Maeneo ya kutembelea sikukuu ya Eid
Ni pamoja na sehemu za fukwe na migahawa ili kukutana na marafiki kubadilishana mawazo.
- Ni pamoja na sehemu za fukwe na migahawa.
- Pia unaweza kukubali au kuitisha mwaliko kwa jirani, ndugu na jamaa.
- Sikukuu inapendeza pale unapotengeneza tabasamu kwa wengine.
Dar es Salaam. Kila mtu ana namna yake anayopenda kusherehekea sikukuu yake. Wapo ambao hutumia siku hizi kama mapumziko na hivyo kupenda kukaa na familia zao wakifurahia mahanjumati na vinywaji kwa pamoja.
Lakini pia wapo ambao huamua siku hiyo kuwa siku ya kuiweka familia pamoja yani mama asiguse mwiko wala sufuria na badala yake, familia nzima itoke ikavinjari mbali na mazingira waliyoyazowea.
Kama wewe mpango wako ni kwenda mbali na nyumbani, makala hii itakupatia sehemu kadha wa kadha za kwenda ili kufurahia na familia yako.
Kama wewe unakaa nyumbani, siyo mbaya ukasoma kwa ajili ya sikukuu ijayo. Utembelee wapi na kwanini?
Tembelea sehemu za maduka makubwa (malls)
Sehemu hizi ni maarufu kwani huwa na machaguo mengi ya sehemu za chakula. Mathalani kwa Dar es Salaam, malls huwa na seheu za kula ambazo zimejipambanua kwa namna tofauti.
Zipo sehemu zinazoandaa kuku wa aina yake, wengine ni samaki na wengine ni chakula cha Kitanzania.
Katika sehemu hizi, uzuri ni kuwa zina maeneo ya watoto kucheza ambazo pia zina waangalizi hivyo hautopata tabu na watoto wako.
Hata hivyo, inabidi uwe na pochi iliyoshiba kwani kauli za “baba au mama nataka ile” zinaweza kuwa nyingi.
Sikukuu ni muda muafaka wa kutafakari na kupata muda wa kupumzika sehemu nzuri. Picha| K15 Photos.
Fukwe na sehemu za kuogelea
Kwa sikukuu, ni muhimu kufanya mambo tofauti. Licha ya kuwa siku zingine mnatembelea fukwe lakini katika sikukuu, kutembelea fukwe na sehemu za kuogelea huwa tofauti.
Mbali na kufurahia uwepo wa watu wengine, ni nafasi ya kukutana na marafiki wapya, kuonana na jamaa ambao mmepotezana na kuongeza mtandao wa mawasiliano.
Endapo utanenda na familia yenye watoto wadogo, ni muhimu kuwaweka karibu na kuwasimamia ili wasipotee au kudhurika.
Mfano wengine wakifika sehemu, huwekeana sehemu ya makutano na muda wa kukutana na kisha kutawanyika. Hilo ni kwa watu wazima lakini kwa watoto, inashauriwa uwe nao karibu.
Kubali au hitisha mwaliko
Sikukuu inapaswa kuwa siku iliyojaa furaha. Kama furaha yako ni kuona tabasamu kwa watu wengine, ni vyema kufikiria kuwaita wadau wengine kufurahi na wewe. Rafiki, ndugu na majirani zako.
Ni fursa ya wewe na jirani yako kupata la kuongelea mbali na salamu za asubuhi na za jioni pale mnapokutana kwa bahati mbaya.
Ni fursa ya kumpatia mtoto wako nafasi ya kujenga urafiki mapema na watu walio karibu naye na kupata mtu salama wa kucheza naye na hata kushirikiana kimasomo kwa siku zijazo.
Pale unapopata mwaliko, jitahidi kwenda au kutoa taarifa ya kutokuenda mapema. Unapokaa kimya, unaiacha familia ya watu njia panda.
Mbali na yote, unaweza kutumia sikukuu yako kwa kusaidia wale wasio na uwezo na wenye mahitaji maalumu. Kama una uwezo, unaweza kutembela familia za watoto yatima, wazee, wajane na wengine ambao sikukuu kwao ni kama siku zingine na kuwabadilishia mtazamo huo.
Mimi mwandishi wako sijapata mwaliko bado. Siyo mbaya na mimi ukanikaribisha ili tuchinje pamoja. Kwenye suala la msosi, sitokuangusha.