July 8, 2024

Magufuli afanya mabadiliko ya uongozi Wizara ya Maliasili na Utalii

Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu iliyotolewa leo imeeleza kuwa licha ya uteuzi huo, Dk Kijazi ataendelea kuwa Kamishna wa Uhifadhi wa Tanapa.

  • Amemteua Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) Dk Allan Kijazi kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii.
  • Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Dk Aloyce Nzuki ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo.
  • Viongozi wote walioteuliwa wanatakiwa kuwepo Ikulu Dodoma Jumatatu (Julai 20, 2020).

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amemteua Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) Dk Allan Kijazi kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii akichukua nafasi ya Dk Aloyce Nzuki ambaye ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo. 

Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu iliyotolewa leo (Julai 17, 2020) imeeleza kuwa licha ya uteuzi huo, Dk Kijazi ataendelea kuwa Kamishna wa Uhifadhi wa Tanapa.

Dk Nzuki anachukua nafasi ya mtangulizi wake Profesa Adolf Mkenda. 

Aidha, Rais Magufuli amemteua Mhandisi Anthony Sanga kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya maji akichukua nafasi iliyoachwa na Prof Kitila Mkumbo ambaye amechukua fomu ya kuomba kuteuliwa kugombea Ubunge katika jimbo la Ubunge kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Kabla ya uteuzi huo, Dk Sanga alikuwa akitumika kwenye Wizara hiyo hiyo kama Naibu Katibu Mkuu ambapo nafasi yake imechukuliwa na Mhandisi Nadhifa Kemikimba. 

Sambamba na uteuzi huo, Dk Magufuli amemteua Dk Jumanne Fikha aliyekuwa kwenye Ofisi ya Rais kuwa Mkuu wa Mkoa wa Njombe akichukua nafasi ya Christopher Ole Sendeka.

Ole Sendeka ni miongoni watia nia ambaye tayari amechukua fomu ya kuomba ridhaa ya CCM kugombea Ubunge katika jimbo la Simanjiro mkoani Arusha. 


Zinazohusiana


Katika hatua nyingine Rais amemteua Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Lindi Fadhili Juma kuwa Mkuu wa wilaya ya Geita mkoani Geita.

Kabla ya Juma, nafasi ya Mkuu wa wilaya ya Geita ilishikiliwa na Josephat Maganga ambaye amehamishwa kituo cha kazi na kuwa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma mkoani Dodoma.

Maganga anachukua nafasi ya Patrobas Katambi ambaye naye amechukua fomu ya kuomba ridhaa ya CCM kugombea Ubunge katika jimbo la Shinyanga Mjini. 

“Wateule wote wawepo Ikulu, Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 20 Julai, 2020 saa 4:00 asubuhi,” imesomeka sehemu ya taarifa ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Gerson Msigwa.