November 24, 2024

Kwanini vijijini wanaongoza matumizi ya tumbaku Tanzania?

Asilimia 7 ya wakazi wa vijijini wanatumia bidhaa za tumbaku ikilinganishwa na asilimia 6.3 ya wakazi wa mjini.

  • Asilimia 7 ya wakazi wa vijijini wanatumia bidhaa za tumbaku ikilinganishwa na asilimia 6.3 ya wakazi wa mjini.
  • Wanawake wa vijijini hutumia tumbaku mara mbili zaidi ya wale wa mijini. 
  • Urahisi wa upatikanaji wa tumbaku ndiyo huwafanya wakazi wa vijijini kuwa vinara wa matumizi wa bidhaa hizo. 

Dar es Salaam. “Bila hii kitu siyo siku kabisa babu. Mimi natumia tangu enzi na enzi,” amesema mzee Hamisi Ntibahezwa (78) ambaye ni mtumiaji wa Tumbaku.

Katika makala iliyopita tuliangazia Tumbaku inavyohatarisha maisha ya watu zaidi ya milioni 2 Tanzania. Leo tunaendelea tena safari ya kufahamu  juu ya uhalisia wa matumizi ya bidhaa hiyo nchini Tanzania.

Kila asubuhi, Mzee Ntibahezwa mkazi wa Kasulu mkoani Kigoma huamka na kukaa nje ya nyumba na hapo huchukua kijifuko chenye tumbaku iliyokaushwa na kisha kiufundi huichambua na kutoa visivyofaa kwenye bidhaa hiyo kabla ya kuisokota na kuivuta. 

Mzee huyo ni miongoni mwa wakazi wa vijijini wanaotumia kwa kiwango kikubwa tumbaku. Tumbaku hiyo hutumika kwa kuvuta kama sigara au kuinusa puani ili “kupata mzuka”. 

“Nimeanza kuvuta tumbaku hata kabla hujazaliwa,” mzee Nibahezwa ameiambia Nukta (www.nukta.co.tz) na kusema hakumbuki muda ambao amekuwa akitumia bidhaa za tumbaku.

“Tungu tupo wadogo tulikuwa tunavuta hata kwa kuibia. Baba yetu alikuwa mvutaji na yeye na ilikuwa kawaida. Ni kama ilikuwa lazima kwa mwanaume kuvuta,” ameelezea Ntibahezwa.

Ripoti ya Utafiti wa Tumbaku kwa Watu Wazima Duniani (GATS) wa mwaka 2018 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Shirika la Afya Duniani (WHO) na Ofisi Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanziabar (OCGS) inaeleza kuwa watu saba kati ya 100 au asilimia 7 ya wakazi wa vijijini wanatumia bidhaa za tumbaku.

Wanaotumia bidhaa hizo vijijini ni wengi ukilinganisha na vijijini ambao ni asilimia 6.3.

Kila jinsia inayoishi vijijini inaongoza kwa matumizi ya bidhaa hiyo inayoelezwa na wataalamu kuwa ni hatari kwa afya za binadamu kutokana na kuchochea magonjwa hatarishi kama saratani. 

Kwanini wakazi wa vijijini wanatumia zaidi tumbaku kuliko wale mijini?

Mtaalam wa afya kutoka Hospitali ya Cardinal Rugambwa iliyopo Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam Dk Hans Olomi amesema hali hiyo inasababishwa na watu wa vijijini kuwa karibu zaidi na zao hilo.

Dk Olomi anabainisha kuwa tofauti na wenzao wa mijini wanaotumia bidhaa za tumbaku zilizochakatwa viwandani hususan sigara, wenzao wa wijijini hutumia zao hilo kwa namna nyingi tofauti ikiwemo kuvuta na kunusa. 


Zinazohusiana


Nchini Tanzania tumbaku hulimwa zaidi katika mikoa ya Songea, Tabora, Iringa, Mara, Mbeya na Katavi. 

Kwa mujibu wa Bodi ya Tumbaku Tanzania (TTB), mwaka 2017/18, kituo cha uzalishaji wa tumbaku cha Chunya mkoani Mbeya ndiyo kiliongoza kwa uzalishaji wa zao hilo kwa wingi zaidi baada ya kuzalisha kilogramu milioni 10.065.. 

Uzalishaji huo  ni sawa na asilimia 19 ya uzalishaji wote uliofanyika mwaka huo nchini ambao ni kilogramu milioni 50.522. 

Hata hivyo, Mkoa wa Tabora ndiyo unaongoza kwa kilimo cha zao hilo huku ukiwa na vituo vinne vya uzalishaji wa zao hilo kikiweo kituo cha Kaliua, Sikonge, Tabora na Urambo.

“Ukaribu wa bidhaa hiyo unasababisha matumizi makubwa. Kwa vijijini tumbaku inachanganywa kwenye mboga, inavutwa kama sigara na pia wengine wanakula,” amesema Dk Olomi.

Kwa upande wa wanawake kutumia tumbaku zaidi, mzee Ntibahezwa amesema kwa ufahamu wake ni nadra kwa wanawake wa vijijini kutumia sigara lakini anafahamu baadhi wanaochanganya bidhaa hiyo kwenye mboga huku vikongwe wakiitumia kama ugoro ambao huvuta au kuwekwa mdomoni “kuongeza stimu”. 

“Ukienda sokoni, utakuta wanawake mabibi wanauza ugoro kwenye makopo. Hata ukiwa na mia unapimiwa.” amesema Ntibahezwa aliyefanya mazungumzo na Nukta akiwa kwenye matembezi yake Jijini Dar es Salaam.

Urahisi wa upatikanaji wa tumbaku ndiyo huwafanya watumiaji wa bidhaa hizo kuwa wengi vijijini kuliko mjini. Picha|Mtandao. 

Utafiti wa GATS umeainisha kuwa asilimia 6.5 ya Watanzania wanavuta aina yeyote ya sigara. Asilimia 5.2 huvuta zilizotengenezwa viwandani huku asilimia 2.7 wakitengeneza (kusokota) sigara wenyewe.

Hata hivyo, wakati wanafanya hivyo ni kama wanajichochea moto wao wenyewe kwani matumizi ya bidhaa hiyo ni chanzo cha magonjwa mbalimbali ikiwemo kansa, matatizo ya moyo, kiharusi, maradhi ya mapafu na kisukari.

Kwa mujibu wa Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia magonjwa (CDC), matumizi ya bidhaa za tumbaku huongeza uwezekano wa mtumiaji kupata magonjwa kama kifua kikuu (tuberculosis), magonjwa ya macho na changamoto za kinga ya mwili.

Madhara haya yanawaweka katika hatari zaidi akazi hao ambao katika maeneo yao kuna changamoto nyingi za uhaba wa huduma za afya.

Usikose kuungana nasi katika sehemu ya tatu ya makala haya kesho Julai 22, 2020, tukiangazia kwa undani tatizo la matumizi ya bidhaa za tumbaku na madhara yake kwa maisha ya Watanzania.