October 6, 2024

Kutoka binti mpole hadi kubwa la maadui

Estella anayekua akijua mama yake amekufa, anagundua kuwa mama yake yupo hai na aliagiza mauaji yake wakati akiwa mtoto.

  • Ni simulizi inayomhusu mwanadada ambaye maisha na wanadamu wanamgeuza kubwa la maadui.
  • Licha ya kuwa na kipaji cha kutosha kubadili dunia, waliojua hawamruhusu kuungana nao.
  • Visasi vinaanza baada ya kufahamu mama yake aliagiza kuuawa kwake wakati akiwa mdogo.

Katika kutafuta mafanikio kila mtu atakupatia stori ya mambo ambayo amepitia na kuyafanya. Wapo waliofanya mambo mazuri na wengine waliofanya meusi na ya kushangaza. 

Katika safari ya watenda mambo mabaya, wapo walioua, waliolazimika kukimbia familia zao na wengine wakiamua kuwa wakimbizi katika nchi zilizofanikiwa. Licha ya kuwa mambo hayo meusi ni mabaya lakini ndiyo ilikuwa njia kuu aliyotumia Estella ama Cruella de Vil kuishi duniani. 

Baada ya kumpoteza mama yake, Estella anakimbiilia mjini ambako anakutana na marafiki wawili wanaomfundisha jinsi ya kuishi na watu wa mjini.

Wanamfundisha wizi na ulaghai ili aweze kujipatia fedha za kujikimu maisha ikiwemo kupata chakula katika jiji la London ambalo bila pesa za kueleweka huenda ukahesabu idadi ya nyota usiku.

Wizi na udanganyifu siyo kitu ambacho Estella anatazamia kukifanya maisha yake yote kwani mbali na kuwa msichana aliye na kismati cha kupendwa na mbwa, binti huyo anatalanta kubwa ya ubunifu wa mavazi.

Kama una shughuli ambayo ungependa kwenda na kila jicho ligeuke kwako kiasi cha kuteteresha mahusiano yaliyomo katika ukumbi utakaotembelea, Estella ndio mbunifu wa kumkabidhi kazi ya kukuvisha.

Siku ya kumbukizi yake ya kuzaliwa, rafiki zake wawili, Jasper na Horace wanamzawadia ajira ya kuwa mfanya usafi katika mojawapo ya maduka ya mavazi jijini hapo na ndipo ndoto ya Estella inapoanzia.

Baada ya kupata ajira hiyo, kwa Estella ni kana kwamba milango ya maisha yake imefunguka kwani kwa maisha yake yote amekuwa akichezea vitambaa mikasi na pini. Japo anafanya kazi ya usafi tu lakini kwa kuwa anafanyia usafi vitu anavyovipenda, kwake ni embe dodo chini ya mnazi.

Wakati akiendelea na kazi zake, Estella anaanza kuweka pua yake isipostahili yaani kiherehere  kwa kutoa maoni yake juu ya nguo zinazotengenezwa dukani hapo.

“Hii ingependeza kuwa na mikono mifupi, hii haijapendeza ila ukitoa hii huenda itakaa sawa,” ni baadhi ya marekebisho ambayo Estella anakuwa anapendekeza lakini kwa kuwa ni mfanya usafi, nani ayatilie maanani?


Soma zaidi:


Karibu, tunaweza endelea. Siku moja, Estella akiwa amelewa kidogo, alifanikiwa kutengeneza sehemu ya maonyesho ya mavazi na kitendo hicho kilibadilisha maisha yake kwani alifanikiwa kugusa moyo wa gwiji wa fashion Jijini London.

Baroness von Hellman ambaye ni mama wa Fashion katika jiji hilo, anaona kazi ya Estella asubuhi na hapo hapo, anamuajiri binti huyo katika timu yake ya wasomi waliobobea katika ubunifu wa mavazi na baadaye cheo chake kinapanda na kuwa msimamizi wa mipango ya Baroness. Ushawahi kusikia kukanyaga ganda la ndizi? ndio huku!

Je, Estella atafanikiwa kufikia ndoto yake hasa baada ya kugundua ukweli kuwa Baroness ndiye aliyehusika katika kifo cha mama yeke na pale fumbo kuu litakapofichuka kuwa Baroness ndiye mama yake mzazi aliyemkataa binti huyo na kuagiza aangamizwe kipindi akiwa mdogo?

Shuhudia binti mpole, mrembo na mnyenyekevu anavyogeuka kuwa adui mkuu almaarufu kama Cruella.

Usaliti, wema, utu na watu kujihisi miungu watu ni sehemu ya filamu hii ambayo inapatikana katika kumbi za kuangalia filamu.

Tazama filamu hii kujifaidia mafunzo ya utafutaji katika maisha huku elimu ya ya kupambania ndoto zako ikiwa ni sehemu ya wewe kuwa karibu na skrini utakayoichagua.