July 8, 2024

Magufuli aeleza sababu za kutoifunga Dar licha ya wagonjwa kuongezeka

Rais John Magufuli amesema licha ya jiji la Dar es Salaam kuwa na kiwango cha juu cha wagonjwa wa virusi vya Corona halitafungwa kwa sababu ni kitovu cha uchumi wa Tanzania

  • Amesema jiji hilo ni kitovu cha shughuli za uchumi zinazotegemewa na mikoa mingine.
  • Aagiza uchunguzi wa vifaa tiba vya kutibu Corona vichunguzwe. 

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amesema licha ya jiji la Dar es Salaam kuwa na kiwango cha juu cha wagonjwa wa virusi vya Corona halitafungwa kwa sababu ni kitovu cha uchumi wa Tanzania huku akiagiza baadhi ya vifaa tiba zikiwemo barakoa zinazoingia nchini kuhakikiwa kama zinafaa kwa matumizi ya Watanzania. 

Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Afya za hadi jana Aprili 21, 2020, jiji hilo lenye wakazi takriban milioni 6 lina wagonjwa 143 kati ya 284 walioripotiwa katika mikoa 17 ya Tanzania Bara.

Rais Magufuli aliyekuwa akizungumza leo (Aprili 22, 2020) na viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama mjini Chato katika Mkoa wa Geita amesema Dar es Salaam ni kituo muhimu cha ukusanyaji wa mapato ya nchi yanayotumika kuwaletea wananchi maendeleo. 

“Dar es Salaam ndiyo bandari. Kwa hiyo tuendelee kuchukua hatua lakini si kwa lockdown (kufunga) Dar es Salaam, never! (hapana),” amesisitiza Rais.

Amesema kama Dar es Salaam itafungwa, basi shughuli nyingi za uchumi na usafirishaji zinazounganisha jiji hilo na maeneo mengine zitasimama na kuathiri maisha ya watu. 

“Sasa unapofunga Dar es Salaam, ina maana Dar es Salaam wasipokee mchele, ina maana Dar es Salaam wasipelekewe viazi vya kutoka Mbeya, ina maana Dar es Salaam wasipate ndizi za kutoka Bukoba, ina maana Dar es Salaam wasifanye biashara ya kupeleka vitenge vijijini, ina maana madereva wasibebe mafuta kuyapeleka mikoani,” amehoji Rais. 

Amesema kama jiji hilo litafungwa kwa sababu lina maambukizi ya kiwango cha juu, basi na mikoa mingine inatakiwa kufungwa, jambo ambalo kwa sasa halitawezekana kwa sababu jiji hilo lina watu wengi.

Kwa muda sasa kumekuwa na shinikizo kutoka kwa watu mbalimbali hususan katika mitandao ya kijamii wakishauri Dar es Salaam ifungwe ili kuzuia maambukizi kusambaa zaidi katika mikoa mingine. 

Amewataka viongozi wa vyombo vya usalama pamoja na wizara ya afya kuendelea  kuchukua hatua za kutokomeza janga hilo la duni huku wakiwekeza nguvu katika kuwalinda raia na aina ya taarifa zinazotolewa. 


Zinazohusiana


Agusia takwimu za COVID-19

“Lakini pia taarifa zetu ziendane na ukweli hasa katika watu wanaopona, nina taarifa kwamba mpaka leo tulikuwa na wagonjwa 284 lakini naambiwa karibu 100 ya wagonjwa walishapona. Hizi takwimu za wagonjwa wanaopona nazo zitangazwe ili kuwaondolea hofu wananchi,” amesema Rais Magufuli. 

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli ameagiza Wizara ya Afya na vyombo vya ulinzi kufanya uchunguzi hasa kwa vifaa tiba zikiwemo barakoa na dawa za kuulia wadudu (Chroline) vinavyoagizwa kutoka nje ya nchi kama vinafaa kwa matumizi ya Watanzania. 

“Na ndiyo maana nimewaita viongozi wa vyombo vya usalama mfanye investigation (uchunguzi) hata katika hizo fumigation (dawa ya kupulizia wadudu) zilizokuwa zikifanywa nani alitoa maagizo. Lakini hata hizo barakoa zinazotoka nje ni lazima tujiridhishe kama ziko salama kwa Watanzania.

Amebainisha kuwa hakuna upuliziaji dawa mitaani au kwenye vyombo vya usafiri unaoweza kuua vidudu vya Corona hivyo kile kilichofanywa Dar es Salaam na kwingineko hivi karibuni ni “upuuzi”. 

Kwa mujibu wa Rais, dawa Chlorine haiwezi kuua virusi vya Corona bali bakteria au wadudu kama mende na kunguni.