Madhara ya uvuvi wa mabomu yanavyoendelea kutafuna wengi
Sekta nyingine kama utalii na biashara zimeathiriwa kwa kutokana na uvuvi wa mabomu huku baadhi ya wavuvi haramu walifariki na kupata vilema.
- Baadhi ya wavuvi haramu walifariki, kupata vilema kwa sababu ya kutumia mabomu.
- Uharibifu wa matumbawe umesababisha bei ya samaki kupaa.
- Sekta nyingine kama utalii na biashara zimeathiriwa kwa kutokana na uvuvi wa mabomu.
Dar es Salaam. Miezi kadhaa baada ya operesheni kali ya kutokomeza uvuvi wa mabomu katika ukanda wa pwani ya Bahari ya Hindi, madhara ya uvuvi huo haramu yanaendelea kutesa wengi licha ahueni kidogo kuanza kutokea.
Miaka mitatu iliyopita uvuvi huo ulikuwa umeshamiri katika ukanda huo baada ya baadhi ya wavuvi kuamua kutumia vilipuzi baharini kinyume na taratibu ili kupata samaki wengi kuongeza kipato.
Jambo ambalo wengi walikuwa hawafahamu ni kwamba mbali na vitendo hivyo kuathiri afya na mazingira, madhara yake yameendelea kuitafuna sekta ya uvuvi na nyingine zinazotegemea mazao ya bahari kama utalii na biashara huku baadhi ya wavuvi hao wakibaki vilema.
Uchunguzi uliofanywa na Nukta, Septemba mwaka huu (2018) ulibaini kuwa pamoja na Serikali kudhibiti uvuvi huo wa kutumia mabomu kwa asilimia 85, kiwango cha upatikanaji wa samaki bado kilikuwa hakijaimarika kama awali, bei ya vitoweo hivyo ipo juu kutokana na kuadimika sokoni na wafanyabiashara wanahaha kupata wateja.
Baadhi ya wavuvi wameeleza kuwa uvuvi wa mabomu umesababisha samaki kutopatikana kwa wingi huku aina nyingine za samaki zikipatikana kwa nadra akiwemo Sehewa ambaye huenda akapatikana mara moja kwa mwaka.
Ramadhan Almasi (40) mvuvi wa kijiji cha uvuvi cha Minazi Mikinda Jijini Dar es Salaam anasema kwa sasa kumpata samaki aina ya kolekole ni kama “umeokota almasi”.
“Bunusi ambao wanapenda sehemu iliyotulia, tangia wavuvi waanze kutumia mabomu wamejisogeza mbali,” anasema Almasi ambaye amekuwa akifanya shughuli za uvuvi kwa miaka 21 sasa.
Muuza samaki wa Mbagala Rangi 3, Richard Mmbaga (32) aliyefanya biashara kwa miaka mitano anasema jodari, change, kolekole na vibua ni “samaki wanao patikana kwa manati”.
Wakati mwingine samaki huadimika sokoni, jambo ambalo huleta sintofahamu kwa akina mama waliojiajiri kukosa samaki wa kuuza mtaani. Picha| Gettyimage.
Uhaba huu wa samaki umesababisha biashara ya samaki kutofanya vyema ikizingatiwa wengi wanaokaa ukanda wa Pwani hutegemea sekta hiyo kama moja ya njia ya kujiingizia kipato. Baadhi ya wachuuzi wameeleza kuwa wananunua samaki wanaovuliwa kutoka nje ya nchi wakiwemo vibua ili kumudu mahitaji.
“Samaki wangekuwepo, ungekuta hili soko limechangamka. Sasa hivi samaki hamna ndiyo maana unaona kupo kimya,” anasema Ali Waziri (48) mvuvi na mkazi wa Kunduchi.
Wakati wanahabari wetu wanatembelea soko la Kunduchi mwishoni mwa Septemba mwaka huu, akina mama walikuwa wamekalia ndoo zao pasi na matumaini ya kufanikisha kupata samaki wa kwenda kuuza kwenye vijiwe vyao.
Kutokana na ukosefu wa samaki uliochochewa na kuharibiwa kwa mazalia ya viumbe hao, wale wanaopatikana huuzwa kwa bei ya juu kwa jumla na rejareja.
Samira Mohamed (26) mkazi wa Kunduchi anasema ina walazimu yeye na wenzake wanne kuchanga kiasi cha Sh20,000 ili kununua ndoo ya samaki inayo gharimu Sh80,000.
