November 24, 2024

Kutana na Mtanzania anayechochea mapinduzi ya kidijitali sekta ya utalii

Kupitia jukwaa alilolibuni, mtu anaweza kutembelea vivutio vyote vilivyopo nchini na kufurahia utalii kwa njia rahisi za uhifadhi gharama.

  • Ni jukwaa la mtandao linalomwezesha mtu kuweka pesa kidogo kidogo kwa ajili ya utalii.
  • Jukwaa hilo linatoa taarifa za vivutio vya utalii vilivyomo Tanzania na namna ya kuvifikia.

Dar es Salaam. Siyo kwamba watu hawapendi kufanya utalii wa ndani, wanapenda sana lakini mchakato wa kujiandaa na safari moja ya utalii ni pasua kichwa.

Mambo kama ufikirie wapi utalala, utatumia usafiri gani, utafanya nini huko uendapo huku bajeti yako ikiwa nayo ni ya makadirio yasiyo na uhakika ni kati ya vitu ambavyo baadhi ya watalii wa ndani wanaona kama kikwazo kufika sehemu mbalimbali za utalii.

Tanzania inasifika zaidi kwa vivutio vya mbuga za wanyama, fukwe za baharini na maziwani, milima na malikale.

Kuangalia jambo hilo kama fursa, Prisca Magori aliumiza kichwa na kuibuka na jukwaa la kidijitali la kumsaidia mtu kuweka pesa kidogo kidogo kwa ajili ya kufanya utalii wa ndani.

Kwa lugha rahisi ni sawa na kusema, mfano kama unataka kwenda kupanda Mlima Kilimanjaro mwezi wa 12 mwaka huu, unaweza kuanza kuweka pesa kidogo kidogo hadi kufikia Disemba ukawa umekamilisha kiasi ambacho kitakidhi mahitaji yako yote ya safai hiyo.

Kuanzia chakula, sehemu ya kulala, usafiri na kila kitu. Ni wewe kubeba nguo zako tu! Ni kama kusema, jukwaa hili ni kibubu cha utalii.

Corona ilivyoibua wazo

Magori ambaye ni mtaalamu wa masuala ya uhandisi wa petroli alipata wazo hilo kipindi cha mlipuko wa ugonjwa wa Corona, baada ya baadhi ya nchi kufunga mipaka yake na hivyo kupungua kwa idadi ya watalii kutoka nje ya nchi.

“Mimi ni rafiki zangu tulifanya utafiti tukagundua kuwa waongoza utalii wengi waliwekeza kwa wageni wa kutoka nje ya nchi. Waliwasahau wazawa,” amesema Magori.

Changamoto nyingine iliyobainika ni kuwa Watanzania wengi hawana tabia ya kutalii kutokana na ukubwa wa gharama za kufanya hivyo hasa wakiwaza juu ya usafiri, malazi na chakula.

“Endapo tutamrahisishia Mtanzania kuhifadhi pesa mdogo mdogo nje ya mipaka yake, anaweza kufikia ndoto zake za kitalii kwa kununua vifurushi mbalimbali anavyoweza kumudu,” amesema Magori.

Binti huyo na wenzake walianza kufanyia kazi mawazo yao na hapo ndipo walipobuni programu tumishi (app) inayoambatana na tovuti ya TenTen Explore.

Hadi sasa Prisca ametoa nafasi nne za ajira huku akiwa na malengo ya kufungua fursa zaidi kwa vijana. Picha| Gift Mijoe.

TenTen Explore na utalii wa ndani

“TenTen Explore” inatoa fursa ya mtu kuchagua kifurushi cha utalii ambacho kinakuwa kimetengenzwa na watoa huduma na kukiweka ndani ya jukwaa hilo na kisha kukiwekea malengo ya kulipa ikiwa ni papo kwa happo, kwa wiki, wiki mbili au kwa mwezi.

“Kwa ambao tayari wanahamasa na utalii, wanaweza kulipa pesa yote kwa mkupuo na kisha kuendelea na utalii lakini kwa ambao hupata shida ya kuweka fedha kwa ajili ya utalii, wanaweza kuweka kidogo kidogo hadi wafikishe lengo lao,” amesema Magori.

Ikiwa ni miezi mitatu tangu kusajiliwa kwa jukwaa la TenTen Explore, app ya jukwaa hilo imepakuliwa na watu 1,500 ndani ya mwezi mmoja tangu kuzinduliwa kwake na tayari kuna vifurushi vya mtu mmoja, wapenzi wawili, familia na makundi huku safari zikianzia kima cha uhifadhi wa hadi Sh3000 kwa wiki.

Mathalan, safari ya mtu mmoja ya kwenda Zanzibar Disemba 9 mwaka huu, inagharimu  Sh72,600 na mtu anaweza kuchagua kuilipia kwa Sh3,457 kila wiki hadi wiki 21 au ukalipa Sh6,600 mara mbili kwa mwezi kwa wiki 11.

Kifurushi hicho hicho ambacho kinaambatana na kufurahia michezo ya baharini, vyakula, vinywaji na kupiga mbizi (snorkeling) kinaweza kulipiwa kwa awamu (instalment) sita endapo mtu atachagua kulipa Sh12,100 kila mwezi au akalipa sh72,600 kwa mkupuo na kungoja safari yake.

