November 24, 2024

Maandamano ya kwenda Ikulu yalivyozima ndoto za vijana 854 wa JKT Tanzania

Ni kati ya 2,400 waliokuwa wameahidiwa ajira jeshini na Hayati Rais Magufuli baada ya kushiriki katika ujenzi wa Ikulu ya Chamwino, Dodoma.

  • Ni kati ya 2,400 waliokuwa wameahidiwa ajira jeshini na Hayati Rais Magufuli baada ya kushiriki katika ujenzi wa Ikulu ya Chamwino, Dodoma.
  • Jenerali Venance Mabeyo asema wamesitishiwa mikataba yao na kurejeshwa makwao.

Dar es Salaam. Ndoto za vijana 854 wa kujitolea katika Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) zimezimika baada ya kufurushwa kutokana na kufanya maandamano ya kudai ajira ya kwenda Ikulu ili kumuona Rais Samia Suluhu.

Vijana hao wameaga JKT hivyo kupishana rasmi na fursa ya ahadi ya ajira waliokuwa wameahidiwa mwaka jana na Hayati Rais John Magufuli ya kuandikishwa jeshini baada ya kushiriki katika ujenzi wa Ikulu mpya ya Chamwino mkoani Dodoma.

“Wakishamaliza hili jengo usiwapeleke mahali popote bali wapeleke jeshini wakaajiriwe wawe wanajeshi wote. Mkimaliza katika kipindi cha miezi miwili…muanze kuwaandaa, hawa ninawapa ajira moja kwa moja. Walichokifanya ni kikubwa sana,” alisema Hayati Magufuli mapema Desemba mwaka jana.

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Venance Mabeyo alimweleza Rais Samia jana Aprili 17 kuwa Aprili 8 mwaka huu vijana hao 854 ambao ni sehemu ya vijana 2,400 waliokuwa wameahidiwa ajira waliamua kugoma, kukataa kufanya kazi eneo jingine na kuandamana kwenda Ikulu kumuona Rais wakishinikiza kuandikishwa jeshi.

Katika taarifa ya video iliyotolewa na Kuruguenzi ya Mawasiliano Ikulu, Jenerali Mabeyo amesema hata Mkuu wa JKT Meja Jenerali Charles Mbuge alipowasihi kusitisha mgomo huo na kutoandamana, hawakumsikiliza.

Taarifa ya Ikulu inaeleza kuwa jeshi lilikuwa limewapunguza vijana hao katika kazi ya ujenzi wa Ikulu Chamwino baada ya shughuli hizo kupungua na kuwataka kwenda kufanya kazi katika maeneo mengine lakini walikataa kwa madai kuwa wangekosa kuandikishwa jeshini.

“Kitendo hiki hakikubaliki. Kugoma au kuandamana jeshini ni kosa la uasi. Wangekuwa ni askari wangefikishwa mahakamani na adhabu zake zipo wazi, adhabu ya juu kabisa ya uasi na adhabu ya chini kabisa ya uasi,” amesema Mabeyo na kuongeza kuwa JKT wamesitisha mikataba yao kuanzia Aprili 12 na tayari wamesharejeshwa makwao.

Mabeyo amesema JKT siyo sehemu ya ajira bali ni kwa ajili ya kupatiwa malezi kwa vijana na kujifunza stadi za kazi na kwamba kutokana na yalitokea wanatafakari utaratibu mpya utakaowasaidia kupata vijana wa kujitolea.

“Tunasikitika vijana wale walifanya kazi kubwa na walikaa Jeshi la Kujenga Taifa kwa takriban miaka mitatu lakini nafasi hiyo wameiaharibu,” amesema Jenerali Mabeyo.

Haya ni moja ya matukio nadra kwa vijana wa JKT kugomea maelekezo ya viongozi wao na taarifa hiyo ya Jenerali Mabeyo imeibua mijadala mtandaoni huku baadhi wakisihi mamlaka akiwemo Rais Samia kuwasamehe.

Hata hivyo, baadhi wamesema kitendo walichofanya vijana hao si cha kizalendo na kinaonyesha hawakuwa tayari kulitumia Taifa kupitia vyombo vya ulinzi.