October 7, 2024

Mabadiliko ya teknolojia kuwarudisha viongozi wa Serikali vyuoni

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kutokana na mabadiliko ya teknolojia hakuna namna ya kukwepa kujifunza na kupata maarifa hasa kwa viongozi wa Serikali.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema unapokuwa kiongozi kuna baadhi ya mambo unatakiwa uyaache. Hata kama ulikuwa umezoea kushangilia mpira kwa kuvua shati, ukiwa kiongozi unaacha kuvua shati. Picha! Ofisi ya Waziri Mkuu.


  • Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kutokana na mabadiliko ya teknolojia hakuna namna ya kukwepa kujifunza na kupata maarifa hasa kwa viongozi wa Serikali.
  • Amesema Serikali itaangalia uwezekano ili viongozi wa ngazi mbalimbali wapate mafunzo ya uongozi na maadili kwenye Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kama sehemu ya kurejesha maadili kwa viongozi.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kutokana na mabadiliko ya teknolojia hakuna namna ya kukwepa kujifunza na kupata maarifa hasa kwa viongozi wa Serikali wanaoshughulika na matatizo ya wananchi.

Kutokana na mabadiliko hayo, amesema Serikali itaangalia uwezekano ili viongozi wa ngazi mbalimbali wapate mafunzo ya uongozi na maadili kwenye Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kama sehemu ya kurejesha maadili kwa viongozi.

Majaliwa ametoa kauli hiyo leo (Aprili 11, 2019) wakati akifungua kongamano la Kumbukizi ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere lililofanyika katika chuo hicho, Kigamboni, jijini Dar es Salaam ambapo amebainisha kuwa Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Manispaa, Miji na wakuu wa taasisi mbalimbali za umma wanastahili kupelekwa kwenye chuo hicho ili wapigwe msasa juu ya maadili ya uongozi.

“Kwa viongozi wetu wote kuanzia Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurgenzi wa Halmashauri na Wakuu wa taasisi mbalimbali za umma ambao wanatakiwa kujengewa msingi imara wa namna ya kuongoza, hapa ndiyo mahali pake. Nalichukua ombi lenu ili tuwape fursa ya wiki moja au mbili waje hapa wajifunze miiko ya uongozi.”

“Wanatakiwa waje kupata namna ya kuwa kiongozi, miiko ya namna kiongozi anavyotakiwa awe. Unapokuwa kiongozi unatakiwa ujue mambo gani unapaswa uyaache. Unapokuwa kiongozi kuna baadhi ya mambo unatakiwa uyaache. Hata kama ulikuwa umezoea kushangilia mpira kwa kuvua shati, ukiwa kiongozi unaacha kuvua shati,” amesema Majaliwa.


Soma zaidi: 


Amesema kutokana na mabadiliko ya kiteknolojia hakuna namna ya kukwepa kujifunza na kupata maarifa mapya huku akinukuu maneno ya Baba wa Taifa, Mwl. Julius K. Nyerere ambaye aliwahi kusema:”Watu walio hatari sana ni wale ambao wanafikiri kuwa wanajua kila kitu, wala hawana haja kujifunza zaidi. Hii ni tabia mbaya ambayo huzuia kabisa maendeleo.”

Waziri Mkuu alikuwa akijibu hoja iliyotolewa na Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Shadrack Mwakalila kwamba mwitikio wa viongozi na watendaji wakuu wa Serikali kushiriki katika mafunzo ya uongozi, maadili na utawala bora umekuwa hafifu licha ya jitihada kubwa za kutangaza mafunzo haya kupitia njia mbalimbali.

Kongamano hilo lilihudhuriwa na balozi wa Namibia hapa nchini Theresia Samaria, balozi wa Msumbiji hapa nchini Monica Patricio Clemente, Waziri Mkuu Mstaafu Jaji Joseph Sinde Warioba ambaye alikuwa mwenyekiti wa kongamano hilo. 

Wengine ni mawaziri wastaafu wa Serikali ya awamu ya kwanza, Mzee Ibrahim Kaduma na mama Thabitha Siwale.