Kwangwaru ya Harmonize inavyotikisa Youtube
Wimbo huo ulioingia Youtube Aprili 14, 2018 umetazamwa na watu wengi zaidi tangu mwaka huu uanze na kuzifunika nyimbo zingine za wasanii maarufu Tanzania.
- Wimbo huo ulioingia Youtube Aprili 14, 2018 umetazamwa na watu wengi zaidi tangu mwaka huu uanze na kuzifunika nyimbo zingine za wasanii maarufu Tanzania.
- Wasanii waifagilia Youtube kwa kuwakutanisha na mashabiki wao duniani.
- Wataalam wa muziki wahimiza mabadiliko ya teknolojia katika kazi za wasanii
Dar es Salaam. Ni miezi mitano sasa imepita tangu wimbo wa “Kwangwaru” ulioimbwa na msanii Rajab Kahali a.k.a Harmonize akimshirikisha Nasib Abdul (Diamond Platnumz) ukitamba katika mitandao ya kijamii ikiwemo Youtube ambao ni mahususi kwa kurusha video mbalimbali.
Wimbo huo ni kati ya nyimbo zilizowika zaidi Aprili na Mei mwaka huu wa 2018 na kupokelewa vizuri na mashabiki wa msanii huyo kutoka kona mbalimbali za dunia.
Kwangwaru uliingia Youtube Aprili 14, 2018 umekuwa ni wimbo aliotazamwa na watu wengi zaidi tangu mwaka huu uanze na kuzifunika nyimbo zingine za wasanii wakubwa Afrika Mashariki.
Uchambuzi uliofanywa na Nukta katika mtandao wa Youtube hadi Septemba 20 mwaka huu wa nyimbo za wasanii wa Tanzania zinazotamba katika mitandao ya kijamii, umebaini kuwa Kwangwaru umepata watazamaji 25.7 milioni na kuvunja rekodi kwa kutazamwa za watu wengi zaidi.
Kwangwaru umeendelea kuwa gumzo na kivutio kikubwa, ikizingatiwa kuwa umeupita kwa watazamaji 3 milioni wimbo wa ‘African Beuty’ wa msanii Diamond Platnumz ambao uliingia Youtube Machi 16 mwaka huu ikiwa ni mwezi mmoja kabla ya Kwangwaru kutoka na hadi Septemba 20 mwaka huu umejipatia watazamaji 22.7 milioni.
Katika wimbo wa African Beauty ambao Diamond alimshirikisha msanii wa kimataifa, Omari Grandberry (Omarion) ambaye ana mashabiki wengi zaidi duniani.
Hiyo ina maana kuwa takribani watu 5.2 milioni hutazama wimbo huo kila mwezi ambapo idadi ya watazamaji inaongezeka kwa kasi, licha ya jimbo mpya za wasanii mbalimbali kuingia Youtube tangu April mwaka huu.
Pia Idadi hiyo inaonekana kuwa kubwa ikizingatiwa ziko nyimbo za wasanii mbalimbali nchini ambazo hazijafikia rekodi ya Kwangwaru.
Hata hivyo, wimbo huu umekuwa ni mafanikio makubwa kwa Harmonize kwasababu umevunja rekodi ya kutazamwa na watu wengi kuliko nyimbo zake zote alizowahi kuzitoa tangu alipoanza kusikika zaidi mwaka 2015 kwa kibao chake cha Aiyola.
Zinazohusiana:
- Wanafunzi vyuo vikuu waugeukia muziki kutoka kimaisha.
- Maboresho: Kupitia Twitter utatazama video mubashara.
Siri ya Kwangwaru kutamba Youtube yatajwa
Kwa wasanii wakongwe kama Dully Sykes wanalichukulia jambo hilo la Harmonize kama ni mafanikio makubwa yanayoacha changamoto kwa wasanii wengine kuboresha kazi zao ili zipate muitikio mkubwa katika jamii.
Dully Sykes ambaye pia amefanya kazi na Harmonize kwenye wimbo wake wa “Inde” amesema kwa kiasi fulani Youtube imembeba msanii mwenzake na kumuweka kwenye ramani ya dunia.
“Hili ni swala kubwa sana kiukweli kwasababu vijana wanaangalia huko. Hata mimi natazamia huko kwa sababu kipindi ninaanza muziki hakukuwa na Youtube wala mitandao ya kijamii,” anasema Dully Sykes.
Mkuu wa Idara ya Sanaa na Ubunifu kutoka Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Kedmon Mapana, amesema zama za muziki zimebadilika, watu wanataka kutunga na kuonyesha kazi zao kwa haraka.
Amesema YouTube imekatilia mbali ukiritimba kwa wasanii wa muziki kwasababu inawapatia uhuru wa kusambaza kazi zao bila kuingiliwa na mtu.
