October 6, 2024

Kwanini vijana tusiogope kazi za kujitolea?

Kupitia kujitolea huenda ukafunguka milango ya fursa ambazo haujawahi kuzifikiria.

  • Kujitolea ni changamoto kwa wengi hasa pale inapokuwa ni kazi isiyomnufaisha mtu kifedha.
  • Hata hivyo, kuna faida nyingi za kujitolea ikiwemo kuongeza ujuzi na kuvumbua vipaji vyako vilivyojificha.
  • Pia, kupitia kujitolea utakutana na watu ambao watakufunza mengi usiyoyafahamau.

Dar es Salaam. Kabla  ya kuanza kuandika makala hii, ilinibidi nicheke kwa muda kidogo kwani ni kumbukumbu nyingi za kuchekesha zilizonirudia mara tu ya kuandika kichwa cha habari.

Kuanzia changamoto za usafiri, kunyeshewa mvua na kupiga “hamza kanuni” siku moja moja ilikuwa ni kawaida kwa siku zangu za mwanzo wakati nikianza kujitolea lakini hiyo ni stori ya siku nyingine.

Safari yangu ya kujitolea haikuwa ngumu na wala nyepesi. Lakini wakati nilipowaeleza watu kuwa ninajitolea, kwa kazi ambayo nilikuwa ninafanya walikuwa wakinishangaa na wakiona kuwa sina mipango ya maisha na kuwa muda wangu wa chuo sikuutumia vizuri.

Wengine walinishauri ni heri nikazane kuimba kwa sababu ni kipaji changu, wengine waliniambia ni bora nitafute mtaji nifanye biashara. Lakini fumbo ambalo wote hawakuweza kufumbua ni wapi ningelipata fedha ya kuyafanya hayo yote waliyonishauri.

Kuna rafiki yangu mmoja yeye alitia fora kwani alinIambia, “sasa si bora ukae tu nyumbani. Unaendaje kufanyia watu kazi ambayo haulipwi?.” Sikatai maneno yake kwa sababu yalinifikirisha lakini sikukata tamaa. Niliendelea kujitolea kwani niliamini kuwa “Mji wa Roma haukujengwa siku moja.”

Turudi kwenye reli kidogo… kwa nini vijana tusipuuze kazi za kujitolea? Kila mtu ana safari yake lakini hii ni safari yangu.


Kujitolea kutakukutanisha na watu wapya

Ni kweli ningeweza kukaa nyumbani na kuwasaidia wazazi kazi huku ni kila na kuishi bure lakini mawazo ya kuwa umri haurudi nyuma yalinifanya nitafute pa kuanzia kimaisha.

Nilianza kujitolea nikiwa sipewi chochote mwisho wa mwezi. Ilinilazimu kuendelea kumpigia baba yangu simu za kumuomba pesa ambayo ingenisaidia katika nauli na chakula niwapo ofisini licha ya kuwa nilikuwa nimehitimu masomo yangu ya chuo kikuu. 

Kwa siku ambazo baba aliniambia kuwa “yupo maweni”, niliwapigia ndugu zangu wakiwemo kaka zangu na dada zangu. Kuna siku zingine wote waliniambia kuwa mifuko yao imetoboka na ndio siku hizo ambazo umbali wa Makumbusho na Mwenge (jijini Dar es Salaam) ulikuwa ni kama hatua moja tu.

Nilikua mgeni na sipendi kuomba hela kwa mtu yeyote nje ya ndugu zangu. Hivyo kiburi changu sikuweza kukimeza. Nilipiga moyo konde na kuendelea na maisha.

Ndani ya muda mfupi, nilipata marafiki ambao wamekua msaada mkubwa katika maisha yangu. Wapo wabunifu wa picha, wapiga picha, wahasibu, mameneja, wakurugenzi na wamesimama na mimi kwa muda sasa huku baadhi yao wakiwa ni wateja wangu wa biashara ya  juisi.

