbani kutengeneza funzo na kwa kuanzia wataanza kutumia tani mbili za taka zinazozalishwa katika jiji la Dar es Salaam ambazo zinapatikana kwa wingi na kuharibi mazingira ya jiji hilo. 

Kwa mujibu wa ripoti ya Takwimu za Taifa za Mazingira ya mwaka 2017 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Hadi kufika mwaka 2017 uzalishaji wa taka katika jiji hilo ulifikia takribani tani 4,600 kwa siku huku asilimia 75 ya taka hizo zikizalishwa majumbani.

Kwa sasa Katala anaendesha mradi huo nchini Rwanda huku akiwa na matazamio makubwa ya kuileta biashara hii nchini Tanzania.

“Tumeshanunua eneo Singida na tumeshalilipia. Karibuni endapo majaaliwa, tutaanzisha kiwanda hikii nchini Tanzania,” amesema Katala.

Amewashauri vijana kutumia changamoto zilizopo katika bara la Afrika kwani “lina changamoto nyingi sana hivyo hatuna budi kuzitumia changamoto hizo kama fursa.”

“Vijana wengi wanatafuta kazi ambazo wanakuwa comfortable (wanarizika) nazo. Sikatai, hata mimi nilipoanza harakati hizi haikuwa rahisi  lakini kwakuwa ninafahamu ninachokifanya, ninaendelea na kazi.”