November 24, 2024

Magufuli aeleza wizara ya maji ilivyomtesa miaka mitano iliyopita

Amesema katika kipindi chake cha kwanza cha uongozi wa miaka mitano, Wizara ya Maji ilimtesa sana kwa sababu miradi mingi ya maji ilikua haikamiliki kwa wakati

Rais John Magufuli leo Januari 29, 2020 amezindua mradi wa maji unaopeleka maji katika miji ya Kagongwa na Isaka mkoani Shinyanga. Mradi huo unaotoa maji Ziwa Victoria umetekelezwa kwa fedha za ndani  Sh23.1 bilioni. Picha| Msemaji Mkuu wa Serikali.


Asema miradi ilikuwa ahaikamiliki kwa wakati na hata iliyokamilika haikufikia asilimia 30.

  • Atoa maagizo mapya kwa wizara ya kukamilisha miradi ambayo haijakamilika.
  • Ataka mito itumike kumaliza shida ya maji.  

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amesema katika kipindi chake cha kwanza cha uongozi wa miaka mitano, Wizara ya Maji ilimtesa sana kwa sababu miradi mingi ya maji ilikua haikamiliki kwa wakati, huku akitoa maagizo mapya kuhusu miradi ya maji ambayo haijakamilika nchini Tanzania. 

Amesema miradi iliyokuwa inaanzishwa na wizara hiyo, utekelezaji wake ulikuwa hauzidi asilimia 30, jambo lililowafanya wananchi kuendelea kukosa huduma muhimu ya maji katika maeneo mbalimbali nchini.  

“Katika wizara iliyonitesa katika miaka mitano iliyopita ni Wizara ya Maji, miradi ilikuwa haikamiliki. Katika kipindi cha muda mrefu miradi iliyokuwa imekamilika ilikua haizidi asilimia 30 kati ya miradi iliyoanzishwa,” amesema Dk Magufuli wakati akizindua mradi wa maji unaopeleka maji katika miji ya Kagongwa na Isaka mkoani Shinyanga leo Januari 29, 2020. 

Mradi huo unaotoa maji Ziwa Victoria umetekelezwa kwa fedha za ndani Sh23.1 bilioni. 

Kutokana na miradi mingi ya maji kutokamilika kwa wakati, ameiagiza Wizara ya maji na Halmashauri zote nchini kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati kabla hajawachukulia hatua kali. 

“Nataka Waziri (wa Maji, Juma Aweso) miradi ambayo ilikuwa haijakamilika, wewe pamoja na watendaji wako mlioko ndani ya wizara na wahandisi wote katika nchi nzima wanaohusika na maji kila mmoja katika eneo lake ahakikishe miradi ambayo iko kwenye maeneo yenu inamilika. 

“Watanzania wamechoka kusubiri miradi iko kwenye visibility study (upembuzi yakinifu) na detailed design (usanifu) wakati hawapati maji. Nataka miradi ikamilike mapema ikiwezekana hata kabla ya muda lakini isiwe inazaa variation (tofauti),” amesisitiza kiongozi huyo mkuu wa nchi. 


Soma zaidi:


Amemtaka Waziri Aweso kutokuwavumiliwa wakandarasi wazembe wanaotekeleza miradi ya maji, badala yake awafukuze na wasipewe kazi yoyote nchini Tanzania.  

“Nashukuru umeanza kuchukua hatua kwa kuwafukuza wakandarasi feki kule Mwanga (mkoani Kilimanjaro), ungechelewa ningekufukuza wewe. Sasa ni vizuri uwe unawahi wale wanaokuchelewesha fukuza tu kwa sababu hawakuja huku kutangaza mambo ya mchezo, wamekuja kufanya kazi,” amesema Rais Magufuli na kubainisha kuwa,

“Ukitaka hela ya Tanzania lazima ufanye kazi. Hatuhitaji makandarasi matapeli katika nchi hii, tunataka mtu akipewa pesa za Watanzania hawa masikini akazitumie kikamilifu kwa ajili ya kukamilisha mradi.”

Aidha, ameitaka Wizara ya Maji kutumia vizuri rasilimali za mito zilizopo nchini kuwapatia wananchi maji kuachana na utaratibu wa kuchimba visima kila eneo lenye shida ya maji wakati mito inaweza kutatua changamoto hizo.