“Yawezekana kulikuwa kumejaa ukiritimba kwenye vyombo vya habari kama redio na TV. Ili wimbo wako uchezwe ilikuwa lazima upitie kwa mtu na kuukubali. Youtube haina ukiritimba wowote mtu anaweka wimbo wake na anausambaza,” anasema Dk Mapana
Amebainisha kuwa mabadiliko ya sayansi na teknolojia yamechangia kubadilisha mfumo wa usimamizi wa muziki kutoka mikononi mwa watu wachache ambao walikuwa wananufaika na kazi za wasanii.
Watu wengi wamehamia kwenye simu za mikononi na hata hivyo watu wengi wanaona ni heri watumie mitandao ya kijamii katika kusambaza kazi zao za sanaa na kuwataka wadau wa muziki waanze kufundisha masomo yanayohusu teknolojia ya muziki ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia yanayotokea duniani.
Nukta ilimtafuta Harmonize ili kuelezea siri ya mafanikio yake ambapo amesema hawezi kuongea wakati huu kuhusu nyimbo zake zilizopita kwasababu yuko kwenye maandalizi ya kutoa wimbo mpya ambao anadhani utakuwa na muitikio mkubwa kwa wafuasi wake.
“Sifanyi mahojiano sasa hivi, nikiwa tayari nitakwambia,” amesema Harmonize wakati akijibu simu ya Mwandishi wa Nukta.
Msanii Rajab Kahali a.k.a Harmonize (aliyesimama katikati) amepata mafanikio katika kipindi kifupi. Picha| Millardo Ayo.
Ubora na wafuasi ni kiki nyingine kwa mtandao wa Youtube
Mategemeo ya kila kazi anayofanya binadamu ni kumpatia malipo kwa namna yeyote ile.
Malipo hayo huja kwa njia ya fedha, fadhila au hata neno “asante”. Vivyo hivyo wasanii wengi wa muziki wa kizazi kipya (Bongo Fleva) hutegemea kunufaika na kazi zao, kama ilivyo kwa kazi zingine kama udaktari, ualimu na hata Uhandisi.
Kabla ya wasanii kufahamu nguvu ya mitandao ya kijamii, walitegemea televisheni na redio ili kusambaza kazi zao lakini mambo yamebadilika na wameanza kuigeukia mitandao ya kijamii hasa Youtube kama njia ya kuwafikia mashabiki wao waliopo maeneo mbalimbali duniani.
Tofauti kubwa kati ya Youtube na majukwaa mengine ni kuwa mtandao huo unaweza kuvuka mipaka ya nchi ukilinganisha na runinga na radio ambazo zinawafikia watu wa eneo fulani tu.
Kwa msanii wa muziki wa Bongo Fleva kama Juma Said a.k.a Jay melody, mtandao huo umemsaidia kumtangaza kimataifa ambapo angetumia vyombo vya habari vya kawaida asingefika mbali.
“Mtu wa Mali na Angola na kwengineko anaweza ona kazi zako bila kuwa nchini kwako. You tube Inaangaliwa na watu wengi na kufikia watu kirahisi japo kila jukwaa lina umuhimu wake” anasema Jay.
Youtube imeenda mbali zaidi na kugusa maisha ya wadau wengi wa muziki wakiwemo wasimamizi, waandaji wa video na wapiga picha. Lakini ili mtu yeyote afaidike na fursa zilizopo Youtube inambidi afanye kazi kwa bidii na kuzingatia ubora, viwango vya kimataifa vya muziki.
Mkuu wa Kitengo Cha Dijitali kutoka kampuni ya Clouds Media Group, Bilal Saadat na Mtayarishaji wa vipindi, Faraji Kakingo wanasema mtandao wa Youtube humlipa mtu pale tu vigezo muhimu vinapokuwa zimezingatiwa.
Pia malipo hayo hutegemea idadi ya wafuasi alionao msanii na idadi ya watazamaji wanaotazama na kusikiliza nyimbo husika.
“Kwa mtu mwenye watazamaji 54,000 analipwa hadi Dola za Marekani 2,100 (Tsh4,796,351) kama mzunguko wa kazi yake ni mkubwa. Kwa watazamaji hao hao mtu anaweza kulipwa Dola 2,000 na mwingine Dola1200,” anaseama Kakingo.
Tofauti ya malipo ya wasanii wanaotumia Youtube pia hutegemeana na kasi ya watazamaji kuangalia matangazo katika mtandao huo.
Saadati anabainisha kuwa wasanii wanaotaka kutoka kupitia Youtube wanapaswa kuwa ni mikakati kabambe ya kuboresha kazi zao na kuwahimiza wafuasi wao kuangalia matangazo yanayorushwa mtandaoni.
Kwa mujibu wa utaratibu wa Youtube, mtu huanza kulipwa pesa ikiwa mzunguko wa malipo yake umefika Dola 100 (Tsh 228,401)