Mabadiliko ya uongozi kuipaisha sekta bima Tanzania?
Rais Magufuli amemteua Dk Elirehema Doriye kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Bima la Taifa (NIC), amechukua nafasi ya Samwel Kamanga ambaye uteuzi wake umetenguliwa.
- Rais Magufuli amemteua Dk Elirehema Doriye kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Bima la Taifa (NIC), amechukua nafasi ya Samwel Kamanga ambaye uteuzi wake umetenguliwa.
- Kamanga ameiongoza NIC tangu Oktoba 2016.
- Wahadhiri wa IFM waendelea kupata fursa katika sekta ya bima.
Dar es Salaam. Huenda sekta ya bima Tanzania ikaongeza ufanisi wa kutoa huduma na kuchangia katika ukuaji wa uchumi, kutokana na mabadiliko ya uongozi wa ngazi ya juu wa taasisi mbili za bima yaliyofanyika hivi karibuni.
Ni jana (Julai 29, 2019), Rais John Magufuli amemteua Dk Elirehema Doriye kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Bima la Taifa (NIC), amechukua nafasi ya Samwel Kamanga ambaye uteuzi wake umetenguliwa.
Kabla ya uteuzi huo Dk Doriye alikuwa Mhadhiri wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM).
“Uteuzi wa Dk Doriye unaanza leo Julai 29, 2019,” inaeleza taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa.
Kutenguliwa kwa Kamanga kunahitimisha safari ya zaidi ya miaka miwili na nusu ya uongozi wake NIC tangu alipoteuliwa na Rais Magufuli kuiongoza taasisi hiyo Oktoba 27, 2016.
Soma zaidi:
Mabadiliko hayo yamekuja ikiwa umepita zaidi ya mwezi mmoja tangu Rais Magufuli afanye mabadiliko mengine ya uongozi katika Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA).
Juni 25 mwaka huu, alimfuta kazi Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Dk Bhagayo Saqware na kumteua Mhadhiri wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Dk Mussa Juma kuchukua nafasi hiyo ya kuiongoza taasisi nyeti katika sekta ya fedha na bima nchini.
Kutenguliwa kwa Dk Saqware kulihitimisha safari ya miaka miwili na nusu ya uongozi wake TIRA baada ya kuteuliwa na Rais kuiongoza taasisi hiyo Februari 2017.
Huenda mabadiliko hayo yakaisaidia sekta ya bima kuongeza ufanisi katika shughuli zake, ikizingatiwa kuwa walioteuliwa yaani Dk Juma na Dk Doriye wanatoka katika taasisi muhimu ya elimu ya juu ya IFM ambayo imekuwa ikitoa wahitimu hodari na mahiri kila mwaka ambao wanahitajika kulitumikia Taifa.
Kwa mujibu wa ripoti ya robo ya kwanza ya mwaka 2019 ya ukuaji wa pato halisi la Taifa (Quarterly Gross Domestic Product (QGDP)) iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), ukuaji wa sekta fedha pamoja na bima umefikia asilimia 5.6 katika robo ya kwanza ya mwaka huu ukilinganisha na asilimia 2.9 katika kipindi kama hicho 2018.
Miongoni mwa sababu za ukuaji huo ni kuongezeka kwa huduma zinazotolewa na makampuni ya bima nchini.