July 3, 2024

Macho na masikio kwa Rais Samia sherehe za mei mosi Tanzania

Mtarajio ya wafanyakazi ni kuona anatoa mwelekeo mpya wa utatuzi wa changamoto zao za muda mrefu ikiwemo nyongeza ya mishahara.

  • Mtarajio yao ni kuona anatoa mwelekeo mpya wa utatuzi wa changamoto zao za muda mrefu ikiwemo nyongeza ya mishahara.
  • Sherehe hizo zitafanyika jijini Mwanza na Rais Samia atakuwa mgeni rasmi.

Mwanza. Mkoa wa Mwanza utakuwa mwenyeji wa siku ya wafanyakazi ya Mei mosi mwaka huu huku macho na masikio yakielekezwa kwa mgeni rasmi katika sherehe hizo ambaye anatarajiwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan.

Hiyo itakuwa mara ya kwanza kwa Rais Samia kuhudhuria sherehe hizo tangu aapishwe kuwa Rais wa sita wa Tanzania Machi 19 mwaka huu akichukua nafasi ya Hayati John Magufuli. 

Macho na masikio ya wafanyakazi wa sekta binafsi na umma yatakuwa kwake ili kufahamu atazungumza nini kuhusu kuhusu maslahi na mustakabali wa ajira zao hasa kuongeza kima cha chini cha mshahara katika sekta ya umma na ile ya sekta binafsi na kupandisha madaraja wafanyakazi wa umma.

Jambo lingine ambalo litaibua mjadala katika sherehe hizo ambazo zinazofanyika kila mwaka ni nyongeza ya mishara kwa watumishi wa umma na kupungua kwa kiwango cha kodi katika mishahara (PAYE) ambacho kwa sasa ni asilimia tisa kilichoanza mwaka wa fedha wa 2016/17.

Mwaka jana sherehe za Mei Mosi hazikufanyika ili kuepusha mikusanyiko ya watu, ikiwa ni hatua muhimu ya kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona (Covid-19).

Rais aliyekuwepo Hayati Magufuli  alitoa ujumbe wake kupitia Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu akisema Serikali inatambua mchango mkubwa unaotolewa na wafanyakazi katika ujenzi wa Taifa na itaendelea kusimamia maslahi yao na kuboresha mazingira ya kazi.

Hata hivyo, hakuzungumzia suala la nyongeza ya mishahara ambalo limekuwa likipigiwa kelele na wafanyakazi kwa muda mrefu ili kupata vipato vitakavyokidhi mahitaji ya familia zao. 

Lakini mwaka 2019, Hayati Dk Magufuli aliwaahidi wafanyakazi kuwa angeowaongezea mishahara kabla ya kuondoka madarakani mwaka 2020 lakini hakutimiza ahadi hiyo mpaka umauti unamfika. 

“Katibu Mkuu wa Tucta (Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi Tanzania) amenikumbusha kuhusu ahadi yangu niliyoitoa mwaka jana wakati sherehe kama hizi zilifanyika Iringa kwamba kabla sijaondoka madarakani nitaongeza mshahara. Hilo ni kweli kabisa! Nilitoa ahadi hiyo lakini ni lazima tuelewe hadi sasa sijaondoka madarakani,” alisema Rais Magufuli katika sherehe za Mei Mosi 2019 zilifanyika mkoani Mbeya. 

Wafanyakazi wakiwa wameshikana mikono huku wakiimba wimbo wa mshikamano katika kilele cha maadhimisho ya sikukuu ya Wafanyakazi Duniani Mei Mosi iliyofanyika katika uwanja wa Sokoine jijini Mbeya mwaka 2019. Picha| Michuzi. 

Haenda Rais Samia akafufua matumaini ya wafanyakazi katika hotuba yake atakayoitoa Mei mosi ya mwaka huu kama inavyosubiliwa kwa hamu na wafanyakazi mbalimbali nchini. 

Mwalimu Isack Edson aliyepo mkoani Mbeya amesema anaamini Mama Samia atasikiliza kilio chao cha muda mrefu cha kuboreshewa maslahi na atafanya kitu ambacho kitawapa matumaini ya kufanya kazi kwa bidii.

“Tumekaa muda mrefu bila kuongezea mishahara, na pia mazingira ya kazi siyo rafiki, nadhani huyu ni mama atalifikiria hili na kuongeza mshahara mwaka huu,” amesema mwalimu huyo wa shule moja ya sekondari mkoani humo. 


Soma zaidi: 


Viongozi wa wafanyakazi watoa mwelekeo

Rais wa Shirikisho la wafanyabiashara Tanzania (TUCTA),  Tumaini Nyamhokya amesema wamepata kibali cha kufanyia sherehe ya Mei Mosi Jijini Mwanza na kuwataka  wafanyakazi wote kujitokeza kwa wingi katika sherehe hizo. 

“Hili litakuwa ni tukio la kwanza kubwa kwa Rais Samia kukutana na wafanyakazi  na kuzungumza  nao hivyo wana imani naye kuwa ataweza kuzisikia na kuzifanyia kazi changamoto zilizopo kwa wafanyakazi wa hapa nchini,” amesema Nyamhokya jana April 13 jijini Mwanza. 

Amesema wafanyakazi wana imani  na rais na kuwa wajitokeze kwa wingi siku  hiyo ili kudhihirisha upendo  na imani  waliyonayo kwake. 

Mwenyekiti wa wafanyakazi wa sekta ya mawasiliano na uchukuzi Kanda ya Ziwa, Wambura Mtani ameelezea sherehe hizo zitaleta fursa kwa wafanya biashara kufanya shughuli zao vizuri kutokana na wingi wa watu lakini wafanyakazi kupata matumaini mapya. 

Amesema changamoto ambayo wanapigania siku zote ni kuona wafanya kazi wakipata stahiki zao kwa wakati na za kuridhisha ili waweze kupata maendeleo  yao na Taifa.

Habari hii imeandikwa na Mariam John na Daniel Samson