July 8, 2024

Lijue ghorofa la kwanza kujengwa Dar

Hadi sasa ghorofa hilo lililokuwa likitumika kuwakirimu wageni wa Sultan lipo katikati ya jiji na huend siyo watu wengi wanalifahamu.

  • Jengo hilo lilijengwa kwa malighafi zinazopatika maeneo ya baharini yakiwemo matumbawe na mikoko.
  • Hadi sasa ghorofa lililokuwa likitumika kuwakirimu wageni wa Sultan lipo katikati ya jiji.
  • Mtanzania kuingia kulitalii ni Sh3,000 tu.

Dar es Salaam. Tumeshuhudia Jiji la Dar es Salaam likikua kwa kasi tangu Tanzania ipate uhuru miaka 58 iliyopita huku likizungukwa na majengo marefu ya kisasa yanayomea kama uyoga kila siku.

Jiji hilo, lenye wakazi zaidi ya milioni tano, ndiyo linaloongoza kwa kuwa na jengo lefu zaidi Afrika Mashariki na Kati la PSPF Twin Towers lenye urefu wa mita 147 sawa na ghorofa maarufu la 88 on field liliopo jijini Durban, Afrika Kusini.

Lakini umewahi kujiuliza ghorofa la kwanza Dar es Salaam lipo wapi, lilijengwa lini na linamuonekano gani?

Swali jingine ambalo huenda wengi wakauliza, je katika kipindi ambacho majengo ya kale yanabolewa kwa kasi, ghorofa la kwanza kujengwa jijini hapo lipo mpaka sasa?

Hata hivyo, ukweli ni kwamba baadhi huenda hupita kila siku katika ghorofa hilo Bongo iwe kwa gari au kwa miguu.

Kando kando ya makutano ya barabara ya Sokoine na barabara ya Morogoro karibu na Chuo Cha Mabaharia Tanzania (DMI) lipo jengo jeupe lenye muundo wa kizamani. 

Mlango wake wa mbao wenye nakshi za kizamani unaonekana ‘kuchafua’ hadhi ya mitaa iliyopo kando kando ya Barabara ya Sokoine ambayo ni maarufu kuingilia katikati ya jiji kutoka maeneo ya Mbagala, Kariakoo na kwingine.

Jengo hilo ndiyo ghorofa la kwanza kujengwa Dar es Salaam ambalo kwa sasa si chochote kabisa mbele vya vilele kama TPA HQ Tower, PSPF Business Twin Towers au LAPF II Millenium Tower lilopo Kijitonyama.

Tofauti na majina maghorofa mengi ya kisasa yanayopewa majina ya kizungu, ghorofa hilo la kipekee kwa wakati huo lilipewa jina rahisi tu la ‘Old Boma.

Msimamizi wa  Kituo cha Urithi wa Ubunifu Majengo jijini Dar es salaam (DARCH) kilichopo chini ya Hamalshauri ya Jiji la Dar es salaam, Gwamaka Mwakalinga ameiambia Nukta kuwa ghorofa hilo lilijengwa miaka 159 iliyopita na Sultani Majid bin Said wa  Zanzibar karibu na Ikulu yake ambayo ilishapotea kwenye ramani baada ya kubomolewa.

Jengo la Old Boma |Picha kwa hisani ya mtandao

Guest house?

Jengo hilo la ghorofa moja na vyumba nane lilijengwa kwa dhumuni  kubwa la kuwakarimu na kuwapa malazi wageni wa Sultani. Sultani anayezungumziwa hapa ni yule wa miaka takriban 200 iliyopita…kwa kifupi achana na kumfikiria yule wa kwenye tamthilia.

Lakini baada ya utawala wa Kisultani kuondoka, jengo hilo ambalo kwa sasa ni kivutio cha utalii,  lilichukuliwa na Wajerumani ambao walilizungushia ukuta kama ngome yao wakati huo kujikinga na mashambulizi ya vita. Ukuta huo upo mpaka sasa mtaji ni nauli ya daladala kujionea.

‘’Wajerumani walipokuja baada ya mgawanyo wa Bara la Afrika mwaka 1886 na baada ya kukutana na ‘resistance’ (upinzani) kubwa kutoka kwa Waarabu wakati wa vita ndipo walipoamua kujenga ukuta wa nyumba hiyo na hapo ndipo jina la Old Boma lilipoanza,” anasema Mwakalinga.

Ujenzi wa jengo hilo ni wa tofauti kidogo na majengo ambayo wengi tumezoea kwa kuwa sehemu kubwa limejengwa na malighafi zinazopatikana katika maeneo ya bahari.

“Old Boma imejengwa kwa kutumia matumbawe (Coral reef), miti ya mangrove pamoja na chokaa tu,” anasema.

Kati ya mejengo lukuki aliyojenga Sultani Majid bin Said aliyeingia jijini kutoka Zanzibar katika eneo hilo la Mzizima, ni matano tu alifanikiwa kukamilisha ujenzi wake kabla mauti hayajamkuta mwaka 1870, ghorofa la kwanza Dar likiwemo.

Majengo mengine yalisalia  ni ‘Custom House’ ambalo kwa sasa lipo ndani ya Bandari ya Dar es Salaam na ‘Antiman House’ lililopo mkabala na Kituo cha mabasi ya yaendayo haraka cha Posta ya Zamani.

Mwaka 2014 DARCH ilifanikiwa kufanya ukarabati mkubwa ghorofa hilo la kwanza ili angalau kulirudisha kwenye sura yake ya zamani.

Hata hivyo, ugumu ulikuwa ni kwenye malighafi ambazo zilitumika kujenga jengo hilo.

Ili kuendana angalau na uhalisia, DARCH ambayo ni taasisi ya wasanifu majengo jijini Dar es Salaa, walitumia malighafi nyingine za kisasa kuhakikisha halipotezi muonekano wake.  

Ukarabati wa jengo hilo na mradi mzima wa kuliweka katika ubora wa sasa awali ulifanywa kwa ufadhili kutoka Umoja wa Ulaya (EU) lakini baada ya ufadhili huo kuisha DARCH wanapambana katika kuuendeleza.

Hata hivyo, Mwakalinga hakuweka bayana gharama zilizotumika katika kulikarabati jengo hilo.

Kwa sasa Old Boma linatumika kama ofisi za DARCH na pia ni sehemu ya maonyesho mbalimbali ya kitamaduni.

Mwakalinga amesema ingawa kuna historia kubwa katika eneo hilo lakini bado mwamko wa Watanzania kuja kujifunza historia ni mdogo sana.

“Kwa mwaka tunaweza pata watembeleaji wa kitanzania wapatao 30 tu ukilinganisha na wageni kutoka nje ambao ni takribani 600 wengi wao wakiwa kutoka nchi ya  Ujerumani,” amesema.

Gharama za kutembelea

Lakini je, unawezaje kutembelea jengo hilo?

Kwa Mtanzania kutembelea ghorofa hilo la kwanza anatakiwa kulipia Sh3,000 na wanafunzi Sh1,000 huku wageni  kutoka nje ya nchi wakitakiwa kulipiwa Sh5,000.

Moja ya jitihada wanazofanya ni kutembelea shule mbalimbali na kuhamasisha kuja kujionea historia hiyo.

Sehemu ya juu ya gorofa la Old Boma ambapo sasa ni sehemu ya maonyesho. Picha|Daniel Mwingira.