November 24, 2024

Magufuli amfuta kazi bosi wa TIRA

Amteua kigogo wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) kusimamia taasisi ya udhibiti wa sekta ya bima.

Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Dk Bhagayo Saqware ambaye uteuzi wake umetenguliwa. Picha|Mtandao.


  • Amteua kigogo wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) kuchukua nafasi yake. 
  • Ni Mkuu wa Idara ya Bima katika Kitivo cha Bima na Hifadhi za Jamii cha IFM.
  • Kutenguliwa kwa Dk Saqware kunahitimisha safari ya uongozi wake TIRA tangu alipoteuliwa mwaka 2017.

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amemfuta kazi Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Dk Bhagayo Saqware huku akimteua Mhadhiri wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Dk Mussa Juma kuchukua nafasi hiyo ya kuiongoza taasisi nyeti katika sekta ya fedha na bima nchini.

Taarifa kutoka Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu iliyotolewa jana inaeleza kuwa uteuzi wa Dk Juma, aliyekuwa Mkuu wa Idara ya Bima katika Kitivo cha Bima na Hifadhi za Jamii cha IFM, ulianza 25 Juni 2019.

Kutenguliwa kwa Dk Saqware kunahitimisha safari ya miaka miwili na nusu ya uongozi wake TIRA baada ya kuteuliwa na Rais Magufuli kuiongoza taasisi hiyo Februari 2017.  


Soma zaidi: Rais Magufuli amng’oa Kichere TRA, ateua waziri mpya wa viwanda


Kama ilivyo kwa Dk Juma, Dk Saqware naye aliteuliwa kushika wadhifa huo akitokea IFM. DK Saqware alichukua nafasi ya Israel Kamuzora aliyekuwa amestaafu wakati huo.

Rais anatengua uteuzi wa Dk Saqware ikiwa ni wiki chache tu tangu ateuliwe kuwa Makamu wa Rais wa taasisi ya muungano wa vyombo vya kusimamia bima barani Afrika (AAISA).  

Dk Saqware ni moja ya vigogo wa TIRA ambao katika uongozi wao walisimamia mabadiliko makubwa ndani ya taasisi hiyo ikiwemo uanzishwaji wa mifumo ya kidijitali katika utoaji wa huduma za bima nchini.