Maajabu ya visiwa 11 ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Rubondo
Utajiri mkubwa ni uwepo wa misitu ya asili ambayo inatoa makazi kwa wanyamapori wa aina mbalimbali wakiwemo Tembo, Twiga, Mbega mweusi na mweupe.
- Ipo Kusini Magharibi mwa Ziwa Victoria mkoani Geita imezungukwa na visiwa vidogo 11.
- Utajiri mkubwa ni uwepo wa misitu ya asili ambayo inatoa makazi kwa wanyamapori wa aina mbalimbali wakiwemo Tembo, Twiga, Mbega mweusi na mweupe.
- Ni miongoni mwa maeneo machache yaliyofanikiwa kuhifadhiwa kwa muda mrefu bila kupoteza asili yake.
Ukifika Rubondo utashuhudia wanyama wengi wakiwemo viboko na mamba katika fukwe za Ziwa Victoria. Picha| Manna Expedition and Safari Ltd.
Dar es Salaam. Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo ipo Kusini Magharibi mwa Ziwa Victoria mkoani Geita. Mwaka 1965 kisiwa hicho kilipewa hadhi ya kuwa Pori la Akiba ambapo zoezi la kupandikiza wanyama lilianza katika maeneo yaliyoko nje ya kisiwa na mwaka 1977 ilipewa hadhi ya kuwa Hifadhi ya Taifa.
Kwa mujibu wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Rubondo ina ukubwa wa kilomita za mraba 456 ambapo kilomita za mraba 220 ni eneo lenye maji wakati kilomita 237 ni nchi kavu.
Ni eneo zuri kwa ajili ya watalii wa ndani na nje kutokana na mandhari nzuri iliyosheheni ndege wa aina mbalimbali, samaki aina ya Tilapia kutoka mto Nile. Kwa muda mrefu eneo hilo lilipo kwenye Ziwa Victoria ndiyo limeonekena kuhifidhaziwa vizuri ukilinganisha na maeneo mengine ambayo yanakumbwa na changamoto ya magugu maji.
Upekee wa Hifadhi hiyo ni uwepo wa visiwa vingine 11 ambavyo ni Izilambuba, Kalera, Rubiso, Makozi, Irumo, Mizo, Chambuzi, Chitebe, Manyila, Chitende na Nyamitundu ambavyo vinapambwa na vivutio mbalimbali.
Utajiri mkubwa Hifadhi ya Taifa ya Rubondo ni uwepo wa misitu ya asili ambayo inatoa makazi kwa wanyamapori wa aina mbalimbali wakiwemo Tembo, Twiga, Mbega mweusi na mweupe, Suni na ndege mbalimbali. Pia ni moja ya maeneo muhimu ya mazalia ya ndege wahamao pamoja na jamii ya samaki ya Tilapia.
Zinazohusiana:
- Kitulo ‘Bustani ya Mungu’ fahari ya Nyanda za Juu Kusini.
- Ijue milima 10 mirefu zaidi Tanzania.
- Ndani ya Ifisi: Hifadhi ya wanyamapori inayotoa pumziko kwa wakazi wa Mbeya.
Muda mzuri wa kutembelea ni kuanzia mwezi Juni mpaka Septemba na wakati wa mvua ni Novemba hadi Machi mbapo maua ya porini yanaaza kuchanua. Pia kwa watalii wanaopendelea ndege basi mwezi Disemba hadi Februari ni wakati muafaka kwasababu katika kipindi hicho ndege wengi wanahama kutoka maeneo mbalimbali ya hifadhi hiyo.
Ukiwa ndani ya hifadhi mambo haya yatakuhusu
Ndani ya hifadhi ya Rubondo kuna shughuli tofauti za utalii ikiwemo uvuvi wa burudani (sport fishing) ikiwa ndio shughuli kuu, sambamba na kujionea maeneo ya makazi ya ndege, mamba na fukwe za Ziwa Victoria kwa kutumia boti.
Mtalii anaweza kufanya utalii wa kutembea kwa miguu kwa muda wa hadi masaa 7 huku macho yake yakishuhudia wanyama wengine kama Mamba, nguchiro wa makazi ya ardhi oevu, panya walao miwa, saruya au digidigi, ngiri, kuro, tumbili, kindi, twiga, viboko, Tembo, nguruwe mwitu, sokwe mtu, nyati au mbogo pamoja na wanyamapori wengineo jamii ya nyani. Pia uwanda mpana wa misitu yenye kutoa kivuli hasa wakati wa jua kali.
Furaha yako itahitimishwa na maeneo matatu ya utamaduni ndani ya hifadhi hiyo ambayo ni Maji Matakatifu, Ntungamirwe, and Alutare/altare.
Maji matakatifu ni eneo la kihistoria ambalo jamii ya Wazinza ambao walikaa Rubondo kabla ya kuwa hifadhi ya Taifa walikuwa wanatumia eneo hilo kama kuwatakatisha wanawake na wanaume ambao hawakuwa na watoto ili waweze kupata watoto.
Ntungamirwe ni pango la kihistoria la kiimani kwa Wazinza ambao lipo karibu na Kageye, lilitumika kwa ajili ya kutolea kafara. Sehemu ya tatu ya kihistoria ni ambayo ni muhimu ni Altare ambapo watu wa jamii ya Banyarubondo walijificha huko katika pango la Karobhela waliposhambuliwa na maadui.