Hata hivyo, fedha hiyo haijumuishi gharama za usafiri wa kufika Zanzibar, vinywaji vikali (liquor) pamoja na tozo za kuendesha boti za baharini.

“Uzuri ni kuwa mfumo unakuelezea kila kitu kinachoambatana na kifurushi hicho ikiwemo vitu utakavyopata kwa pesa yako na vitu ambavyo utatumia pesa yako mwenyewe,” ameelezea Magori ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa jukwaa hilo.


TANGAZO


Ni nini kipya kwa TenTen Explore

Huenda ukafikiri TenTen Explore ni waandaaji wa safari lakini hapana, ni daraja la kiteknolojia kati ya waandaaji wa safari na watalii kwani kabla ya jukwaa hilo, ulihitaji kupekua mtandaoni endapo kuna safari imeandaliwa ili na wewe uungane nayo.

TenTen Explore imeondoa hilo kwa kuzisogeza safari zote hizo kwenye jukwaa moja na kuziboresha zaidi kwa kumpa mtu uwezo wa kutumia jukwaa hilo kuchagua kifurushi cha kwenda mwenyewe na ampendaye au familia na makundi  huku wakiwa hawana mawazo ya wapi watafikia, wapi watalala au wapi watakula kwa siku hiyo.

Zaidi, TenTen Explore inamwezesha mtu kulipa pesa yake kidogo kidogo kwa njia ya mtandao huku ikimhakikishia mteja wake kurudishiwa fedha yake pale anapoahirisha safari lakini akitoa taarifa mapema.

“Ukitoa taarifa mapema, tunarudisha asilimia kadhaa ya fedha yako uliyotoa lakini endapo umetoa taarifa na siku ya safari imefika, hatutokuwa na la kufanya mbali na kukupa ruhusa ya kusogeza mbele safari yako. 

“Japo kwa baadhi ya vifurushi vingine unaweza kuhitajika kuongezea fedha ili waweze kukutengea nafasi ya kusafiri tarehe ya mbeleni,” ameeleza Magori huku akisema mifumo ya malipo ni kwa njia ta TigoPesa na MPesa kwa sasa huku huduma za kadi za benki zikiwa mbioni kuongezwa.

Kupitia TenTen Explore, mtu anaweza kutembelea vivutio vyote vilivyopo nchini na kufurahia utalii.

Changamoto na malengo

Kila jema halikamiliki bila kupitia milima na mabonde na kwa mabonde ya binti huyu katika kuchangia utalii wa ndani, ni tozo za kutengeneza maudhui kwa ajili ya matangazo ya vivutio vya utalii pamoja na ushirikiano mdogo kwa baadhi ya watoa huduma ikiwemo wamiliki wa hoteli.

“Tozo za kurekodi video na picha kwenye vivutio ni ghali sana kwa kampuni changa. Kwa vivutio vya majini (marine reserves) ni takribani Sh2.3 milioni kwa kurekodi video kwa wiki moja. Pia kwa wanaomiliki sehemu za utalii wengi wao wamejikita kutoa huduma kwa wageni wa nje na inakuwa changamoto kwa wao kubadili nadharia zao ikihitajika kuandaa maudhui yanayoendana na hali za wazawa ili kufikia mahitaji yao,” ameelezea Magori alikisema yeye na timu yake wanapambana hivyo hivyo.

Ndoto ya timu hii ya vijana ni kuongeza wigo wa ajira katika sekta ya utalii hasa kwa vijana na kuhamasisha utalii miongoni mwa Watanzania na wageni.

“Tamaa yangu ni kuona wageni wakiitumia TanTen kuja kutalii nchini na tukiongeza wigo wa vituo vya utalii kwa kufikia nchi zingine za Afrika. Ifike kipindi mtu akitaka kwenda kutalii Kenya, atumie TenTen Explore moja kwa moja,” amesema mwana dada huyo ambaye ndani ya miezi mitatu tangu kuzinduliwa rasmi kwa TenTen Explore, ametoa fursa ya ajira kwa vijana wanne.

Kupitia jukwaa la TenTen Explore, mtu anaweza kulipa fedha kidogo kidogo na kutimiza ndoto zake kitalii. Picha| TenTen Explore.

Nini kiboreshwe  TenTen Explore

Wadau wameshauri timu hiyo kuangazia masuala ya malipo kwa kuweka njia zinazoaminika kimalipo ikiwemo mfumo wa “Nilipe”, na “E Wallet” ambazo ni maarufu katika shughuli za utalii.

Mkuu wa Biashara na Mafunzo wa kampuni ya habari na teknolojia ya Nukta Africa, Daniel Mwingira amesema kwa kutumia mifumo ambayo tayari ni jumuishi, itakuwa rahisi kwa watalii wengi zaidi kufikia huduma za TenTen Explore kwani hadi sasa inamaanisha ni watoa huduma za kifedha kwa njia ya simu wawili tu ndiyo wanaifikia TenTen Explore yaani TigoPesa na MPesa.

Bado unasubiri ajira? Ushauri wangu kwako ni kuangalia changamoto ambazo unapitia na kutafutia suluhu ambayo itakupatia ajira. Tumemwona Moses Katala na ufugaji wa funza kwa ajiri ya wafugaji wa mifugo, Idrissa Magesa na biashara ya uji na Jessica Mashama ambaye biashara na muziki ni sehemu ya kujikwamua kwake. 

Kazana, huenda siku zijazo, Nukta Habari itaandika stori yako.