October 6, 2024

Magufuli afuta sherehe za Uhuru kwa mara ya pili

Ameagiza Sh995 milioni zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya kufanikisha sherehe hizo zitumike kujenga hospitali ya Uhuru mkoani Dodoma.

 Rais John Magufuli alishiriki kufanya usafi katika maeneo ya kuzunguka Ikulu Jijini Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya kusheherekea siku uhuru Desemba , 2015. Picha|Ikulu.


  • Rais Magufuli ameagiza Sh995.18 milioni zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya kufanikisha sherehe hizo zitumike kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya Uhuru.
  • Hospitali hiyo itakayojengwa katika eneo la kati ya barabara ya kwenda Hombolo na Chamwino katika barabara ya kwenda Dar es Salaam itakuwa inawahudumia wakazi wa mkoa wa Dodoma.
  • Wakuu wa mikoa na wilaya waagizwa kuandaa matukio ikiwemo kufanya usafi katika maeneo yao yatakayoashiria maadhimisho ya siku ya Uhuru. 

Dar es Salaam. Rais John Pombe Magufuli ameahirisha maadhimisho ya sherehe za Uhuru zilizotarajiwa kufanyika Desemba 9, 2018 na fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya kufanikisha shamrashamra hizo ameelekeza zitumike kujenga hospitali mkoani Dodoma itakayoitwa hospitali ya Uhuru.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana (Novemba 20, 2018) na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Rais Magufuli ameagiza kiasi cha Sh995.18 milioni zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya kufanikisha sherehe hizo zitumike kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo.

Waziri Mkuu ametoa taarifa hiyo wakati alipokutana na viongozi waandamizi wa mkoa wa Lindi pamoja na wilaya zake katika kikao cha maandalizi ya shughuli za kuzima Mwenge kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano kwenye ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi.

Hii ni mara ya pili kwa Rais Magufuli kuahirisha sherehe za uhuru ambapo awali alifanya hivyo Desemba 2015 mwezi mmoja tu tangu aingie madarakani. Fedha zilizotengwa aliagiza zitumike kupanua kipande cha barabara kutoka Morocco hadi Mwenge Jijini Dar es Salaam.

Pia siku hiyo ya Desemba 9, 2015, Rais Magufuli alishiriki kufanya usafi katika maeneo ya kuzunguka Ikulu Jijini Dar es Salaam hadi katika soko la samaki la feri na kueleza kuwa ni aibu kwa Taifa kukumbwa na kipindupindu kwa sababu ya uchafu.

Miaka yote Tanzania imekuwa ikiadhimisha siku kuu ya Uhuru wa Tanganyika kwa gwaride maalum la kijeshi lakini Rais Magufuli ambaye aliingia madarakani baada ya uchaguzi wa Oktoba 25, 2015 aliamua watanzania washeherekee maadhimisho ya uhuru kwa kufanya usafi ili kukabiliana na magonjwa ya mlipuko ikiwemo kipindupindu.

Katika uamuzi huu wa sasa, Majaliwa ameeleza kuwa hospitali hiyo itakayojengwa katika eneo la kati ya barabara ya kwenda Hombolo na Chamwino kwenye barabara ya kwenda Dar es Salaam itakuwa inawahudumia wakazi wa mkoa wa Dodoma pamoja na wananchi wengine watakaokuwa mkoani humo.


Zinazohusiana:


Aidha, Majaliwa amesema Rais Magufuli amewaagiza wakuu wa mikoa na wilaya waandae matukio watakayoyatekeleza katika maeneo yao yatakayoashiria maadhimisho ya siku ya Uhuru. 

“Wanaweza kutumia siku hiyo kwa kufanya usafi maeneo ya wazi au kwenye hospitali,” amesema Majaliwa.

Kufuatia maagizo hayo, Majaliwa amewataka wananchi wajiandae kufanya shughuli mbalimbali za kijamii zitakazopangwa na wakuu wao wa mikoa na wilaya kufanyika katika maeneo yao nchini.

Maadhimisho ya mwaka huu ni ya 57 tangu Tanzania Bara (Tanganyika) ipate uhuru toka kwa wakoloni wa Uingereza mwaka 1961.