“Enzi samaki wapo ilikuwa raha sana na tulikuwa tunanunua ndoo moja kwa Sh40,000 tu. Sasa hivi tunachanga wanne kununua ndoo ya Sh80,000 na faida unapata kidogo,” anasema Samira.
Uhaba wa samaki unawatesa hadi mama ntilie ambao ili kupata faida kidogo baadhi yao wameamua kumkata samaki katika vipande viwili badala ya kumweka mzima kama ilivyo kuwa awali.
Zinazohusiana:
- Njia zilizotumika kufyekelea mbali uvuvi wa mabomu Dar
- Mpina apania kujenga viwanda vya samaki, nyama nchini
- Ripoti Maalum: Mbinu za kubaini samaki waliovuliwa kwa mabomu
Mbali na kugawa vipande, baadhi ya magenge ya kuuza chakula cha haraka kuuza yanauza samaki kwa bei ya juu ukilinganisha na nyama na vitoweo vingine na kuwafanya wasio na kipato kikubwa kutomudu.
Mama ntilie na wauza chips wanaeleza kuwa kwa sasa samaki zimekuwa kitoweo kisichokimbiliwa kirahisi na wateja kama awali.
“Wateja wengi wakija huuliza samaki lakini nikiwaambia nauza Sh2,500 huulizia chakula kingine,” anasema Mama Tina ambaye ni muuza chakula katika mtaa wa Mpakani, Mwenge Jijini hapa.
Wengi waliofika katika mgahawa wa Mama Tina, uliokuwa umefurika wanafunzi, wafanyakazi na kina mama, waliagiza ugali nyama, wali nyama, ugali dagaa na ni wateja wawili tu kati ya 10 waliagiza wali samaki.
“Zamani watu wengi wangekuwa wameagiza samaki lakini kwa sasa wengi hawali na ukinunua idadi kubwa ya samaki wanalala unaishia kupata ‘shoti’ (hasara),” anasema Mama Tina akionekana kutoridhishwa na biashara hiyo.
Chama cha Uhifadhi Wanyamapori Duniani (WCS) kinaeleza kuwa uvuvi wa mabomu unatishia soko la samaki nchini, utalii wa kuogolea na ni hatari kwa usalama wa Taifa.
Wataalamu wa viumbe wa baharini wanaeleza kuwa uhaba wa samaki unaoendelea kwa sasa hauhusiani na msimu wa hali ya hewa baharini bali matumizi ya mabomu yaliyokuwepo na kuathiri matumbawe ambayo ni muhimu katika kuongeza mazalia ya samaki.
Baada ya mabomu kupigwa, matumbawe hayo huharibika na baadhi ya viumbe bahari ambao husalimika katika kadhia hiyo kama samaki hulikimbia eneo hilo na kwenda mbali zaidi ambapo siyo rahisi kwa mvuvi mwenye vifaa duni kuwavua.
“Viumbe vingi vya baharini hutegemea matumbawe kwa sababu wanapata chakula na hifadhi. Pia, ‘mangrove’ (miombo) ambazo ni chakula kwa samaki huweza kuharibika kwa sababu ya mabomu yanayopigwa na wavuvi haramu,” anasema John Mchiwa, Profesa wa Sayansi ya Viumbe wa Majini na Uvuvi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Ili matumbawe hayo kurudi katika hali yake ya kawaida na kuzalisha samaki kwa wingi, huchukua muda mrefu na kuacha wavuvi wakilia na ukame na walaji wa samaki wakihaha kupata kitoweo hicho katika afya ya mwanadamu.Baadhi ya wavuvi wanasema uvuvi wa mabomu umepunguza kasi ya watalii waliokua wakitembelea Kigamboni na kupiga mbizi ili kuangalia viumbe baharini kwasababu mazalia ya samaki yakiwemo matumbawe yameharibiwa sana. Picha| Shutterstock_
Afisa Miradi wa Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi na Bahari wa Mfuko wa Wanyamapori Duniani (WWF), Lydia Mwakanema anasema tafiti zinaonyesha kuwa mwamba wa matumbawe, ambao samaki hupenda kuwepo kwa sababu ya chakula na mazalia, huchukua takriban miaka 100 ili kufikia urefu wa nchi moja.
