July 3, 2024

Kutana na mwanaume aliyeishi bila utaifa kwa zaidi ya miaka 70

Ni Sergio Chekaloff ambaye anaishi Hispania baada ya kupewa hadhi ya kutokuwa na utaifa.

  • Ni Sergio Chekaloff ambaye anaishi Hispania baada ya kupewa hadhi ya kutokuwa na utaifa.
  • Alizaliwa mwaka mmoja baada ya vita ya pili ya dunia kwenye kambi ya wakimbizi ya Ujerumani.
  • Mpaka sasa hajafahamu asili ya nchi yake. 

Dar es Salaam. Haki ya kuishi na kuwa huru kwenye Taifa lako ni ya kila binadamu bila kujali hali  ya kimaisha. Lakini kwa baadhi ya watu haki hii kwao ni kama ndoto. 

Miongoni mwa watu hao ambao wamekua wakitafuta utaifa (nchi ya asili) kwa muda mrefu ni Sergio Chekaloff ambaye kwa zaidi ya miaka 70 ameishi katika nchi mbalimbali duniani kama mkimbizi. 

Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), Chekaloff ameishi katika hali hiyo baada ya nchi tatu alizodhani kuwa ni asili yake ambazo ni Ujerumani, Urusi na Armenia zote kukataa kumtambua.  

Mwanaume huyo mwenye miaka 74, kwa msaada wa UNHCR anaishi Ibiza nchini Hispania baada ya kupewa hadhi ya kutokuwa na utaifa.

Akihojiwa na redio ya Umoja wa Mataifa, Chekaloff amesema hana utaifa baada ya kuzaliwa kwenye kambi ya wakimbizi nchini Ujerumani mwaka 1946 walikokutana wazazi wake ambako mama yake alikua akifanya kazi ya utafsiri kambini hapo. 

“Mama yangu alikuwa Mjerumani, baba yangu Mrusi akitoka eneo la Yerevan ambalo sasa ni mji mkuu wa Armenia na alienda kwenye vita vya pili vya dunia (kati ya mwaka1939 na 1945). 

“Huko ndiko baba na mama yangu walikokutana kwenye kambi ya wakimbizi, vita vilipomalizika na makambi kuundwa. Baada ya mwaka mmoja hivi nikazaliwa na hapo walikuwa wanapanga kwenda Argentina.” 

Sergio ameishi miaka 60 nchini Argentina akitumia kitambulisho cha kigeni kabla ya kuhamia Hispania anakoishi sasa na familia yake. 

Kwa muda mrefu hadhi ya utaifa ya Chekaloff haikuorodheshwa popote hadi UNHCR lilipomsaidia kuomba hadhi ya kutokuwa na utaifa nchini Hispania ambayo aliipata rasmi mwaka 2019 kwa sababu kila alikodhani ni asili yake walimkana. 

“Kwa Waargentina wanasema mimi ni Mjerumani, kwa Wajerumani wanasema ni Mrusi, kwa Warusi wanasema baba yangu alizaliwa Armenia na Armenia hawajapata nyaraka yangu yoyote nao hawanitaki pia, hivyo sina utaifa,” amesema mzee huyo akihojiwa na redio ya Umoja wa Mataifa.  


Soma zaidi: 


Kuishi bila utaifa maana yake nini?

Kwa mujibu wa UNHCR duniani kote kuna mamilioni ya watu wanaoishi kama Chekaloff bila utaifa wowote, na mpaka sasa hakuna takwimu rasmi zinazobainisha suala hilo. 

Kukosa utaifa kunaweza kutokea kwa sababu mbalimbali ikiwemo unyanyasaji wa kikundi fulani cha kijamii au kidini; au kwa misingi ya jinsia; kuibuka kwa Taifa jipya na kuhama kwa mataifa yaliyopo; na ugomvi unaotokana na sheria za uraia. 

UNHCR inaeleza zaidi kuwa kukosa utaifa ni matokeo ya sera ambazo zinadhamiria kuwatenga watu ambao wanadhaniwa kuwa ni wageni wa eneo fulani.

Mathalani, zaidi ya watu 600,000 wa mji wa Rakhine nchini Mynamar hawana utaifa kutokana na sheria ya sasa ya uraia, ambayo inatoa fursa ya utaifa kwa wanachama wa makundi ya kijamii yanayotambulika pekee.