November 24, 2024

Kwanini huwezi kuukuta mswaki kwenye chumba cha hoteli?

Pamoja na huduma zote nzuri utakazopata hotelini, ni mara chache sana katika hoteli hizo kupata mswaki kwa ajili ya kusafisha kinywa, licha ya kuwa ni kifaa muhimu kwa afya ya binadamu.

  • Ni kwa sababu wageni hawaombi kifaa hicho wakifika hotelini.
  • Baadhi ya hoteli zinapunguza gharama na haziwezi kumpa kila mteja mswaki.
  • Hata hivyo, bado una nafasi ya kuomba kwa wahudumu kama hujabeba wa kwako.

Dar es Salaam. Hoteli ni sehemu muhimu ya wageni au wasafiri kumpumzika wakati wakiendelea na majukumu mengine ya kibiashara, matembezi au kikazi.

Raha ya kukaa hotelini ni kuwa unakutana na mazingira tofauti uliyoyazoea nyumbani hasa muonekano wa choo na huduma unazopata ukiwa ndani ya chumba. Kwa ujumla ni raha inayoambatana na utulivu wa nafsi.

Pamoja na huduma zote nzuri utakazopata hotelini, ni mara chache sana katika hoteli hizo kupata mswaki kwa ajili ya kusafisha kinywa, licha ya kuwa ni kifaa muhimu kwa afya ya binadamu.

Huenda wapo watu wanaochukizwa wanapokuta miswaki haijawekwa kwenye vyumba vya hoteli, lakini zipo sababu za msingi kwanini hoteli haziweki miswaki kwenye vyumba vya kulala wageni.

Moja ya sababu hizo ni kuwa, wageni wengi wakienda hotelini hawaombi miswaki kwa wahudumu. Kwa hiyo hoteli hazijishughulishi kuwapatia wateja huduma hiyo.


Soma zaidi:


Baadhi ya watu wanaamini kuwa miswaki ni kifaa muhimu kwahiyo kinahitaji umakini katika kuhifadhi. Ndiyo maana wengi hubeba miswaki yao na hawawezi kutumia miswaki ambayo hawajaithibitisha. 

Kwa mujibu wa mtandao wa Reader’s Digest, baadhi ya hoteli hazitoi miswaki ili kupunguza gharama za kumpa kila mteja kifaa hicho. Badala yake gharama hizo huzielekeza kutoa vitu vingine kama sabuni zenye manukato mazuri ili kuwavutia wateja.

Hata hivyo, haikuzuii kwenda kwa wahudumu wa hoteli kuomba upewe ikiwa, umesahau kubeba mswaki wako.