Lindi kununua viazi mviringo kwa bei ya juu zaidi Tanzania
Wakazi wa Mkoa wa Lindi leo Mei 8, 2020 wananunua gunia la kilo 100 la viazi mviringo takriban mara tatu ya wenzao wa Mkoa wa Rukwa, jambo linalowafaidisha zaidi wafanyabiashara na wakulima wa zao hilo.
- Wafanyabiashara wanauza gunia la kilo 100 takriban mara tatu ya wenzao wa Rukwa ya Sh45,000.
- Bei inayotumika leo Lindi imeongezeka kwa Sh10,000 ikilinganishwa na Sh120,000 iliyotumika Jumatatu.
Dar es Salaam. Wakazi wa Mkoa wa Lindi leo Mei 8, 2020 wananunua gunia la kilo 100 la viazi mviringo takriban mara tatu ya wenzao wa Mkoa wa Rukwa, jambo linalowafaidisha zaidi wafanyabiashara na wakulima wa zao hilo.
Viazi mviringo ni miongoni mwa mazao makuu ya chakula yanayolimwa Tanzania. Mengine ni maharage, mchele, mahindi na mtama.
Takwimu za Wizara ya Viwanda na Biashara kuhusu mazao makuu ya chakula zilizotolewa leo (Mei 8, 2020) zinaeleza kuwa gunia hilo linauzwa kwa Sh130,000 mkoani Lindi huku wenzao wa Rukwa wakinunua kwa Sh45,000.
Hiyo ni sawa na kusema wananchi wa Lindi wananunua viazi hivyo ambavyo ni maarufu kwa kutengeneza chipsi takriban mara tatu ikilinganishwa na wenzao wa Rukwa, jambo litakalowafaidisha wafanyabiashara na wakulima waliopeleka zao hilo mkoani humo.
Bei inayotumika leo mkoani Lindi ndiyo bei ya juu huku ya Rukwa ndiyo bei ya chini Tanzania bara.
Hata hivyo, bei inayotumika Rukwa haijabadilika ikilinganishwa na ile iliyorekodiwa Jumatatu Mei 4, 2020.
Wafanyabiashara wa lindi wanaouza viazi mviringo wataendelea kufurahia soko kwa sababu bei inayotumika leo imeongezeka kwa Sh10,000 ikilinganishwa na Sh120,000 iliyotumika jumatatu.
Hata hivyo, bei hiyo ni maumivu kwa walaji wa aina hiyo ya chakula katika mkoa huo wa Kusini mwa Tanzania.