October 7, 2024

Madaraka aliyokuwa nayo Mengi nje ya makampuni ya IPP

Madaraka hayo aliwahi kuyashika katika taasisi za umma na binafsi ikiwemo taasisi ya sekta binafsi Tanzania (TPSF) ambako alionyesha umahiri mkubwa wa uongozi.

  • Madaraka hayo aliwahi kuyashika katika taasisi za umma na binafsi ikiwemo taasisi ya sekta binafsi Tanzania (TPSF). 
  • Madaraka hayo aliyapata kutokana na uwezo wa kuongoza watu kwa hekima na busara. 

Dar es Salaam. Licha ya marehemu Dk Reginald Mengi kuwa mwanzilishi na Mwenyekiti Mtendaji wa makampuni ya IPP, siku za uhai wake alifanikiwa kushika madaraka katika taasisi zingine ambazo zinaendelea kuenzi mchango alioutoa wakati wa uongozi wake. 

Mengi aliyekuwa moja ya watu matajiri na mashuhuri nchini Tanzania alifariki dunia usiku wa kumkia Mei 2, 2019 akiwa mjini Dubai, Falme za Kiarabu.

Akizungumza wakati wa kuaga mwili wa marehemu leo (Mei 7, 2019) katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Salum Shamte amesema taasisi yake inamkumbuka Dk Mengi kwa kukubali madaraka ya kuongoza taasisi zingine mbali na makampuni yake ya IPP, jambo lililotoa fursa ya watu wengine kufaidika na mawazo na uongozi wake. 

Mengi alikuwa mmoja wa waasisi walioratibu uanzishwaji wa taasisi ya sekta binafsi Tanzania (Tanzania Private Sector Foundation- TPSF) ambayo alikuwa Mwenyekiti wake kutoka mwaka 2013 mpaka mwaka jana na alipoendelea kuwa mjumbe wa bodi mpaka kifo chake.

Kwa mujibu wa Shamte, Mengi aliwahi kuwa Mwenyekiti wa zamani wa Baraza la Afrika Mashariki la Biashara (East Africa Business Council) ambapo TPSF ni taasisi mwakilishi hapa nchini. 

“Kwa wengi wetu mtakubaliana nami kwa asili Dk Mengi ni mtu wa asili ya unyenyekevu ingawaje hakua mtu wa kukata tamaa wala hakua muoga wa kujaribu mambo mapya,” amesema Shamte.

Rais John Magufuli akitoa salamu za mwisho kwa mwili wa marehemu Mengi katika ukumbi wa Karimjee mapema leo (Mei 7, 2019). Picha|Michuzi.

Pia aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Chama cha wa Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT) tangu kilipoanzishwa mpaka mauti yanamkuta. Katika uongozi wake alisaidia kuimarisha na kuendeleza uhuru wa vyombo vya habari nchini. 

Hakubaki nyuma katika kuwasaidia watu wenye ulemavu ambapo alianzisha taasisi yake inayojihusisha na masuala ya watu wenye ulemavu (Dk Reginald Mengi Persons with Disabilities Foundation) yenye lengo la kuwatambua na kuwawezesha watu wenye ulemavu wajione kama wanaweza. 

“Sisi watu wenye ulemavu Dk ametuachia taasisi ya Dk Mengi Foundation, wakati tunaendelea kulia tuangalie tunavyoweza kuwasaidia watu wenye ulemavu katika taasisi hii na kuwasaidia kupitia taasisi zao tupate ukombozi,” amesema Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Walemavu Tanzania (Shiwavata), Ummy Hamis  wakati akitoa salama zake leo.

Kutokana na umahiri wake wa uongozi, Mengi aliwahi kuwa Mwenyekiti wa kwanza wa  Shirikisho la wenye Viwanda Tanzania (CTI) lililoanzishwa mwaka 1991 ambaye alikuwa mstari wa mbele katika uanzishwaji wa viwanda nchini. 

“Na sisi kama CTI, mimi ni Mwenyekiti wa sita tumempoteza mwenyekiti wa kwanza ambaye ni ndugu yetu, tumeumia lakini hapa hapa tujifunze watanzania wengi wana nafasi kama yeye au zaidi tuwe tuna roho ya kutoa na kusaidia kama aliyokuwanayo yeye,” amesema Mwenyekiti wa sasa wa ICT, Subhash Patel.


Soma zaidi:


Uongozi katika mashirika ya umma

Mengi amewahi kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Taifa La Mazingira Tanzania (NEMC); Mwenyekiti wa Vyombo vya habari vya Jumuia ya Madola Tanzania  (CPU)); Mkurugenzi wa bodi ya LEAD (Leadership for Environment and Development International); Kamishna wa Tume ya Ukimwi Tanzania (TACAIDS).

Pia amewahi kuwa katika nafasi kadhaa za uongozi wa umma ikiwa ni pamoja na Mwenyekiti wa magazeti Tanzania (Chairperson of Tanzania Standard Newpapers); Kamishna wa kamati inayoshughulikia mishahara (Commissioner of Salary Review Commission); Mwenyekiti wa bodi ya Wahasibu na Wakaguzi Tanzania(NBAA)

Nafasi nyingine ni kuwa Mwenyekiti wa ICC Tanzania (National Committee of the Intenational Chamber of Commerce); na Mkurugenzi wa Bodi Ya Baraza la Biashara la Jumuiya ya Madola. 

Katika taasisi zote alizopita Mengi ameacha alama muhimu ya utu na unyenyekevu katika kuwaongoza watu kuelekea mafanikio ya kweli.