Kwanini simu ya mpenzi wako ni kitunguu machoni
Tabia hiyo huchochewa na dhana za ukosefu wa uaminifu na mawasiliano duni.
- Mwanaume mmoja kati ya watano hupekuwa simu za wapenzi wao.
- Tabia hiyo huchochewa na dhana za ukosefu wa uaminifu na mawasiliano duni.
- Kuchungulia simu ya mpenzi wako huleta madhara mengi.
Dar es Salaam. Katika mahusiano ya kimapenzi, yapo mambo mengi ambayo husababisha ugomvi kati ya mtu na mpenzi wake. Kukosa mawasiliano, wivu, usahaulifu na tabia ya kukagua simu ya mwezi wako.
Ni wachache ambao hupitia simu za wapenzi wao na kuirudisha simu hiyo wakiwa na amani kama walivyokuwa nayo wakati wanaishika.
Kitendo hicho huwaacha baadhi ya watu katika filamu inayoisha kwa kumwaga machozi.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na tovuti ya habari ya Avast (2014) nchini Marekani, katika kila wanaume watano, mmoja anachungulia simu ya mpenzi wake na kati ya wanawake wanne, mmoja huchungulia simu ya mpenzi wake.
Sababu kubwa ya watu kuchungulia simu za wapenzi wao ni pamoja na kufikiri kuwa mwenzi wake anachepuka, kukosa imani naye na kuyumba kwa mawasiliano hivyo kutaka kujua yamehamia wapi.
Katika upekuzi huo, watu huangalia jumbe zinazotumwa na tabia yake ya mtandaoni. Upekuzi huo hujikita zaidi kwenye mitandao ya kijamii ikiwemo Instagram, Facebook na Twitter.
Hata hivyo, mapokeo ya tabia hiyo yanatofautiana kutoka kwa mtu na mtu. Wengine wanachukulia kitendo hicho kama kipimo cha uadilifu katika mahusiano huku wengine wakisema ni kuingilia faragha ya mtu kwani kuwa kwenye mahusiano haikupi ruhusa ya kutaka kufahamu kila jambo linalomhusu.
Je kuna wakati sahihi wa kupekua simu ya mpenzi wako? Picha| Thought Catalogue.
Yanini kujipa presha ya maisha?
Kwa kuwa kupekua simu ya mtu inasababishwa na mabadiliko ya tabia na mtu kuhisi kuwa hayupo peke yake, baadhi wanaona haipo haja ya kuchunguza simu ya mtu kama haonyeshi dalili ya kukosa uaminifu kwako.
Mkazi wa Japan, Whitney Ndusilo, amesema kuna haja ya kupitia simu za wapenzi wao kwa sababu siku hizi watu wanatumia muda wao mwingi kwenye simu hata kama wakiwa wamekaa wawili na zaidi.
Hali hiyo huanza kujenga “kihumwehumwe” cha mtu kutaka kujua mpenzi wake anafanya nini kiasi cha kushindwa kuongea naye na badala yake kutumia simu.
“Kuna wale watu ambao wanafuata mikumbo, wenzi wao wala hawana tuhuma zozote lakini kwa sababu shoga yake hupekua simu ya mumewe, na yeye atafanya ,” amesema Ndusilo.
Binti huyo amesema yeye anapenda mtu mstaarabu ambaye anajua umuhimu wa uwepo wake hivyo anahitaji mtu mkweli na anayemuheshimu.
Endapo mpenzi wake anamjali, haoni haja ya yeye kuanza kujipa mshtuko wa moyo katika umri mdogo kwa kupekua simu ya mtu.
TANGAZO:
Kupekua simu ya mtu ni kuingilia faragha
Unaposhika simu ya mpenzi wako na kukagua mazungumzo yake, kwa baadhi ni sawa na kuingilia yasiyokuhusu kwani kama kuna jambo na hajakuambia, ina maana kuwa muda mwafaka haujafika wa wewe kujua.
Mkazi wa Dar es Salaam, Ibrahim Samwel amesema kuchunguza simu ya mpenzi wako ni mbaya kwa sababu inaweza leta mafarakano baina ya wapenzi wawili na pia unakuwa unafuatilia ambayo hayakuhusu kwa muda huo.
“Kuna vitu hasa vya ndani ya familia ya kila mmoja wapo huwa anaongea na ndugu zake ambavyo mke au mume hapaswi kujua isipokua kwa wakati sahihi,” amesema Samwel.
Ni muhimu kufahamu kuwa mwenzi wako ana uhuru wa kuwa na marafiki. Huenda maudhui wanayotumia yanaweza yasikufae kwa sababu watu wana njia tofauti za kuwasiliana.
Simu ni kifaa cha mawasiliano lakini kisipotumika vizuri kinaweza kusababisha migogoro katika mahusiano ya watu. Picha| Nukta Africa.
Ni kipimo cha uaminifu
Mkazi wa Dodoma, Witness Sosoma, amesema mahusiano ni kuaminiana hivyo mali ya mpenzi wako ni mali yako pia kwani kitu anachofanya mpenzi wako ni muhimu ukajua ili kuepusha mahusiano kuvunjika au kulinda moyo wako.
Sosoma amesema katika mahusiano ni ngumu kuaminiana kwani wakati undhani upo peke yako, kuna wenzio watatu wanakusindikiza.
“Siyo kwa wanaume tu hata baadhi ya wanawake nao siku hizi siyo waaminifu kwenye mahusiano. Unakuta ana mtu huku, kule na kule na wote hawajuani. Mtu kama huyo akikutana na mwanaume ambaye hana nia naye kimaisha, anakuwa anampotezea muda mbaba wa watu.
“Hivyo kuangalia simu na mawasiliano yake itakupa mwanga kama kuna matumaini au hakuna, kama kweli anakupenda au una msaidizi wako au wewe ndiyo unamsaidia mtu mwingine,” amesema Sosoma.
Wiki ijayo katika makala hizi za njiapanda, utapata kujua mtazamo wa wataalamu wa saikolojia, viongozi wa dini na wazazi kuhusu upekuaji wa simu miongoni mwa wapenzi.
Je kuna wakati sahihi wa kupekua simu ya mpenzi wako? Au muda wowote wewe sawa. Endelea kubaki na www.nukta.co.tz.