October 6, 2024

Madeni ya umeme yanavyoikwamisha Zanzibar

Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) limetakiwa kushughulikia changamoto za madeni ya ndani ili kuboresha upatikanaji wa umeme visiwani humo.

  • Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) limetakiwa kushughulikia changamoto za madeni ya ndani ili kuboresha upatikanaji wa umeme visiwani humo. 
  • Hatua hiyo inakuja siku moja baada ya Baraza la Mawaziri la Tanzania kuridhia utozwaji wa VAT kwa kiwango cha asilimia zero kwa umeme unaouzwa kwa shirika hilo. 

Dar es Salaam. Wakati Baraza la Mawaziri likiridhia utozwaji wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa kiwango cha asilimia sifuri kwenye umeme unaouzwa na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kwa Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO), limeshauriwa kushughulikia changamoto za madeni ya ndani ili kuboresha upatikanaji wa umeme visiwani humo. 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu jana (Januari 21, 2019), mbali na kufuta VAT kwa asilimia zero, Baraza hilo liliridhia kufuta deni la kodi hiyo linalofikia Sh22.9 bilioni la umeme uliouzwa kwa Zeco.

Akizungumza baada ya kikao hicho, Rais Magufuli alisema baada ya kufanya uamuzi huo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango atawasilisha marekebisho madogo ya sheria ya VAT, sura ya 148 kupitia sheria ya fedha ya mwaka 2019 ili umeme unaouzwa Tanzania Zanzibar utozwe VAT kwa kiwango cha asilimia sifuri.

“Kwahiyo madeni yatakayokuwa yanadaiwa kwa Zanzibar ni yale madeni ya kulipia umeme, umeme wametumia kiasi fulani wanalipa kama wanavyolipa wa maeneo mengine kwa mfano wanavyolipa Dar es Salaam, suala la kutoza VAT sasa halipo,” alisema Rais.


Zinazohusiana:


Uamuzi huo huenda ni suluhisho la madeni yanayoikabili ZECO ambapo Machi 5, 2016, Rais Magufuli aliiagiza Tanesco kuwakatia umeme wateja wote wenye madeni makubwa kwa kampuni hiyo ikiwemo Zecoambayo ilikuwa deni la Tanesco kiasi cha Sh121 bilioni.

Licha ya ZECO kusamehewa madeni yake ya VAT, bado itakuwa na kibarua kingine cha kutatua changamoto za malimbikizi ya madeni kutoka taasisi za ndani ambazo zimekuwa zikipata umeme kutoka shirika hilo. 

Changamoto hizo huenda zimekuwa kikwazo pia kwa ZECO kukidhi mahitaji umeme kwa wananchi kutokana na gharama kubwa za uendeshaji ambazo zinachangiwa na taasisi hizo kutokulipa fedha kwa wakati. 

Upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa wananchi wa Zanzibar utachchochea shughuli za maendeleo ikiwemo uzalishaji mali na kuwaondolea umaskini wa kipato. PIcha|Dar24.

Kwa mujibu wa ripoti ya Kamati ya Ardhi na Mawasiliano ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar kwa mwaka wa fedha 2017/2018 iliyotolewa Februari 2018 inaonyesha kuwa Hadi kufikia Disemba 2017, madeni ya wateja kwa upande wa Unguja yalikuwa  zaidi ya Sh15.3 bilioni.

Madeni hayo ni ya taasisi za Mamlaka ya Maji Zanzibar (Zawa), Taasisi nyingine za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) na Serikali ya Muungano ya Tanzania. 

Kwa upande wa Pemba madeni makubwa ya baadhi ya taasisi za Serikali hadi kufikia Disemba, 2017 yalikuwa Sh4.4 bilioni. 

Hali hiyo imekuwa ikiathiri uboreshaji wa miundombinu na miradi ya umeme katika makazi ya watu na maeneo ya uzalishaji. 

“Uchakavu wa nguzo za umeme hali inayopelekea wananchi kukosa huduma muhinu ya umeme katika maeneo mengi ya Unguja na Pemba,” imeeleza sehemu ya ripoti hiyo. 

Kushughulikiwa kwa changamoto hizo kutasaidia kutanua wigo wa kuwafikia wananchi wengi kwa nishati, wakati huu ambao Zanzibar imeanza mchakato wa utafiti na utafutaji wa mafuta na gesi asilia ambayo yatasaidia kuchochea shughuli za uchumi na kupunguza utegemezi umeme kutoka Tanzania bara.