Mabilionea kulijenga upya kanisa la Notre Dame Ufaransa
Jengo hilo la historia lina miaka 850 lililoungua jana sehemu ya paa na mnara wakati linafanyiwa ukarabati limekuwa alama ya Ufaransa na kivutio kikubwa cha watalii wanaotembelea nchi hiyo.
Kanisa kongwe la Notre Dame la mjini Paris, Ufaransa baada ya sehemu ya kanisa hilo kuteketea kwa moto na kuharibika. Picha|Mtandao.
- Mabilionea na wafadhili binafsi wameahidi kutoa fedha zitakazosaidia kulijenga upya kanisa kongwe la Notre Dame la Jijini Paris, Ufaransa baada ya sehemu ya kanisa hilo kuteketea kwa moto na kuharibika.
- Bilionea Bernard Arnault anayemiliki kampuni ya LVMH Group ameahidi kutoa Dola za Marekani 226 milioni (Sh522.7 bilioni).
- Jengo hilo la historia lina miaka 850 ambalo lilikuwa linafanyiwa ukarabati limekuwa alama ya Ufaransa na kivutio kikubwa kwa watalii wanaotembelea nchi hiyo.
Mabilionea na wafadhili binafsi wameahidi kutoa fedha zitakazosaidia kulijenga upya kanisa kongwe la Notre Dame la mjini Paris, Ufaransa baada ya sehemu ya kanisa hilo kuteketea kwa moto na kuharibika jana usiku.
Hatua hiyo inakuja baada ya Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron jana (Aprili 15, 2019) kutangaza kuwa kwa uzaidizi wa kimataifa watalijenga upya kanisa hilo lililookolewa na maafisa wa zima moto lakini paa na mnara wa jengo hilo vimeteketea kabisa.
Jengo hilo la historia lina miaka 850 lilloungua wakati linafanyiwa ukarabati limekuwa alama kuu ya Ufaransa na kivutio kikubwa kwa watalii wanaotembelea nchi hiyo.
Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Ufaransa la AFP, Bilionea Bernard Arnault anayemiliki kampuni ya LVMH Group ameahidi kutoa Dola za Marekani 226 milioni (Sh522.7 bilioni) ili kusaidia juhudi za kulijenga upya jengo hilo ambalo lina historia ya muda mrefu.
LVMH Group ambayo inahusika na biashara ya bidhaa za anasa (luxury goods) imesema itasaidia kutoa ushauri wa kitaalam na kuhamasisha watu wengi kujitoa ili kukamilisha kazi hiyo kwa wakati.
Ahadi iliyotolewa na Bilionea Arnault imekuja baada ya kampuni ya mitindo na ubunifu ya Kering iliyoasisiwa na bilionea wa Ufaransa, Francois Pinault kuahidi kutoa Euro 100 milioni (takriban Sh261 bilioni) kusaidia juhudi za kulijenga upya kanisa hilo.
Soma zaidi:
- Shirika la ndege la Ethiopia limesitisha safari zote za ndege aina ya Boeing 737
- Tanzania yaangazi masoko 18 kukuza utalii duniani
Viongozi mbalimbali duniani wametuma salamu za pole kutokana ajali hiyo akiwemo Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ambaye amesema kanisa hilo ni ishara ya Ufaransa na utamaduni wa Ulaya.
Mapema leo, Meya wa Jiji la Paris, Anne Hidalgo amesema ofisi yake itatoa Euro 50 milioni na amezitaka jumuiya za kimataifa kuungana na ufaransa kutoa michango yao ili kulirejesha kanisa hilo katika hali yake ya awali.
Baadhi ya kampuni zinahusika kuhamasisha watu kutoa misaada ikiwemo ya French Heritage Foundation kupitia tovuti yake ya www.fondation-patrimoine.org imetoa wito kwa watu mbalimbali kutoa michango yao ili kuungana na wadau wa maendeleo walio tayari kutoa fedha zao kwa ajili ya ukarabati huo.
Katika mahojiano jana, Mchambuzi wa masuala ya historia kutoka Shirika la Utangazaji la BBC, Henri Astier amesema Notre-Dame linawakailisha Ufaransa likifuatiwa na mnara wa Eiffel Tower.
Ameeleza kuwa Notre-Dame limesimama wima juu ya mji wa Paris tangu miaka ya 1200. Mara ya mwisho kanisa hilo liliharibiwa ni wakati wa mageuzi ya Ufaransa na limenusurika vita kuu viwili vya dunia bila kuharibiwa.
Kanisa kongwe la Notre Dame la mjini Paris, Ufaransa kabla ya sehemu ya kanisa hilo kuteketea kwa moto na kuharibika. Picha|Mtandao.
UN nao waingilia kati
Kufuatia kuungua kwa Kanisa hilo Kuu Katoliki la kale, shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni, (Unesco) limetangaza kuwa tathmini ya uharibifu itaanza haraka iwezekanavyo.
Taarifa ya Unesco iliyotolewa mjini Paris na Mkurugenzi wake Mkuu, Audrey Azoulay inaeleza kuwa tathmini itafanywa na mamlaka husika ikiwemo za kitaifa na mitaa, wasimamizi wa eneo hilo na mamlaka za kanisa ili kuandaa mpango wa utekelezaji na kuepusha uharibifu zaidi wa eneo hilo na kuhifadhi vifaa halisi kadri iwezekanavyo.
Amesema Unesco kwa upande wake utasaidia mamlaka za Ufaransa katika ukarabati, ikizingatiwa kuwa mwaka 1991, kanisa hilo pamoja na maeneo mengine ya ukingo wa mto Seine mjini humo yalitangazwa kuwa maeneo ya urithi wa dunia yaliyoorodheshwa na shirika hilo.
Taarifa hiyo inabainisha kuwa kanisa hilo la kale lilijengwa kuanzia kuanzia mwaka 1163 hadi mwaka 1345 na moto wa jana Jumatatu umeteketeza mnara wake mkuu. Hata hivyo minara mingine miwili ya kanisa hilo iko salama