July 6, 2024

Maeneo ya wapigania uhuru wa Afrika kuundiwa sheria kuvutia watalii

Serikali ya Tanzania iko katika mchakato wa kuandaa sheria ya kulinda na kuhifadhi maeneo yaliyotumiwa na wapingania uhuru wa nchi za Kusini mwa Afrika yanayopatikana nchini ili yatumike kwa shughuli za utalii wa utamaduni na historia.

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza  akiangalia handaki lililotumiwa na Rais wa kwanza wa Msumbiji, Samora Mashel lililopo wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma wakati akitembelea maeneo ya historia ya Ukombozi wa Afrika. Picha|Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.


  • Serikali yasema iko kwenye mchakato wa kulinda na kuhifadhi maeneo hayo kisheria.
  • Pia yatatumika kwa shughuli za utalii wa utamaduni na historia.
  • Programu ya uhifadhi na uendelezaji wa historia ya ukombozi wa Afrika nayo inatekelezwa.

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania iko katika mchakato wa kuandaa sheria ya kulinda na kuhifadhi maeneo yaliyotumiwa na wapingania uhuru wa nchi za Kusini mwa Afrika yanayopatikana nchini ili yatumike kwa shughuli za utalii wa utamaduni na historia. 

Imesema inaendelea kubainisha maeneo yaliyotumiwa na wapingania uhuru wa nchi za Kusini mwa Afrika ambayo yanasimamiwa na programu ya urithi wa ukombozi wa Afrika iliyopo chini ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Naibu Waziri wa wizara hiyo, Juliana Shonza aliyekuwa akizungumza katika ziara ya kikazi Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma amesema maeneo hayo ni kumbukumbu muhimu inayotakiwa kuendelezwa ili itumike kwa manufaa ya wananchi na Taifa.

“Lengo kubwa ni kuhakikisha maeneo haya yanalindwa kisheria ili yaweze kutumika kama vivutio vya utalii wa kiutamaduni pamoja na utalii wa kihistoria kwa sababu huu ni urithi muhimu wa historia nzuri ya nchi yetu, haya ni maeneo yaliyotumika kusaidia ukombozi wa Nchi za Kusini mwa Afrika” amesema Shonza.  

Katika kutekeleza programu ya uhifadhi na uendelezaji wa historia ya ukombozi wa Afrika, Wizara inakarabati jengo lililokuwa la kamati ya ukombozi ya iliyokuwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) ambayo kwa sasa ni Umoja wa Afrika (AU).

Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara hiyo, kazi nyingine ambazo Serikali imekamilisha ni uandaaji wa tovuti ya programu, ubainishaji wa maeneo yaliyotumika wakati wa harakati za ukombozi.

“Utambuzi wa nyaraka na vitu mbalimbali vinavyohusiana na harakati hizo pamoja na kufanya mahojiano na watu walioshiriki au kushuhudia harakati za ukombozi wa Afrika ambayo yamehifadhiwa kwa njia ya kidijitali,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.


Zinazohusiana:


Kongwa kitovu cha utalii wa historia ya ukombozi wa Afrika

Mji wa Kongwa, kihistoria ni kitovu cha harakati za Ukombozi wa Afrika kwani harakati zote za mapambano ya kutafuta uhuru zilianzia Kongwa na baadaye zikaendelea katika maeneo mengine nchini kama sehemu ya kupanua wigo wa harakati hizo na huduma kwa wapigania uhuru.

Mkuu wa wilaya hiyo, Deogratius Ndejembi amesema eneo hilo lilitumika kwa ajili ya mafunzo kwa wapigania uhuru ambapo kwa sasa lina vielelezo muhimu vya kihistoria likiwemo handaki alilokuwa akilitumia Rais wa kwanza Msumbiji, Samora Machel, nyumba za makazi kwa wapigania uhuru, majengo ya shule ya sekondari Kongwa, eneo la mafunzo ya kijeshi, kiwanja cha ndege na makaburi ya wapigania uhuru. 

Maeneo mengine ya kihistoria ni makaburi ya mashujaa wa harakati za ukombozi ambayo jumla yake ni 11; makaburi matano ya wapigania uhuru kutoka Msumbiji, makaburi matatu ya wapigania uhuru kutoka Afrika Kusini na makaburi matatu ya wapigania uhuru kutoka Namibia.

Naibu Waziri, Shonza yupo katika ziara ya kikazi kutembelea maeneo ya historia ya ukombozi wa Afrika katika mikoa ya Dodoma, Morogoro pamoja na mkoa wa Pwani hasa Wilaya za Chalinze na Bagamoyo.