Ndani ya muda mfupi, utapata marafiki wapya ambao huenda wakawa ndio “connection” yako hapo mbeleni. Picha| CIO.

Utagundua vipaji vilivyojificha

Kipaji kikubwa ambacho kilionekana na watu wengi ilikuwa ni kuimba lakini kupitia kujitolea, nimejifunza kumbe nina kipaji cha kusimamia matukio na kuongea mbele za watu. 

Nilikugundua nina hiyo talanta wakati natimiza majukumu mbalimbali yakiwemo ya kuongoza semina na kufanya mawasilisho na nimepokea maoni mazuri baada ya kazi hizo.

Nisingeliyafahamu hayo kama ningelikuwa nimekaa tu nyumbani.

Pia, kupitia kujitolea, nimekutana na watu walionisaidia kujielewa zaidi kitaaluma na kunifua katika uandishi wa habari, muziki na mengine mengi.


Utapata fursa zingine

Wakati nikijitolea, nimekutana na watu wengi katika harakati za kila siku. Wapo ambao waliona vitu ninavyovifanya lakini hakuniambia hapo hapo kuwa wamefurahishwa na ninachofanya ila tu siku kadhaa mbele nilipokea simu iliyoniunganisha na fursa ya kutosha kunipatia ugali wa siku mbili tatu.

Pia, wapo ambao hawakufurahishwa na nikifanyacho lakini walinipatia mawazo yao ya kuwa bora katika nikifanyacho.

Wapo walionishauri nishibishe CV yangu, wapo walionishauri nijifue katika uandishi wangu, wapo walionishauri nivae vizuri na wengine wakinishauri kuwa na ujuzi mzuri katika mawasiliano. Ushauri na mawazo yao yameendelea kunijenga kila siku.

Narudia tena, nisingeyapata hayo kama ningekaa nyumbani.

Ni sehemu ya wewe kupata ujuzi na uzoefu

Mara nyingi pale matangazo ya kazi yanapotoka yanahitaji uwe umefanya kazi hiyo walau kwa mwaka mmoja, miwili na kadhalika.

Hauwezi kupata uzoefu huo endapo hautapata eneo la kukupatia ujuzi huo. Kupitia kujitolea, unaweza kuongeza uzoefu na kupata ujuzi unaohitajika kupata ajira zingine zitakazokuja mbele.

Pia kupitia ujuzi ambao utaupata wakati unajitolea, huenda ukakusaidia kuanzisha biashara yako na hivyo kuachana na kutegemea ajira kama chanzo cha kujikwamua kiuchumi.


Soma zaidi:


Ni njia ya kufikia malengo yako

Endapo una malengo ya kuwa bora katika kitu fulani, ni muhimu kujifunza kutoka kwa watu walio na ubora wa fani unayotaka kuifanya.

Mfano, kama wewe unataka kuwa mjasiriamali mzuri, muhimu ujifunze kutoka kwa wajasiriamali waliofanikiwa. Unataka kuwa mcheza mpira mzuri, ni muhimu kujifua kupitia wacheza mpira waliofanikiwa na hivyo ndivyo unaweza kufikia ubora unaoutazamia.

Malengo yangu yalikuwa niwe mwandishi bora wa habari. Kupitia kujitolea, nimekutana na waandishi bora wa habari za kuchapishwa na kwa kipindi kirefu nimejifunza mambo mengi na kuwa bora.

Taratibu, nuru ya malengo yangu inaanza kuonekana. 

Mbali na hayo yote, kujitolea kumenifunza nidhamu ya pesa, nidhamu ya maisha na kunipunguzia “mihemko ya kimaisha” niliyokuwa nayo wakati namaliza elimu yangu ya chuo kikuu. 

Huwezi amini nilipanga kununua walau kiwanja mwaka wangu wa kwanza wa ajira lakini sikuumaliza mwaka huo nikiwa na hata baiskeli. 

Hadi siku nyingine, ni wako mtiifu @Rodjazz