October 6, 2024

Maeneo yanayoweza kuwatoa kimaisha wabunifu wa teknolojia Tanzania

Maeneo hayo yanagusa sekta kama kilimo, fedha, mazingira, uchumi ambayo yanahitaji teknolojia rahisi kutatua changamoto cha jamii.

  • Maeneo hayo yanagusa sekta kama kilimo, fedha, mazingira, uchumi ambayo yanahitaji teknolojia rahisi kutatua changamoto cha jamii.
  • Utafiti wa mahitaji ya jamii, ubora wa bidhaa na huduma zinazotolewa na wabunifu ni msingi wa kufanikiwa.

Dar es Salaam. Unapoitaja Tanzania hutaacha kuiusisha na mabadiliko ya teknolojia yanayotokea katika shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo huduma za kifedha kupitia simu za mkononi.

Kampuni za ndani na nje ya nchi zinafanya kila jitihada kutumia fursa mbalimbali zilizopo katika teknolojia kutafuta njia za ubunifu wa teknolojia kutatua changamoto zilizopo katika jamii ili kuboresha maisha ya wananchi. 

Vijana nao hawako nyuma kuchangamkia fursa hizo ili kutengeneza ajira na kujenga msingi kwa ajili ya maisha ya baadaye. Kutoka sekta ya elimu, afya, kilimo na hata mawasiliano na uchukuzi utakutana na kampuni zinazochipukia zikitumia teknolojia kuhakikisha huduma na bidhaa zinapatikana kwa urahisi. 

Lakini siyo sekta zote zimefikiwa kikamilifu. Hata zile zilizofikiwa bado zinahitaji msukumo mkubwa wa kuboresha utendaji na mfumo wa sekta husika ili kuleta matokeo chanya kwenye jamii. 

Wadau wa teknolojia wameiambia nukta.co.tz baadhi ya sekta zinahitaji kupewa kipaumbele na zikitumiwa vizuri na wabunifu zitasaidia kusogeza mbele ajenda za Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG’s) ifikakapo mwaka 2030 ambayo kwa sehemu kubwa yanalenga kuifanya dunia kuwa sehemu nzuri ya kuishi kwa watu wote. 

Mwanzilishi wa mtandao wa Safari Wallet, Iddy John anasema sekta ya fedha ni eneo muhimu kwa wabunifu ambayo halijatumiwa vizuri ikizingatiwa kuwa pesa inaziungaisha sekta zote kwenye jamii ambazo zinatakiwa kuwa katika mfumo rasmi ili kuongeza usalama kwa watumiaji.

“Maeneo muhimu ambayo wabunifu wanaweza wakaenda pia Fintech (fedha), angalia kwamba kuna asilimia ngapi ya watu wanaiogopa benki, kuna asilimia ngapi ya watu ambao fedha zao zinapita nje ya mfumo, unawezaje kubuni vipi kumfanya mtu akaona kuna umuhimu kujumuishwa kwenye masuala ya kifedha,” anasema John. 

Anaeleza kuwa fursa nyingine inayoweza kuwatoa wabunifu wa teknolojia ni sekta isiyo rasmi ambayo inahusisha biashara na shughuli za uzalishaji mali ambazo zikitengenezewa mfumo mathubuti utakaosaidia jamii kubadilika kitabia na kuwa bora zaidi.

“Kikubwa ni kutengeneza bidhaa au huduma inayoweza kugusa jamii moja kwa moja.”

“Kama mbunifu kuna mahali lazima utaanzia kujua matatizo waliyonayo watu kuhakikisha kile unachokitengeneza kinakupatia pesa lakini kinabadilisha maisha na tabia yaani kunakuwa na mabadiliko baada ya miaka mitano unaleta kitu kipya.”

Akitolea mfano wa kasi ya matumizi ya mtandao wa WhatsApp ambao kwa sehemu kubwa umechukua nafasi ya ujumbe mfupi wa maneno (SMS) unaotumika na simu za kawaida, amesema ilitokana na wabunifu kutumia nguvu kubwa ya kubadilisha tabia za watumiaji wa simu na kuwaaminisha kuwa WhatsApp ni njia rahisi ya kuwasiliana. 

Baadhi ya sekta ambazo zimeweza kufikiwa na wabunifu kwa upana nchini ni pamoja na elimu, afya, kilimobiashara, ujarsiriamali na teknolojia. 


Soma zaidi:


Mmiliki wa mtandao wa Daily Talk, Jane Shusha anasema sekta ya kilimo nayo inapaswa kupewa kipaumbele hasa upande wa kubuni mifumo ya masoko itakayosaidia wakulima kupata tija ya mazao wanayolima. 

“Tunahitaji vijana ambao watafikiria kufanya kilimo hata kama sio cha mashamba makubwa lakini kiwe na thamani. Nafikiri kikubwa ni kuwa mbunifu,” amesema Jane.

Amesema vijana wakiongeza ubunifu na kuwa na kiu ya kuja na suluhisho la matatizo katika jamii ni rahisi kuzifikia sekta mbalimbali kwa sababu tatizo moja linaweza kuwa linagusa zaidi sekta moja ambazo zote zinaweza kuwa zinahitaji suluhisho la pamoja.

Uchafuzi wa bahari ni miongoni mwa maeneo yanayohitaji suluhisho la teknolojia ili kuhakikisha ustawi mzuri wa viumbe wanaotegemea rasilimali hiyo kuishi. Picha|Mtandao.

Mbali na wadau wa teknolojia nchini, Bilionea Bill Gates katika moja ya makala zake kwenye mtandao wa MIT Technology Review anaeleza kuwa yeye anafikiri fursa zaidi zipo kwenye usafishaji wa bahari kwa sababu kila siku takataka za plastiki zinaingia baharini na kuhatarisha afya za binadamu na viumbe wengine. 

Gates anasema bado hakuna njia iliyobuniwa mpaka sasa kuhakikisha fukwe zinakuwa safi wakati wote.

Anabainisha maeneo mengine kuwa ni pamoja na matumizi ya magari yasiyo na dereva, kutabiri matetemeko ya ardhi, kinga ya mafua na vifaa vya utunzaji wa umeme mdogo unaozalishwa na nishati jadidifu. 

Hata hivyo, John ambaye pia anamiliki mtandao wa Place Listed anasema pamoja na yote hayo, muhimu ni kutengeneza bidhaa au huduma bora zinazokidhi thamani na matarajio ya watu waliokusudiwa.