Kwanini siyo sahihi kutumia simu kwenye vituo vya mafuta
Sababu kuu ya maelekezo hayo ni kwa ajili kuwalinda watumiaji wa vituo hivyo dhidi ya hatari inayoweza kutokea ikiwemo mlipuko wa mafuta ambayo ni rahisi kushika moto.
- Simu inaweza kukuondolea umakini unapopata huduma ya mafuta.
- Inaweza kusababisha ajali kwa watumiaji wa vituo hivyo.
Dar es Salaam. Kama wewe ni mtumiaji wa huduma za vituo vya mfuta, utakuwa umekutana na maelekezo au alama inayokukataza kutumia simu unapokuwa kwenye eneo hilo.
Maelekezo hayo huambatana na mengine yanayomtaka dereva kuzima gari na kushusha abiria kabla hawajawekewa mafuta kwenye gari lake.
Sababu ya maelekezo hayo ni kwa ajili kuwalinda watumiaji wa vituo hivyo dhidi ya hatari inayoweza kutokea ikiwemo mlipuko wa mafuta ambayo ni rahisi kushika moto.
Lakini maelekezo hayo yamekuwa yakipuuzwa na watumiaji wa vituo vya mafuta kwa kujua au kutokujua.
Kwa nini unatakiwa kuzima simu ukiingia kwenye kituo cha mafuta?
1. Umakini wakati wa kupata huduma
Unapokuwa unatumia simu yako huku unaweka mafuta, huenda ukasababisha kutokuelewana baina yako na mhudumu kwani upo uwezekano wa kuzidisha mafuta au kutoa maagizo ambayo siyo uliyodhamiria.
Kwa mujibu wa tovuti ya Express, simu zinaweza kuondoa umakini siyo kwa mtu anayeendesha tu bali hata kwa raia ambao wanaweza kuwa wanapita kwenye maeneo ya vituo vya mafuta.
Ukosefu wa umakini huo unaweza kusababisha ajali kwa watu wanaotumia vituo hivyo.
Zinazohusiana
- Petroli, majiko ya gesi vyachangia kushusha mfumuko wa bei
- Petroli, mafuta ya taa vyachangia kushusha mfumuko wa bei
- Mfumuko wa bei washuka na kuvunja rekodi
2. Uhalisia wa teknolojia ya simu
Kila teknolojia au bidhaa huwa inakuja na maelekezo ya namna gani inafaa kutumika na ni wapi isitumike. Ni kama vile pombe na sigara zinavyokatazwa kutumika na watu wenye umri chini ya miaka 18. Ndivyo ilivyo simu.
Simu ya mkononi imetengenezwa huku ikielekezwa kutokufaa kutumika sehemu ambazo kuna uwezekano mkubwa wa milipuko (ikiwemo vituo vya mafuta).
“Japo uwezekano wa simu kusababisha ni mdogo, bidhaa hiyo siyo salama na haitakiwi kutumika kwenye maeneo hatarishi,” imesomeka sehemu ya taarifa ya Express.
Inaelezwa kuwa matumizi ya simu unapokuwa katika kituo cha mafuta yanaweza kusababisha mlipuko kutokana na mionzi inayotoka kwenye simu kukutana na hewa yenye petroli.
Hata hivyo, wadau mbalimbali wameendelea kukosoa imani hiyo kwani simu inazalisha mionzi isiyotosha kusababisha mlipuko.
Kwa mujibu wa tovuti ya Express na Blogthinkbig, simu inatoa mionzi ambayo ni sawa na wati 0.1 hadi mbili ambazo kiuhalisia wanasayansi wamesema haina uwezo wa kusababisha mlipuko wowote.