“Sasa kitu ambacho kimekua kufikia nchi moja kwa miaka 100 ukikiharibu unaweza ukatafakari kwamba madhara yake yanakuwa ni makubwa namna gani. Kwa hiyo kurudishia yale maeneo ambayo yamepigwa na mabomu katika hali yake ya awali inachukua muda mrefu sana,” anasema Mwakanema na kuongeza:
“Wakati mwingine ni kama haiwezekani na hasa kama maeneo ambayo ni miamba ya matumbawe.”
Mmoja wa wavuvi wa Kigamboni ambaye hakutaka kutaja jina lake anasema uvuvi wa mabomu umepunguza kasi ya watalii waliokua wakitembelea Kigamboni na kupiga mbizi ili kuangalia viumbe baharini.
“Zamani walikuwa wanakuja watalii wengi hapa kuja ‘kudive’ (kuzamia) kuangalia samaki chini ya bahari lakini kwa sasa mabomu yamewafukuza. Watalii wengi wamesitisha kwa kweli siyo kama zamani,” anasema.
Mbali na kuathiri viumbe bahari na mazingira, mabomu yanayotumika kuvulia yameathiri hadi wavuvi wenyewe wakiwemo baadhi kufariki au kujeruhiwa viungo na kubaki na vilema.
“Baadhi wamefariki dunia na wengine wamekatika mikono. Hata mimi kidole hiki hakikutika na mapanga ila ilitokea wakati wa kurusha bomu baharini kwa bahati mbaya sikuona kama limewaka, sasa katika kujitetea likanikata kidole,” anasema Omary Mussa Omary, mvuvi wa Kimbiji jijini hapa ambaye alijisalimisha kwa mamlaka na kuachana na uvuvi huo.
“Nilisikia uchungu sana baadhi ya wavuvi wenzangu walinikimbia wengine majasiri walibaki kwa sababu ni kiongozi wao wakanichukua wakanipeleka hospitali…baadaye niliendelea na tiba za sirisiri kwa kuwa ajali ilitokana na kazi haramu,” anaongeza.
Lindsey West, Mkurugenzi wa Sea Sense, taasisi inayojihusisha na uchunguzi wa samaki na viumbe bahari anaesema kuwa ni vigumu sana kuwafikia watu waliopata madhara hayo kwani shughuli nyingi za aina hiyo hufanyika kwa siri na ni vigumu kuwafikia waathirika.
Omary Mussa Omary, mvuvi wa Kizito Huonjwa halmashauri ya Kigamboni ambaye alikatika kidole kimoja cha mkono wa kulia wakati akirusha bomu baharini. Kwa sasa ameachana na uvuvi wa mabomu. Picha| Daniel Samson.
Msako mkali wa wavuvi haramu waendelea
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema uvuvi wa mabomu kwa kiasi kikubwa umedhibitiwa jijini humo kutokana na kuwepo kwa doria mbalimbali zinazofanywa baharini na kuwakamata wanaohusika na shughuli hizo.
“Ila sasa ni kimya hakuna uvuvi wa aina hiyo, kama kuna uvuvi wa namna hiyo watoe taarifa mapema ili michakato ifanyike na kuwakamata,” anasema Kamanda Mambosasa.
Hata hivyo, amesema wanaendelea kufanya doria na kutoa elimu kwa wavuvi na wananchi kuachana na uvuvi wa mabomu kwasababu sio endelevu na siyo salama kwa afya ya binadamu.
Mkurugenzi wa Uvuvi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Emmanuel Bulayi anasema opresheni maalum iliyoendeshwa na kikosi kazi maalum kijulikanacho kama (Multi Agency Task Team) kimesaidia kupunguza uvuvi wa mabomu katika ukanda wa pwani kwa asilimia 85.
“Kwasasa tunaona samaki wanaanza kupatikana tena kwa viwango vizuri na bei nzuri na tunategemea sekta itakuwa zaidi ya asilimia nne. Awali sekta ilikuwa inakuwa kwa asilimia mbili hadi 2.5, na samaki walikuwa hawapatikani, wakina mama walikuwa wanakaa feri bila kupata samaki,” anasema na kuongeza;
“Nawashauri wananchi wafuate sheria na waache uvuvi haramu, hakuna atakayebakia…yeyote atakayefanya uvuvi haramu awe nyumbani kwake au baharini tutamfikia.”
Ripoti hii maalum imeandaliwa na Nuzulack Dausen, Daniel Mwingira, Rodgers George, Daniel Samson, Tulinagwe Malope na Zahara Tunda.